Na Grace Kisyombe
Dar es salam.
Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya
kupambana na wizi pamoja na hujuma katika miundombinu ya umeme.
Akizungunza katika mkutano na Waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander L. Kyaruzi amesema Bodi ya
Wakurugenzi kupitia kamati zake imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya
kupambana na hujuma katika miundombinu ya umeme,
“Baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika kampeni maalum ya kukamata
wahujumu miundombinu ya umeme ni, Jeshi la Polisi, Takukuru, Ofisi ya
Mwendesha mashtaka wa Serikali (DPP), Idara ya Usalama wa Taifa pamoja
na wataalam wengine kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati” Amesema Dkt.
Kyaruzi
Dkt Kyaruzi aliongeza kusema kuwa, kikosi kazi hicho kitakuwa na jukumu
la kukamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanao jihusisha na wizi
pamoja na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Kikosi kazi hicho kimeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Dar e salam,
ambapo tayari watuhumiwa wanne wamekamatwa na kufikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi.
Katika hatua nyingine Dkt. Kyaruzi amewaomba wananchi na wasamaria wema
kushiriki katika kampeni hii kwa kutoa taarifa za siri ambazo
zitafanikisha kuwakamata wananchi wanao hujumu miundmbinu ya umeme.
Dkt Kyaruzi amesema kuwa kutakuwa na zawadi ambazo zitakuwa zikitolewa
kwa wale wote watakao fanikisha kukamatwa kwa watu wanao hujumu
miundombinu ya umeme.
Zawadi hizi ni za fedha tasilimu na kiwango cha zawadi hizi kitategemea
ukubwa wa mali iliyo kamatwa au kuokolewa kutoka katika hujuma hizo.
Aidha, Dkt. Kyaruzi amewakumbusha wananchi wote wenye madeni ya umeme
kulipa madeni hayo haraka kwani muda wa siku 14 ulio tolewa na Mhe
Waziri wa Nishati unakaribia kwisha, hivyo basi kuanzia Septemba 1,
2020 TANESCO itakata umeme kwa kila anaye daiwa, zoezi hili litahusu
taasisi, wafanyabiashara na watu binafsi wanao daiwa.
Pages
August 28, 2020
TANESCO yaunda kikosi kazi kupambana na wizi wa Umeme
August 27, 2020
Wafanyabiashara wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa uhujumu uchumi
Washitakiwa hao ni Ahmed Khalifa, mkazi wa Mikocheni, Abdulrazak Said na Anuary Amdani, ambao wote ni wakazi wa Temeke na Joseph Mwakabanga, mkazi wa Tandale kwa Tumbo,
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Kassian Matembele, upande wa mashitaka ulidai mnamo Julai 29, 2020 Mikocheni, Mtaa wa Ndovu Wilayani Kinondoni, washtakiwa kwa pamoja, Khalfan na Said waliingilia kwa makusudi miundombinu ya TANESCO.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujiunganisha umeme kupitia mfumo wa TANESCO na kukwepa kutumia mita, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Aidha, mnamo Agosti 7, 2020 katika Mtaa wa Magomeni Mikumi Wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, Amdani na Mwakabanga waliingilia kwa makusudi na kinyume cha sheria miundombinu ya TANESCO iliyokusudiwa kutumiwa kusambaza huduma ya umeme.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa washitakiwa hao walibadilisha mita, mali ya TANESCO kutoka kwenye nyumba inayomilikiwa na Amdani yenye deni ya shilingi 3,521,587.70 na kuweka mita mpya kwa lengo la kukwepa deni lililotajwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu mashitaka yao kwa vile mashiataka yao yanaangukia kwenye sheria ya uhujumu uchumi.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mawakili Waandamizi wa Serikali Mantenus Marandu and Wankyo Simon pamoja na Wakili wa Serikali Benson Mwaitenda umedai upelelezi wa mashauri yote mawili haujakamilika.
Baada ya kusomewa mashitaka yao, Mahakimu katika kesi zote mbili walitoa dhamana kwa washitakiwa kwa kuzingatia masharti mbalimbali.
Khalfan na Said walipewa masharti ya kupata wadhamani wawili kila mmoja ambaye angeweka dhamana ya shilingi milioni 5 na Kila mdhamini alitakiwa awe na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake, kuwasilisha vitambulisho vyao, ambayo ni, kadi ya kitambulisho cha Taifa au Kadi ya kupigia kura.
Washtakiwa pia walizuiliwa kuondoka nchini bila kupata ruhusa ya Mahakama.
Kwa upande wa Amdani na Mwakabanga, hakimu aliwapa dhamana kwa masharti ya kupata wadhamini wawili kila mmoja ambaye atasaini dhamana ya 500,000 / na walitakiwa kuwasilisha vitambulisho vyao.
Kesi zote ziliahirishwa hadi Septemba 10, 2020.
Kampeni ya "PETA" yatatua kero za umeme Mkoani Tanga.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Tanga hivi
karibuni limezindua Kampeni ya "PETA" lengo likiwa ni kutoa elimu ya
huduma zote zitolewazo na TANESCO ikiwemo kutatua kero mbalimbali za
umeme kwa wananchi.
Akizindua kampeni ya PETA Kaimu Meneja Mkoa wa Tanga Mhandisi Bakari
Kalulu akiambatana na wakuu wa Idara za TANESCO Mkoa wa Tanga ili
kupokea Kero za Wananchi na kuzitolea majibu yake.
Mhandisi, Kalulu alisema baadhi ya Wateja wa TANESCO wanatumia umeme kwa
ajili ya kufukuza giza yaani kwa ajili ya Taa tu, PETA imekuja na
majibu ya kuwahamasisha wateja waache fikra hizo na kufikiri namna nzuri
ya kutumia umeme kukuza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.
Akiielezea Kampeni hiyo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa
Tanga, Bw. Amon Bandiwe alisema PETA ni kifupi cha maneno P =Pata , E
=Elimu ya matumizi Bora ya umeme, T =Toa kero yako, A = Acha kuhujumu
miundombinu.
Aliongeza, kampeni ya PETA itasaidia TANESCO kufikia malengo ya utoaji
wa huduma ya umeme kwa Wateja na ni chachu ya kubadili fikra za Wateja
kwa kutumia nishati ya umeme kukuza vipato vyao.
Kampeni hii ni suluhisho la changamoto zote za kero zinazotokana na huduma ya umeme Mkoani Tanga.
Wakazi wa Mkoa wa Tanga wameipongeza TANESCO kwa kuzindua kampeni ya
PETA kampeni ambayo itaisaidia TANESCO Mkoa wa Tanga kuboresha huduma
zake kwa Mkoa na Wilaya.
Aidha, Jumla ya kero 21 zilipokelewa na kujibiwa na wakuu wa Idara papo kwa papo.