Pages

October 15, 2017

Wahandisi Wa TANESCO Wapambana usiku na mchana kurejesha umeme katika hali yake ya kawaida Mikoa ya Mtwara na Lindi




 WAHANDISI na Mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wanapambana usiku na mchana kuzifanyia matengenezo mashine za kufua umeme, ili kuondoa tatizo la kukosekana kwa umeme kwa vipindi virefu kila siku kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi.
 Akizungumza mjini Mtwara Oktoba 14, 2017, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Kaitwa Bashaija, amesema kwa sasa Wahandisi na Mafundi wa TANESCO wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana ili kutengeneza mitambo ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Baadhi ya Wananchi wameshuhudia mafundi hao wakifanyakazi ya kurekebisha mitambo hiyo katika Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia Mkoani Mtwara.
“Mitambo hii ina kiasi cha mika 10 tangu ifungwe, na kadiri miaka inavyokweda ndivyo ongezeko la uhitaji wa umeme hususan Mkoani Mtwara linazidi kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi,” Alisema Mhandisi Bashaija.

Aliongeza, miaka michache iliyopita baadhi ya mitambo iliweza kuzimwa na bado hali ya umeme ilikuwa imara.
Wiki iliyopita Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliagiza TANESCO kufanya juhudi za ziada kuhakikisha tatizo la umeme mkoani Mtwara na Lindi linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kutokana na hali hiyo Mhandisi Bashaija, alisema kuwa kwa sasa TANESCO winamipango ya muda mfupi na mrefu katika kuhakikisha miundombinu ya umeme katika Mikoa ya kusini inaimarika.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia gesi asilia cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba, alisema licha ya changamoto hiyo kwa sasa bado mitambo iliyopo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme katika Mikoa hiyo.
“Pamoja na hali hii lakini kwa sasa tunakwenda vizuri kiasi ila si sana maana umeme kuna wakati unarudi na kukatika. Na tunaamini tutafanikiwa kurudi katika hali ya kawaida na kikubwa tunawaomba Wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kutuvumilia kwani nasi tunajua umuhimu wa umeme katika shughuli za uzalishaji.” Alitoa rai Mhandisi Chinumba.


No comments:

Post a Comment