Pages

May 12, 2014

BIG RESULTS NOW:



Ujenzi Kinyerezi 1 wakamilika kwa asilimia 50






Ujenzi wa mradi wa Kituo cha Kufua umeme kwa kutumia gesi asilia Kinyerezi 1 ambao upo chini ya Mpango wa taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umekamilika kwa asilimia 50. Kituo hicho ambacho kitakuwa na uwezo wa kufua megawati  150 baada ya kukamilika kinategemea kutumia gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi nao unakwenda kwa kasi.
Baada ya kukamilika kwa Mtambo huu, kutakuwa na njia mbili za kusafirisha umeme ambapo njia moja ya msongo wa kilovolti 132 itapeleka umeme kwenye Kituo cha Kupooza na kusambaza umeme cha Gongo la mboto na viwandani na njia ya pili ya msongo wa kilovolti 220 itapeleka umeme moja kwa moja kwenye gridi ya Taifa. Mradi huu unajengwa na kampuni ya Jacobsen Elektro ya Norway.
Akizungumzia ujenzi huo Meneja wa Kituo hicho, Mhandisi Simon Jilima alisema ujenzi huo umefikia katika hatua nzuri na unategemewa  kukamilika mwishoni mwa mwaka huu ambapo mwezi wa tisa inategemewa kuanza majaribio ya kufua umeme. Aliongeza kuwa mitambo hiyo imejengwa kisasa ambapo hata moshi unaotoka kwenye mitambo hiyo ni kidogo sana kiasi kwamba hauna madhara kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa mtambo na haina kelele.
Alisema, Mtambo huu umejengwa kwa pesa ya serikali na umegharimu jumla ya dola za Marekani milioni 183 sawa na shilingi bilioni 293 pesa ya kitanzania. Ujenzi wa Mradi huo pia umesaidia kutoa ajira kwa watanzania wazawa ambapo asilimia 93 ya wafanyakazi ni watanzania. Aidha Mhandisi Jilima alibainisha kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo, wananchi wanaoishi pembezoni mwa mtambo huo wataweza kupata huduma ya maji bure.
Mhandisi Jilima aliongeza  kuwa, mtambo huu pia utakuwa na uwezo wa kufua umeme kwa kutumia mafuta ambapo yanajengwa mantenki yenye uwezo wa kuchukua lita milioni moja na nusu, akieleza sababu ya kutumia mafuta kuwa endapo kutakuwa na matengenezo ya visima vya gesi kwa upande wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) au matengenezo kwenye mashine za kusukuma gesi, mitambo hiyo itatumia mafuta ili tusipoteze megawati 150 kwenye gridi ya taifa.
Eneo litakuwa na vituo vinne. Kinyerezi 1 itakayofua umeme megawati 150, Kinyerezi 2 kitakachofua umeme megawati 240, Kinyerezi 3 kitakachofua umeme megawati 600 na Kinyerezi 4 kitakachofua umeme megawati 330, mitambo yote itaendeshwa kwa gesi itakayomilkiwa na TPDC.
Mradi wa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi 1-4 ni sehemu ya utekelezaji wa miradi iliyo chini ya mpango wa taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

No comments:

Post a Comment