Pages

May 7, 2022

TANESCO KUOKOA TAKRIBANI BIL.1.7 NGORONGORO

 

Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) imekamilisha ujenzi wa mradi wa umeme wenye thamani ya shilingi bil. 2.9 wa kuunganisha Wilaya ya Ngorongoro kwenye grid ya taifa.


Awali Wilaya ya Ngorongoro ilitumia umeme wa jenereta ambao ulikuwa ukigharimu kiasi cha bil.1.7 kama gharama za uendeshaji kwa mwaka,huku makusanyo ya wilaya ya ngorongo yakiwa ni Mil.374 kwa mwaka.

Akizindua umeme  huo wa gridi katika Wilaya ya Ngorongoro  Halmashauri ya mji mdogo wa Loriondo Mei 06, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe:John Mongela amesema TANESCO imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuwafikishia huduma ya umeme wananchi na uboreshaji wa miundombinu.

"Leo tunapozindua umeme gridi ya Taifa ni ushahidi tosha wa kazi kubwa wanayoifanya TANESCO, tumeona mradi huu ukikamilika ndani ya muda mfupi" amesema Mhe. Mongela.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Mhandisi Herini  Mhina amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Septemba 25, 2021 na umekamilika Mai 04, 2022, ikiwa ni takribani miezi 7 mpaka kukamilika kwake.

Ameongeza kuwa kuunganisha Wilaya ya Ngorongoro na gridi ya Taifa kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi hao.

"Sasa Wilaya ya Ngorongoro inaenda kuwa na umeme wa uhakika na unaotabirika, jambo kubwa zaidi ni  kulipunguzia Shirika na Taifa  gharama kubwa za kuzalisha umeme wa kutumia mafuta ya dizeli" amesema Mha. Mhina.

Mradi huo umetekelezwa na TANESCO kwa kutumia wataalamu wake wa ndani, unahusisha usimikwaji wa nguzo za zege 686 pamoja na za miti 220 zenye urefu wa mita 13 na ni sehemu ya mkakati endelevu wa Shirika kwenye kuimarisha huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment