Pages

November 11, 2020

JNHPP - Zoezi la kuchepusha Maji kuanza

Kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa handaki la kuchepusha maji katika mradi wa Julius Nyerere, kazi inayofuatia ni uchepushaji wa maji ili kuanza ujenzi wa tuta kuu.

Handaki hilo lina urefu wa mita 703 na upana wa mita 17 huku kimo chake kikiwa mita 12.

Akiongea kuhusu kufikiwa kwa hatua hiyo muhimu, Mhandisi Said Kimbanga ambaye ni Meneja Ujenzi, amesema zoezi linalofanyika kwa sasa ni utoaji wa udongo kwenye njia ya kuingilia maji, kufikia kwenye level ya 68.5 juu ya usawa wa bahari ili maji yaweze kupita.

"Hapa tulipo maji yanapita kuelekea baharini, hatuwezi kujenga tuta kuu hadi tutakapo yachepusha maji kupita kwenye handaki na eneo hilo kubaki kavu" alisema Mhandisi Kimbanga.

Aliongeza handaki hilo limekamilika kwa asilimia 100, zoezi linaloendelea ni uondoaji wa vifaa ndani ya handaki na kukata udongo uliopo mbele ya lango la kuingilia maji ili kuruhusu maji kuingia ndani ya handaki.

Aidha, zoezi lingine litakalofanyika ni ujazaji wa udongo kwenye mto kujenga tuta (cofferdam) ili kufunga mto na kuruhusu maji kupita kwenye handaki mchepusho.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano TANESCO, Johary Kachwamba amesema kukamilika kwa mradi wa Julius Nyerere Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

"Umeme unaozalishwa kwa maji ni umeme wa bei nafuu, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama kidogo hivyo tutarajie bei ya umeme kwa Wateja kushuka" amesema Kachwamba.

Aliongeza, kutokana na umeme wa maji kuwa wa gharama nafuu ambapo unit moja inazalishwa kwa shilingi 36 TANESCO itaweza kujiendesha kwa faida zaidi.

"Tanzania inaelekea sehemu ya kihistoria, kwa kuwa na maendeleo endelevu, tutaokoa mazingira kwani wananchi wataweza kumudu gharama za umeme hivyo kuondoa matumizi ya kuni na mkaa" alisisitiza Kachwamba.
 


 
 


 

Bodi ya TANESCO yaridhishwa na uzalishaji umeme Pangani Falls


 Bodi ya Wakurugenzi TANESCO ikiongonzwa na Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Alexander Kyaruzi imeridhishwa na utendaji kazi wa kituo cha kufua umeme cha Pangani chenye uwezo wa Mw 68.

Katika kituo hicho cha Pangani Bodi ilikagua mitambo ya kuzalisha umeme na kuridhishwa na utendaji kazi kituoni hapo. Pia bodi ilipata fursa ya kutembelea mtambo wa kuingizia maji ambayo pia yanakwenda kufua umeme kituo cha ya Hale.

Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ipo katika ziara ya siku sita kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za TANESCO katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.