Moja ya mitambo ya kufua umeme wa mafuta ya dizeli uliokuwa kwenye kituo cha Songea ikiwa imezimwa.
NA K-VIS BLOG, SONGEA
KUTOKANA na kuzimwa kwa mitambo ya dizeli iliyokuwa
ikitumika kufua umeme kwa matumizi ya mji wa Songea na vitongoji vyake Septemba
13, 2018 baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, Shirika la umeme Tanzania
TANESCO sasa litaokoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 450,108,508
zilizokuwa zikitumika kununua dizeli kila mwezi.
Septemba 13, 2018 TANESCO iliwasha rasmi kituo kipya na
cha kisasa cha kupoza na kusambaza umeme cha Madaba, ambacho kimeunganishwa
kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kuondoa matumizi ya umeme wa mafuta kwenye
Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea na vitongoji vyake.
Kuwashwa kwa mtambo huo ni baada ya kukamilika kwa Mradi
wa umeme wa Makambako-Songea ambao ulihusisha ujenzi wa vituo vya kupoza na
kusambaza umeme vya Makambako na Songea sambamba na upanuzi wa kituo cha kupoza
na kusambaza umeme cha Makambako, lakini pia Ujenzi wa njia kuu ya
usafirishaji Umeme wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilometa 245 kutoka Makambako
hadi Songea kupitia Madaba. Usambazaji Umeme wa msongo wa 33kV zenye urefu wa
kilomita 900 na kuunganisha wateja 22,700 katika Wilaya za Njombe , Ludewa na
mji wa Makambako katika Mkoa wa Njombe, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo
na Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma.
Tayari wakazi wa
mji wa Songea wamepokea taarifa za mji wao kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa
na hivyo kuondoa ile adha ya kukatika umeme iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda
mrefu.
Songea
kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kuna maanisha mji huo sasa umeanza kupata
umeme ulio bora na wa uhakika na hivyo wananchi sasa wanapaswa kuchangamkia
fursa ya uwepo wa nishati hiyo kwa kufungua viwanda vidogo na miradi mbalimbali
ya kiuchumi inayotegemea nishati ya umeme.
Kituo cha Umeme TANESCO Songea ambacho kilikuwa kikitumia mashine zinazoendeshwa kwa mafuta ya dizeli. Kituo hicho sasa kimezimwa.
Tenki la kuhifadhia mafuta ya dizeli, ambalo sasa litabaki kama kumbukumbu, baada ya matumizi yake kukoma rasmi Septemba 13, 2018.
No comments:
Post a Comment