Pages

July 30, 2018

Singida yanufaika na Miradi ya Umeme Vijijini (REA)


Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Singida Witness Msumba akiwaelewesha Wananchi wa Kijiji cha Marya juu ya kifaa cha UMETA ambacho ni mbadala wa "Wiring" ndani kwenye nyumba ndogo.


Na Grace Kisyombe - Singida

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO)  limeendelea na utoaji elimu kwa umma kuhusu  miradi ya umeme vijijini,
Akizungumzia miradi inayoendelea mkoani Singida Mhandisi Abrahmani Nyenye  ambaye ni Meneja wa TANESCO   Mkoa  wa Singida amesema, "Mkoa wa Singida una jumla ya Wateja 34, 185   ujio wa miradi ya umeme vijijini itaongeza wateja 8648 itakapo kamilika" Ambapo aliitaja miradi iliyopo ni Mradi wa uunganishaji umeme vijijini kupitia ufadhili wa Mradi wa njia ya usafirishaji umeme ya 400kV utokao Iringa hadi shinyanga (BTIP )ambao utawanufaisha wanavijiji walio pitiwa na njia hiyo ya umeme ambapo kwa mkoa wa Singida ni vijiji 39 vitanufaika na mradi huu wa BTIP .

Mradi wa pili ni ule wa REA awamu ya Pili  ambao ulipaswa uwe umekamilika lakini kwa changamoto mbali mbali mradi huu bado unaendelea katika baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Singida ,

Mradi wa tatu ni ule wa REA awamu ya Tatu ambao umeanza mnamo mwezi wa tano na utakuwa na awamu tatu zinazo tarajiwa kukamilika mnamo mwaka 2021. Akiendelea kuzungumzia miradi hii Mhandisi Nyenye alisema hadi kukamilika kwa miradi yote mitatu Jumla ya vijiji 156 vitakuwa vimepatiwa umeme.

Akihamasisha uwekezaji mhandisi Nyenye alisema Kuna maeneo ya uwekezaji kama eneo la uchimbaji dhahabu la Sekenke tayari limesha patiwa umeme kwa wawekezaji wawili , na kwa kupitia miradi hii wawekezaji ( wachimbaji wadogowadogo ) wa dhahabu pia watapatiwa huduma ya umeme kuanzia vitalu vya Sekenke 1 hadi Sekenke 5 wachimbaji wote watapatiwa umeme.
Pamoja na kuhamasisha uwekezaji Mhandisi Nyeye aliwaasa wanavijiji kulinda miundombinu ya umeme kwani Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi hii hivyo ni vema wanachi wakalinda miundo mbinu hiyo.

 Akitolea mfano eneo la Sekenke ambapo baadhi ya wananchi walianzisha machimbo katika eneo zilipo nguzo za umeme mkubwa wa 400kV , Mhandisi Nyenye alionya kuhusu kuto kufanya shughuli zozote za kibinadamu  katika njia hizo za umeme kwani ni hatari kwa maisha yao pamoja na hasara kwa Serikali kwani endapo itatokea nguzo hizo zikaanguka .

Naye bi Adelina Lyakurwa ambaye ni afisa Masoko kutoka TANESCO makao makuu, aliwahamasisha wananchi kuhusu kuchangamkia fursa hii ambapo kila mwananchi aliye katika miradi hii yote mitatu afuate taratibu za kuunganishiwa umeme kwani katika muda wa mradi mteja atalipia tshs 27,000 tu ili apatiwe huduma. Gharama ambayo ni kodi ya ongezeko la.thamani pekee.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida Mhandisi Abrahaman M.A Nyenye akitoa taarifa ya utekelezaji Miradi ya Umeme Mkoani kwake.





July 15, 2018

"TANESCO Changamkieni fursa" Naibu Waziri Nishati


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iputi, Kata ya Mbuga, Wilayani Ulanga, akiwa katika ziara ya kazi Mkoani Morogoro,


Na Veronica Simba – Ulanga

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu amewataka watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa wabunifu na kuzitumia vema fursa za kibiashara zinazojitokeza kwa kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali yenye Wateja wengi wanaohitaji huduma hiyo.

Alitoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ulanga, Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri alisisitizia kauli yake hiyo na kuwaagiza Meneja wa Kanda na Mkoa, kuandaa Mradi mdogo unaolenga kuwapelekea umeme Wananchi wa eneo hilo mapema iwezekanavyo, kabla hawajafikiwa na Mradi wa Ujazilizi.

“Nawaachia kazi hii, muandae Mradi wa kuwaletea Wananchi hawa umeme. Nimeona uwezo wa kulipa wanao na wamesubiri kwa muda mrefu sana. Wako tayari.” Alisema Mhe. Mgalu.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Mhe. Mgalu  aliwauliza Wananchi ikiwa wako tayari kupelekewa huduma hiyo na TANESCO kwa gharama ya shilingi 177,000 au wasubiri Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA) uwafikie ambao utawagharimu shilingi 27,000 tu; na kwa umoja wao walitaka wapelekewe umeme wa TANESCO kwa madai kuwa wanao uwezo wa kulipia.

Aidha, alikiri kukerwa na utendaji kazi duni uliooneshwa na Mkandarasi MBH, aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) katika Mikoa ya Pwani na Morogoro; ambapo alieleza kwamba ndiyo sababu Serikali haijampatia tena kazi.

Kufuatia suala hilo, aliwaagiza watendaji wa TANESCO, kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo na kuiwasilisha ofisini kwake Dodoma, kabla ya Ijumaa ijayo, Julai 20 mwaka huu.

“Natambua kuwa Mkandarasi husika alikwishalipwa lakini zipo fedha kidogo zilizosalia kukamilisha malipo yake. Tutafute utaratibu utakaowezesha kuhamishia fedha hizo TANESCO ili zisaidie kutekeleza Mradi wa Ujazilizi badala ya kumlipa mtu ambaye ametutia hasara kwa utendaji duni,” alisisitiza.

Pia, alitoa onyo kwa Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya Umeme Vijijini, hususan REA III, kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayeharibu kazi kwa namna yoyote.
Aidha, sambamba na onyo hilo, alisema kuwa, Serikali itamuwajibisha pia Msimamizi wa Serikali wa Mradi husika, ambaye atabainika kushindwa kumsimamia ipasavyo Mkandarasi na kusababisha kutotekelezwa kwa Mradi kikamilifu.

Maelekezo mengine aliyoyatoa Naibu Waziri katika ziara hiyo, ni kwa TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha wanaunganisha umeme katika maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kuona wananchi ambao wamepitiwa na miundombinu ya umeme, wakiishia kuangalia tu nyaya na nguzo pamoja na kuzilinda huku wao wenyewe wakiwa hawana umeme.
“Hili ni agizo kutoka kwa viongozi wetu wa juu, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli, hivyo kilichobaki ni utekelezaji wake.”

Naibu Waziri amekuwa katika ziara ya kazi kwa takribani wiki tatu, katika Mikoa mbalimbali nchini, kukagua utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi. Vijiji vingine alivyotembelea wilayani Ulanga, ambako ndiko amehitimisha ziara yake, ni pamoja na Chikwera, Kata ya Mwaya pamoja na Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi.

Baadhi ya watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi, Wilaya ya Ulanga, Ijumaa Julai 13, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga, akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kutoka kulia), Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi, wilayani Ulanga, Ijumaa Julai 13, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Sehemu ya umati wa wananchi wa Ulanga, mkoani Morogoro, wakimsiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipowatembelea Ijumaa, Julai 13 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi na kuwaeleza mikakati ya Serikali kuwapelekea umeme wa uhakika.


July 12, 2018

Dkt. Kalemani ameendelea na uzinduzi Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Tabora


Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameendelea na ziara ya uzinduzi wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Wilaya za Kaliua, Sikonge na Uyui Mkoani Tabora.

