Pages

November 15, 2019

Dkt. Kalemani aipa maagizo mazito Bodi ya Wakurugenzi TANESCO



WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani leo Novemba 15, 2019 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) aliyoiteua juzi Novemba 13, 2019.

Dkt. Kalemani akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu, ameizundia Bodi hiyo yenye wajumbe 9 juzi jijini Dodoma na kuipa maagizo yapatayo 16.

Bodi hiyo itaongozwa na Dkt. Alexander Kyaruzi ambaye aliteuliwa Novemba 9, 2019 na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kipindi kingine cha pili kuongoza Bodi hiyo.

Akizindua Bodi hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu, Dkt. Kalemani alimemkabidhi Mwenyekiti Dkt. Kyaruzi kitendea kazi ambacho ni Sheria ya Umeme ya Mwaka 2008 aliyosema ndiyo itakayowaongoza katika majukumu yao.
Aidha, aliwapa maelekezo ya kuwa umeme ndio injini ya uchumi wa viwanda hivyo ni lazima waisimamie Tanesco kuhakikisha umeme unapatikana katika shughuli zote za kiuchumi nchini. Alitaka uwepo umeme wa kutosha na unaotabirika ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali.
Aliwataka wakasimamie miradi hiyo iliyoanza kutekelezwa na itakayotelezwa na Tanesco, na katika hilo, wahakikishe Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji wa megawati 2,115, unakamilishwa kwa wakati ifikapo Juni 14, 2022, kama ilivyoelezwa katika mkataba.
Aliitaja miradi mingine kama wa Ruhuji megawati 358, Rumakari megawati 222 na Malagarasi na mengine, inasimamiwa na kukamilika kwa wakati.
Aliwataka kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 njia zote za kusafirishia umeme zinaunganishwa na Gridi ya Taifa katika kona zote za Tanzania, kwa kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wawe wameanza kutumia umeme wakiwamo wale wanaoishi vijijini.
Dkt. Kalemani pia aliitaka bodi kuhakikisha wanarekebisha, wanaboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirisha umeme, kuisimamia TANESCO na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika miradi ya umeme vijijini kwa kuwabana makandarasi kukamilisha miradi kwa wakati.
“Tusingependa kuongeza hata dakika moja kwa mkandarasi katika mradi wowote ule, tunataka wakabidhi miradi kwa wakati,” alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, aliitaka bodi kuhakikisha viwanda vinapata umeme wa uhakika kwa kutumia transfoma kubwa zenye uwezo wa kuchukua umeme mwingi, na pia kusisitiza mita, transfoma, na nyaya haziuzwi kwa mwananchi yeyote na atakayekiuka agizo hilo achukuliwe hatua.
Alisisitiza kuwa kwa vijijini, mwananchi aunganishiwe umeme kwa Sh 27,000 tu, na atakayekiuka hilo, naye achukuliwe hatua na bodi kwa yule aliye kwenye mamlaka yao.
Kuhusu mapato ya shirika, alitaka wasimamie ukusanyaji huo wa mapato, na kuagiza kuwa kwa yeyote ambaye anadaiwa Ankara na Tanesco akatiwe huduma mara moja na hasa kama madeni hayo ni sahihi na halali.
Aliagiza pia kuyaaangalia maeneo yenye tija kama viwanda, mitambo ya kusukuma maji, zahanati na mengine na kukusanya mapato, huku akiisifu Tanesco kwa kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 9 hadi kufikia Sh bilioni 46 na kutaka waongeze bidii ifike Sh bilioni 60.
Aidha, aliwataka kuongeza vyanzo vya mapato, kuondoa kero ya watu wanaosubiri kuunganishiwa umeme kwani nguzo na nyaya zipo za kutosha, kudhibiti vishoka wachache waliopo, kuhakikisha katikakatika ndogo ya umeme iliyopo inakuwa historia na kuwajengea uwezo wazalishaji wadogo wa umeme nchini.
Mbali ya kuwataka kuwa wabunifu na wenye uthubutu kwa kufanya kazi kwa kuzingatia kasi, wepesi na nidhamu, aliwaagiza kuwa sheria za manunuzi zisiwe kificho cha kuchelewesha kazi.
Kuhusu Jiji la Dodoma, aliagiza liangaliwe kwa ukaribu na kila eneo lipate huduma ya umeme, na hilo anataka kuliona limefanyika ndani ya miezi sita.
Katika utekelezaji wa hayo yote, Dkt. Kalemani ameagiza Bodi itoe taarifa kwa wizara kila baada ya miezi mitatu kuelezea utendaji wao wa kazi.
Naibu Waziri Mgalu kwa upande wake, aliwatakia kila la heri wajumbe wa bodi hiyo, na kueleza kuwa wizara inawategemea sana katika kusukuma mbele majukumu hasa ya kulisimamia shirika hilo la TANESCO.
Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Kyaruzi na wajumbe wake waliokuwapo jana, waliahidi kutekeleza maelekezo yote hayo ya Waziri kwa ushirikiano, uadilifu, weledi, na kutoa utumishi uliotukuka ili kuisaidia serikali katika sekta ya umeme kufikia Tanzania ya viwanda ifikapo 2025.







No comments:

Post a Comment