Pages

January 28, 2022

TANESCO KUFANYA MABORESHO KWENYE VITUO VYAKE VYA UZALISHAJI UMEME VYA KINYEREZI I NA UBUNGO III


Katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa umeme nchini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linaendelea na maboresho kwenye vituo vyake vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I itakayozalisha megawati 185 na Ubungo III megawati 112.


Akizungumza na wanahabari leo Januari 28, 2022 Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo, Maharage Chande amesema mpaka sasa uzalishaji kutoka mitambo ya Ubungo III umefikia Megawati 60 ambazo tayari zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Amesema kwa sasa kazi ya kupanua kituo cha Kinyerezi I inaendelea na megawati 70 za awali zitaingia kwenye mfumo wa gridi mwezi Aprili 2022 na ifikapo mwezi Agosti 2022 kazi hiyo itakuwa imekamilika na kupelekea Kituo cha Kinyerezi I ambacho sasa kinazalisha megawati 150 kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 335.

‘‘Mitambo hii inayoongezwa ili iweze kuzalisha umeme, inapelekea mahitaji ya gesi asilia kuongezeka ambapo inalazimu kufanya uboreshaji wa mfumo wa gesi kwenye mifumo ya TPDC (Tanzania Petroleum Development Company) na PAET (Pan African Energy Tanzania)’’ amesema Maharage.

Aliongeza kuwa zoezi la uboreshaji litafanyika kwenye visima vya gesi vilivyopo Songosongo kuanzia tarehe 01 hadi 10 Februari 2022, ambapo kukamilika kwake kutahakikisha gesi  ya ziada inayohitajika inapatikana.

Hivyo utekelezaji wa maboresho hayo utapelekea mapungufu ya gesi kwenye mitambo ya kuzalishia umeme wa gesi asilia na kulazimika kuzimwa kwa baadhi ya mitambo ili kupisha zoezi hilo muhimu.

Sambamba na matengenezo hayo, hali hiyo itasababisha upungufu wa uzalishaji umeme na kuathiri baadhi ya maeneo, amesema wananchi watapata taarifa za makatizo ya umeme kama zitakavyotolewa na mikoa husika.

Maboresho hayo kwenye vituo vya vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I na Ubungo III yatasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza malalamiko ya wateja ya kutokuwa na umeme wa uhakika na unaotabirika.



No comments:

Post a Comment