Katika toleo lake la Jumanne Julai 8, 2014 Gazeti la Nipashe katika
ukurasa wa tano (5) lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari “Bodi TANESCO
yapinga Baraza la Mawaziri”. Kwa mujibu
wa gazeti hilo ni kwamba taarifa hiyo imetolewa na anayesemekana kuwa ni mjumbe
wa Bodi ambaye hakutaka jina lake
litajwe.
Nikiwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na kwa niaba ya wakurugenzi wa bodi ya TANESCO ninakanusha
vikali kuwa taarifa hiyo si ya kweli, ni ya kupotosha umma na haina maslahi
yoyote kwa maendeleo ya taifa letu. Aidha napenda kukanusha vikali kuwa taarifa
hiyo haikutolewa na mjumbe yoyote wa Bodi ya TANESCO.
Kwa mukhtadha huo napenda umma wa watanzania ufahamu kuwa Bodi ya
wakurugenzi na manejimenti ya TANESCO walishirikishwa kikamilifu katika hatua
zote kuhusu nia ya serikali ya kuligawa shirika ili kuongeza ufanisi zaidi.
Bodi na manejimenti ilifanya warsha ya siku tatu Bagamoyo kwa ajili ya kujadili na hatimaye
kufikia muafaka na kuandaa mapendekezo kuhusu jinsi ya kuligawa shirika.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa rasmi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Madini.
Aidha mapendekezo yaliyopelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ni maamuzi ya
bodi ya TANESCO ambapo kabla ya
kufikishwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri, bodi ya TANESCO pamoja
na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini ilikaa kupitia mapendekezo
hayo kifungu kwa kifungu na kukubaliana juu ya mpango wa kuligawa shirika.
Katika hali hiyo haiwezekani kuwepo kwa
mjumbe yoyote anayeweza kupinga mpango huo.
Kwa utaratibu ulivyo, maamuzi ya Baraza la Mawaziri ni agizo la
serikali kwa taasisi zilizo chini yake. Kwa sababu hiyo hakuna ukweli wowote
kuwa Bodi ya TANESCO inapinga maamuzi ya Baraza la Mawaziri.
Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, nakanusha kuwa taarifa
hizo hazina ukweli wowote na wala hazijatoka kwa mjumbe yeyote wa Bodi ya
TANESCO. Napenda kuwahakikishia watanzania kuwa Bodi yangu inaafiki na
itaendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na taasisi zingine kuhakikisha kuwa
maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusu mpango huo wa kuligawa shirika
unatekelezwa kikamilifu na kwa wakati.
Imetolewa:
Gen. Robert Mboma (Rt)
Mwenyekiti wa Bodi
Kwa niaba ya Wakurugenzi wa Bodi ya TANESCO
No comments:
Post a Comment