Dkt. Kalemani amezindua katika Vijiji vya Ghuliyankulu, Mbeta, Uyowa, Mkindo na Mwongozo vilivyopo Wilaya ya Kaliua.

Vijiji vingine ni Kisanga na Kanyamsenga katika Wilaya ya Sikonge.

Mheshimiwa Waziri ataendelea na ziara kesho ambapo anatarajiwa kutembelea kijiji cha Mbuyuni kilichopo Wilaya ya Uyui.


July 11, 2018

Dkt. Medard Kalemani azindua Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya III Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma



Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani, akiambatana na  Viongozi wengine wa Serikali Wilayani Kasulu na Mkoa kigoma, amezindua mradi wa umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa Vijiji 149 vya Mkoa wa Kigoma.

Kwa Mkoa wa Kigoma uzinduzi huo umefanyika katika Kijiji cha Rusesa Wilayani Kasulu.

Katika uzinduzi huo Dkt. Kalemani alitoa maagizo kwa wasimamizi wa mradi huo kwa Wilaya nne ambazo zilichelewa kupata mradi huo na kuwataka wasimamizi TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi ili ifikapo mwezi Juni, 2019 mradi uwe umekamilika.

Aidha, alitoa maagizo kwa Uongozi wa TANESCO Mkoa wa Kigoma kuanzisha Ofisi ndogo katika eneo la Rusesa kwa minajili ya kusikiliza kero za Wateja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa gharama zilizoidhinishwa na Serikali.

Pia Dkt. Kalemani aliwasisitiza Wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya umeme kwani inagharimu pesa nyingi kujengwa"Niwaombe Wananchi muitunze miundombinu itakayojengwa kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa sana kuwekeza katika miradi ya umeme". Alisisitiza.

Awali, akimkaribisha Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhingwe na ambaye pia anakaimu Wilaya ya Kasulu Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisemaWananchi wamekuwa wakiulizia kupatiwa huduma ya umeme mara kwa mara "Naamini uzinduzi huu utakuwa chachu kwa Wananchi kuanzisha Viwandavikubwa, vidogo na vya kati".






TANESCO Rukwa, NMB watembelea Gereza la Molo

Wafanyakazi wa Shirika la Usambazaji umeme ( TANESCO) Mkoa wa Rukwa wakishirikiana na Benki ya NMB wamewatembelea Maafisa wa Magereza wa Gereza la Molo lililopo Mkoani Rukwa na kutoa elimu inayohusu taratibu za kuunganishiwa huduma ya umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya Tatu.

 katika ziara hiyo, Wateja wapatao 96 ambao ni  Wafanyakazi wa Gereza hilo waliweza  kuunganishiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini  awamu ya Tatu. 

Mbali na kuunganishiwa huduma ya umeme Maafisa hao wa Magereza walipatiwa mafunzo juu ya namna ya kupata huduma, matumizi sahihi ya kutumia nishati ya umeme, usalama juu ya umeme, ulinzi wa miundombinu ya umeme na umuhimu wa kutumia umeme ili kuchochea maendeleo Nchi.

Baadhi ya Maafisa wa gereza la Molo wakisikiliza kwa makini elimu na taratibu za kupata umeme kupitia mradi wa umeme vijijini REA 3
              
Mkuu wa Gereza la Mollo ACP J.L  Mwamgunda,Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja Ndg Lucas C. Kusare na Afisa wa upimaji wakisikiliza maswali kutoka kwa Maofisa wa gereza hilo.

Afisa wa Masoko na Huduma kwa Wateja NMB benki tawi la Sumbawanga akitoa maelezo ya namna ambavyo wateja wa TANESCO wanavyoweza kutumia mfumo wa Benki yao ili kufanya malipo ya huduma mbalimbali za umeme.
Afisa Huduma na Mahusiano kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Rukwa akiwafafanulia maofisa wa Gereza la Molo juu ya utaratibu wa kupata huduma ya umeme kupitia mradi wa umeme wa REA 3

Afisa wa Gereza akiulizia utaratibu wa namna ya kupata huduma za umeme kupitia Mpango wa REA 3