Pages

May 26, 2021

TANZANIA YAPATA DOLA MILIONI 140 UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME MARAGARASI

 

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO, leo Mei 26,2021, imeingia makubaliano ya mkopo wa Dola milioni 140 kutoka Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kufua umeme wa megawati 49.5 kupitia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi uliopo Mkoani Kigoma.

Mradi wa Maragalasi utachochea ukuwaji wa shughuli za maendeleo ya kijamii pamoja na kiuchumi kwa wakazi wa Mikoa ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Mradi huu, utahusisha pia uimarishaji gridi ya Taifa itakayorahisisha biashara ya mauziano ya Nishati ya umeme baina ya Tanzania na Nchi majirani.

Aidha gharama za mradi huo kwa ujumla ni takriban Dola milioni 144.14, ambapo Serikali ya Tanzania itachangia kiwango kinachobakia cha Dola milioni 4.14 kukamilisha fedha za Ujenzi wa Mradi huo muhimu kwa Mikoa ya ukanda wa Kaskazini Mashariki na Tanzania kwa ujumla.

May 1, 2021

KITUO CHA UMEME KIGAMBONI CHAKAMILIKA

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Aprili 30, 2021 majira ya saa 4:28 usiku limefanikiwa kuwasha kituo cha kupokea na kupoza  umeme cha Dege Kigamboni.

Ujenzi wa kituo cha kupokea umeme cha  Dege umefanywa na Wataalamu wa TANESCO, vifaa na mitambo vimeletwa na Mkandarasi Ms Telenergy d.o.o na njia ya umeme imejengwa na  Mkandarasi Kampuni ya JV Tontan Ltd Group Six.

Kuwashwa kwa kituo hicho cha Dege kumeenda sambamba na uwashaji wa umeme kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka kituo cha Mbagala hadi cha Dege.

Kituo cha Dege kinatarajiwa kuwa mkombozi wa changamoto za umeme kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani. 

Awali wananchi wa Kigamboni walipata umeme kupitia njia ndogo ya msongo wa kilovoti 33kV kutokea kituo cha Ilala na walikuwa wakikabiliwa na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara pamoja na umeme kuwa mdogo. 

Baada ya kuwasha kituo hicho umeme wa uhakika utapatikana katika maeneo yote ya wilaya Kigamboni ikiwemo maeneo ya Kimbiji, Mwongozo, Mwasonga, Pemba mnazi, Kisarawe2, na maeneo ya Viwanda vikubwa Wilayani hapo.

Mradi wa  Dege ulianza kutekelezwa Mwezi Mei, 2019 kwa gharama ya shilingi 26.2 Bilioni.