Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linanapenda kutoa
ufafanuzi kwa wateja wake kuhusu kukosekana kwa umeme kwa baadhi ya maeneo ya
jiji la Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:-
Mosi, Kuanzia Novemba 26, 2014 hadi Desemba 1, 2014
Mikoa yote iliyoungwa kwenye gridi ya taifa ikiwemo Dar es Salaam ilikuwa na
upungufu wa umeme kwa baadhi ya maeneo kutokana na kuharibika kwa mashine moja
ya Mtambo wa Kufua Umeme wa Kidatu yenye uwezo wa kufua megawati 50. Mtambo huo
kwa sasa umetengamaa na hakuna Mkoa wenye upungufu wa umeme.
Pili, Novemba 29, 2014 Kulitokea hitilafu ya
kuungua kwa Kikata Umeme (Circuit Breaker) kwenye Kituo cha Kupooza na
Kusambaza Umeme cha Ubungo upande wa msongo wa kilovolti 33 na hivyo
kusababisha baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kinondoni Kusini (Magomeni) kukosa
umeme kwa siku 2 mfululizo. Tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi na Mkoa huo kwa
sasa unapata umeme kama kawaida.
Tatu, Kuanguka
kwa nguzo kwa baadhi ya maeneo katika jiji la Dar es Salaam kutokana na
kuanza kwa kipindi cha mvua.
Nne, Matengenezo yanayoendelea ya ukarabati wa
miundombinu kwa mikoa yote ya Dar es Salaam. TANESCO inaendesha zoezi la
ukarabati wa miundombinu yake kwa mikoa ya Kinondoni Kusini (Magomeni),
Kinondoni Kaskazini (Mikocheni), Ilala na Temeke. Kazi zinazofanyika kwenye
zoezi hilo kwa sasa ni kubadilisha nguzo zilizooza, kunyanyua nguzo
zilizoinama, kuvuta nyaya zilizolegea na kukata miti inayogusa nyaya za umeme.
Zoezi kama hili hufanyika kwa kila mkoa kwa nchi nzima kama tahadhari kabla ya
kuanza kwa kipindi cha masika ambacho kinaambatana na mvua na upepo mkali.
Kwa sababu
hii kubwa, kumekuwa na usumbufu wa kukatwa kwa umeme kwa baadhi ya maeneo mara
moja kwa siku ili kupisha zoezi hilo ambalo tunatarajia litakamilika mwezi huu
wa Desemba.
Uongozi wa
Shirika unaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.
Imetolewa na
Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO MAKAO MAKUU.
No comments:
Post a Comment