Pages

February 2, 2018

TANESCO yamaliza tatizo la umeme Bagamoyo





Na Severin Mvungi,
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepatia ufumbuzi tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika wilaya ya Bagamoyo ambalo limekuwa ni kero kwa wakaazi wa mji huo na viunga vyake.

Kwa kipindi sasa wakaazi wa mji huo wamekuwa wakipata adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na hitilafu mbalimbali za mifumo na miundombinu ya umeme ya Shirika hilo.

Meneja wa Mkoa huo Mhandisi Martin Madullu alieleza kuwa tatizo kubwa la kukatika umeme kwenye Wilaya hiyo lilitokana na upepo na mvua ambazo zilikuwa zikinyesha na kuangusha nguzo zinazovusha umeme kutoka Dar es Salaam katika eneo la Mapinga darajani kwenye mto Mpiji.

Madullu aliongeza kuwa sababu nyingine ilikuwa ni wilaya hiyo kutegemea njia moja ya umeme ambayo pia inagawa umeme kwa wateja wengine ikitokea Tegeta kwenye Kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Kunduchi.

“Kwa sasa ukipita Mapinga darajani utashuhudia kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wetu ya kuvusha umeme kwenye mto mpiji na ni matarajio yetu kuwa hata mvua zikinyesha nguzo hizo haziwezi kuanguka tena au kufikiwa na maji” alisema Mhandisi Madullu.

Kuhusu sababu ya pili, Mhandisi Madullu alisema mafundi wa TANESCO Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wa Tegeta na wataalamu kutoka Makao makuu wamejenga njia maalum “dedicated line” kwa ajili ya Wilaya ya Bagamoyo tu ambayo haitaunganishwa na wateja wengine.

“Bagamoyo tumeitafutia njia ya peke yake ya kupeleka umeme ambayo itakuwa inatoa umeme mkubwa kutoka Kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Kunduchi hadi Bagamoyo. Hii itaondoa matatizo yote ya kukatika umeme mara kwa mara ambayo yalikuwa yanasababishwa na hitilafu za wateja wengine waliokuwa wameungwa njiani” aliongeza Mhandisi Madullu.

Aidha Mhandisi Madullu alisisitiza kuwa wateja wa Wilaya ya Bagamoyo na viunga vyake wategemee umeme wa kutosha na wauhakika kwa sasa kwani pamoja na njia hiyo inayotokea Kunduchi pia njia inayoleta umeme kutokea Kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Mlandizi kuja Bagamoyo nayo imeimarishwa. 

Bagamoyo ni moja ya miji mikongwe nchini  yenye historia ya Taifa letu na inayotembelewa na wageni wengi kujionea makumbusho ya taifa hasa magofu ya Kaole ambayo yaliyokuwepo tangu karne ya 13 na 15.

No comments:

Post a Comment