Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwa Mkoani Njombe Januari 30,
2021 amesema kuwa, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa miradi
miwili mikubwa ya kufua umeme wa jumla ya megawati 580 kwa njia ya maji
ambayo ni, Mradi wa Ruhudji na Mradi wa Rumakali yote kwa pamoja ikiwa
Mkoani Njombe.
Alieleza kuwa, Mradi wa Ruhudji utazalisha megawati 358 na Mradi wa
Ruamakali utazalisha megawati 222 ambapo maandalizi ya ujenzi wa miradi
hiyo miwili mikubwa yameanza utekelezaji wake kwa wakati mmoja ikiwemo
maandalizi ya Miundombinu wezeshi kwaajili ya ujenzi rasmi wa miradi
hiyo.
“Utekelezaji wa Miradi hii ulianza kwa hatua ya kufanya usanifu wa
Miradi tangu Desemba 2020 na unakaribia kukamilika. Sasa tunatarajia
kuingia hatua ya pili ya kutangaza zabuni ili kuwapata wakandarasi
kuanzia mwezi Machi ili ifikapo mwezi Julai wakandarasi wawe
wamepatikana na tuwakabidhi rasmi eneo la ujenzi ili waweze kuendelea na
ujenzi‘’ alisema Waziri Kalemani
Waziri Kalemani aliongeza kuwa, Miradi yote miwili inatarajiwa
kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu na hivyo kuongeza megawati
580 katika Gridi ya Taifa ili kuongeza uwezo ambapo kwa sasa Grid ya
Taifa ina uwezo megawati 1602 tu.
“Kwa mahitaji ya sasa, Nchi nzima tuna uwezo wa kutumia mpaka Megawati
1400, lakini kadri tunavyoongeza umeme katika Gridi, ndivyo tunavyo
hamasisha na kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi toka nje na ndani ya Nchi,
hivyo Serikali imeamua kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi hii
miwili ya Ruhudji na Ruamakali” alisema Waziri Kalemani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya ameushukuru uongozi
wa Serikali ya Awamu ya Tano, Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kuanza
kutekeleza miradi hiyo muhimu kwa Taifa ambayo utafiti wake ulifanyika
miaka mingi iliyopita lakini haikufikia hatua ya utekelezaji.
Mhe. Rubirya aliongeza kuwa mbali na miradi hiyo kuwa na manufaa makubwa
kwa taifa lakini ni matarajio ya Wananchi wa Njombe kuwa, Miradi hiyo
itafungua fursa za uwekezaji mkuba katika Mkoa wa Njombe na maeneo ya
jirani.
Niihakikishie Serikali, Wizara ya Nishati na TANESCO kuwa, Mkoa wa
Njombe utaendelea na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ya kutunza
mazigira ambayo yatawezeha upatikanaji wa maji kwanza kwajili ya Mradi
Mkubwa wa Julius Nyerere lakini pia Miradi hii ya Ruhudji na Ruamakali”
Alisema Mhe. Rubirya
Kwa upande wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Uzalishaji Umeme, Mhandisi
Pakaya Mtamakaya alisema sambamba na Miradi hiyo ya kufua umeme
zitajengwa njia mbili za kusafirisha umeme huo za Msongo wa Kilovolti
400.
“Njia ya kwanza itajengwa kutoka Ruamakali hadi Kituo cha Mwakibete
Mbeya na ya pili kutoka eneo la Ruhudji mpaka kilipo kituo cha kupoza
umeme Mkoani Iringa ili kuwezesha usafirishaji wa umeme huo kuingia
katika Gridi ya Taifa na kutumika katika Mikoa mbalimbali nchini”
alisema Mhandisi Pakaya.
Akimalizia ziara yake Mkoani njombe Waziri Kalemani ametoa rai kwa
wananchi wa Mkoa wa Njombe kujiandaa kupokea miradi yote miwili pamoja
na kuchangamkia fursa zote za kujipatia kipato kutokana na ujenzi wa
miradi hiyo huku akiwasihi wananchi wa Mkoa wa Njombe kulinda vyanzo vya
maji, kutunza mazingira pamoja na miundombinu yote ya umeme.