Pages

May 20, 2011

PRESS RELEASE : TAARIFA KUHUSU KATIZO LA UMEME (19 – 26 MEI, 2011) KUTOKANA NA UKARABATI WA MITAMBO YA GESI YA SONGO SONGO

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawaarifu wateja wake na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia tarehe 19 hadi 26 Mei, mwaka huu, kutakuwa na upungufu mkubwa wa umeme katika Gridi ya Taifa ambao utawaathiri watumiaji umeme wote walioungwa katika Gridi ya Taifa.
Upungufu huu unatokana na Visima na Mitambo ya gesi asili iliyopo katika kisiwa cha Songo Songo, mkoani Lindi, kuzimwa na wamiliki wake – Pan African Energy Tanzania Limited – kwa ajili ya ukaguzi na ukarabati.  Lengo ni kuboresha viwango vya gesi inayozalishwa na kusafirishwa kutoka kisiwa hicho hadi Dar es Salaam kwa kufua umeme na kutumiwa viwandani.
Tangu mwanzoni mwa mwaka jana gesi inayotolewa na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa matumizi ya umeme na viwanda imekuwa ikipungua kutokana na sababu za kiufundi (Corrosion).
Taarifa iliyotolewa na Shirika la TANESCO, jijini Dar es Salaam leo imesema kati ya tarehe 19 hadi 23 mwezi huu kutakuwa na upungufu wa MW (megawati) 200 zinazofuliwa kwa kutumia gesi, kutokana na visima vya Songo Songo kuzimwa kimoja baada ya kingine, kwa ukaguzi wa kiufundi (intensive technical inspection).
Aidha taarifa hiyo iliongeza kuwa upungufu mkubwa zaidi wa umeme utatokea kati ya tarehe 23 hadi 26 mwezi huu.
Katika kipindi hicho cha siku nne, Visima na Mitambo yote ya gesi kwenye kisiwa cha Songo Songo itazimwa, na hivyo kusababisha kukosekana kwa MW 350 za umeme wa gesi.
Hii ina maana kuwa vituo vya Songas, Ubungo Gas Plant na Tegeta Gas Plant vinavyotumia gesi asilia kufua umeme vitasitisha shughuli zake kwa siku hizo nne, jambo litakalosababisha upungufu wa umeme kwenye Gridi ya Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa umeme wa gesi huchangia karibu nusu ya umeme unaofuliwa kwenye vituo vyote nchini.
Hivi sasa kati ya MW 650 hadi 710 hufuliwa kwa siku kwa kutumia vituo vya nguvu ya maji, gesi asili na kiwango kidogo cha mafuta.
Kutokana na upungufu huo, katika  siku  tano za mwanzo, mgao wa umeme  wa MW 200 utaendeshwa na TANESCO kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 5.00 usiku, ambapo umeme utarejeshwa.
Aidha kuanzia tarehe 23 Mei 2011 mchana mpaka 26 Mei 2011 mchana mgao wa Umeme utakuwa MW 300 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tano za usiku, na MW 50 kuanzia saa tano usiku hadi saa mbili asubuhi
TANESCO inawaomba wenye viwanda vikubwa kutumia kipindi hicho kufanya usafi na matengenezo ya mitambo yao, hususan viwanda vile ambavyo havina jenereta za dharura.
Wakati huo huo, Shirika lingependa kuwafahamisha wateja wake kwamba hali ya umeme imekuwa nzuri siku za karibuni kutokana na mvua ambazo zimenyesha na kuongeza maji kwenye vituo vya Kihansi, Kidatu na Pangani.  TANESCO iliongeza uzalishaji umeme kwenye vituo hivyo na kupunguza makali ya mgao wa umeme japo ni  kwa muda tu.
Hata hivyo kina cha maji kwenye bwawa kuu la Mtera bado kipo chini sana na hakiridhishi, hasa ikizingatiwa kuwa msimu wa mvua unakaribia kumalizika na msimu wa kiangazi unaanza.
Mpaka tarehe 6 Mei 2011 kina cha maji kwenye bwawa la Mtera kilikuwa mita 691.18 usawa wa bahari.  Kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 na kina cha chini ni mita 690.00, juu ya usawa wa bahari.  Hii ina maana kwamba tangu mvua zianze kunyesha zimeongezeka sentimita 30 tu.
Tanesco inaendelea na mipango ya kukodisha mitambo ya dharura ili kupunguza makali ya mgao wakati wa kiangazi  kutokana na hali mbaya ya ujazo wa bwawa la Mtera na pia kuongezeka kwa matumizi ya umeme kwa upande wa wateja wetu.
TANESCO inawaomba wateja wake kupunguza matumizi ya umeme yasiyo ya lazima na kutumia umeme kwa uangalifu kwa kuzima taa mtu anapotoka chumbani, kuzima viyoyozi na vifaa vya umeme wafanyakazi wanapomaliza kazi maofisini na viwandani.
Tunatarajia kwamba wateja wetu na wananchi kwa ujumla watatuelewa na kushirikiana nasi katika kipindi hiki kigumu.


-ENDS-
_______________________________________________



IMETOLEWA NA OFISI YA MAWASILIANO, TANESCO
Simu: 2451185

3 comments:

  1. Kama tukijaribu kutathimini mashirika ya umma kwa misingi ya mchango wao ktk maendeleo ya uchumi Tanesco ni moja kati ya mashirika ya umma ambayo ni hopeless na ambayo kwa kiasi kikubwa mnachangia sana kuzorota kwa huduma za kijamii na uchumi nchini.. Katika nyakati hizi ambapo ukuaji wa uchumi na biashara vinahitaji nishati ya kutosha ya umeme ili viwe sustained, nyie mme bweteka tu, hamuwi wabunifu ktk uendeshaji wa shirika, hamgundui vyanzo vipya vya nishati mbadala, mnakula subsidy na kufanya ufisadi tu huku umeme ikiendelea kuwa tatizo...you guys r irritating..

    ReplyDelete
  2. ..ever since mgao wa umeme ulioanzia Tarehe 26 Mei 2011 uishe, maeneo ya mwananyamala, kinondoni, mkwajuni na yana experience mgao wa umeme wa saa 12 kila siku!! Huu mgao unatokana na nini?? Hamuoni kuwa mnaathiri shughuli za wajasiriamali wadogo wanaotegemea umeme ktk biashara na kazi zao?? Huu mgao ambao hauna taarifa rasmi ni mgao wa nini?? Nyie ni Cancer, mnang'aninia ku monopolise kila aspect ktk sekta nzima ya umeme wakati mna ineffiencies kibao, na tena ni wakiritimba, wahafidhina na hamuwekezi ktk modernisation..

    ReplyDelete
  3. Huu mgao unaoendelea ni upi? na unatokana na nini? Basi hata mtoe matangazo tujue tuna mgao ambao hatma yake haijulikani...mnatutesa sana

    ReplyDelete