Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani yameanza kunufaika na Mradi mkubwa wa
Umeme wa Geita-Bulyanhulu baada ya kukamilika rasmi kwa mradi huo wenye
laini ya kusafirisha Umeme mkubwa katika msongo wa Kilovolti 220
sambamba na Vituo viwili vya kupoza na kusambaza Umeme.
Akifanya ziara na kushuhudia uwashwaji Umeme kwa mara ya kwanza katika
mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, amesema kuwa,
kwa muda mrefu Mkoa wa Geita ulikuwa na umeme usio tosheleza mahitaji.
“Hali iliyopelekea Serikali kufanya jitihada za kujenga mradi huu
Mkubwa ulio gharimu zaidi ya shilingi Bilioni 50 ili kuwezesha wananchi
wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na gharama
nafuu” alisema Mhandisi Gabriel.
Aliongeza kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Geita hivi
sasa kumewezesha Mkoa wa Geita kuwa na umeme wa uhakika utakaowezesha
uwekezaji katika sekta mbali mbali hususan uchimbaji wa Madini na
Viwanda.
Mhandisi Gabriel aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Geita
baada ya ujio wa Umeme wa uhakika na gharama nafuu wa TANESCO.
“Hali sasa ni shwari , umeme upo wa kutosha na wa uhakika. kukamilika
kwa ujenzi wa kituo cha Geita kumewezesha mkoa kuwa na zaidi ya Megawati
85 wakati matumizi ya sasa ya ni Megawati 16 pekee” aliongeza
Mhandisi Gabriel.
Aidha, Mhandisi Gabriel amewaasa wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya
jirani ambapo miundombinu ya umeme imepita kuilinda miundombinu hiyo
kwa manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho.
Mhandisi Gabriel pia ametoa onyo kuhusu tabia ya wananchi kuchoma moto
mashamba kiholela, hali inayohatarisha miundombinu ya umeme.
Aliongeza kuwa kwa mwananchi yoyote atakaye bainika kufanya uharibifu
huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho
kwa wote wenye nia za namna hiyo.
Kwa upande wa TANESCO, Mhandisi Emanuel Manirabona ambaye ni Meneja
Mwandamizi wa Miradi -TANESCO amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia
kubwa ya kusafirisha umeme ni miongoni mwa miradi mikubwa ya umeme
inayojengwa katika Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi Kaskazini mwa
Nchi.
Mhandisi Manirabona ameitaja miradi hiyo kuwa ni njia ya umeme ya
Geita-Nyakanazi yenye uwezo wa Kilovolti 220, utakao gharimu zaidi ya
shilingi Bilioni 100 pamoja na ule wa Kigoma hadi Nyakanazi msongo wa
Kilovolti 400.
“yote hii ni kuhakikisha kuwa maeneo ya Uwekezaji katika Kanda ya Ziwa
na Kanda ya Magharibi Kaskazini mwa Nchi yanapata umeme wa uhakika na
wakutosha” Alisema Mhandisi Manirabona.
Manirabona aliongeza kuwa, kuungwa kwa njia ya kusafirisha umeme ya
Bulyanhulu-Geita, kunawezesha wananchi wa mkoa wa Geita na Maeneo ya
jirani na Migodi ya Bulyanhulu pamoja na Geita kuwa na umeme wa uhakika.
No comments:
Post a Comment