Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwa katika
kikao kazi na Watendaji wa TANESCO leo Aprili 25, 2021 Jijini Dodoma,
amesema mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Julius Nyerere
hadi Chalinze kilometa 167 msongo wa kilovolti 400 utajengwa na Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO).
Serikali
imekuwa ikiwaamini na kuwatumia Wataalamu wa TANESCO katika kutekeleza
na kusimamia miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo wa Julius Nyerere
utakaofua megawati 2115.
Dkt.
Kalemani ameongeza kuwa njia hiyo ya umeme inatarajiwa kukamilika mwezi
mmoja kabla ya mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere kuakamilika.
Katika
hatua nyingine Dkt. Kalemani amesema kuwa, Serikali imeridhishwa na
utendaji kazi wa Wafanyakazi wa TANESCO na Wizara ya Nishati imekuwa
ikijivunia utendaji kazi wao.
"Ndugu
zangu mafanikio ya nchi hii yanategemea TANESCO, vigezo vilivyofanya
tuingie kwenye uchumi wa kati umeme umechangia kwa kiasi kikubwa sana"
amesema Dkt. Kalemani.
Maeneo
ambayo TANESCO imekuwa na mafanikio ni eneo la kuunganisha Wateja
ambapo TANESCO iliweka malengo ya kuunganisha Wateja 300,000 na kabla ya
mwezi Juni mwaka huu wamesha unganishwa Wateja 322,000 hivyo kuvuka
lengo.
Eneo lingine ni
ukusanyaji wa madeni sugu ya Serikali na Taasisi za umma deni lilikuwa
bilioni 278 ambapo zimekusanywa bilioni 126.
Dkt. Kalemani
amesema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/21 Wizara
imeainisha vipaumbele ambavyo ni utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya
kufua umeme na kuyafikishia umeme wa gridi ya Taifa maeneo ambayo
haijafika.