Na Severin Mvungi,
Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) limepatia ufumbuzi tatizo la kukatika umeme mara kwa mara
katika wilaya ya Bagamoyo ambalo limekuwa ni kero kwa wakaazi wa mji huo na
viunga vyake.
Kwa kipindi sasa
wakaazi wa mji huo wamekuwa wakipata adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara
kutokana na hitilafu mbalimbali za mifumo na miundombinu ya umeme ya Shirika
hilo.
Meneja wa Mkoa huo
Mhandisi Martin Madullu alieleza kuwa tatizo kubwa la kukatika umeme kwenye
Wilaya hiyo lilitokana na upepo na mvua ambazo zilikuwa zikinyesha na kuangusha
nguzo zinazovusha umeme kutoka Dar es Salaam katika eneo la Mapinga darajani
kwenye mto Mpiji.
Madullu aliongeza
kuwa sababu nyingine ilikuwa ni wilaya hiyo kutegemea njia moja ya umeme ambayo
pia inagawa umeme kwa wateja wengine ikitokea Tegeta kwenye Kituo cha kupooza
na kusambaza umeme cha Kunduchi.
“Kwa sasa ukipita
Mapinga darajani utashuhudia kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wetu ya
kuvusha umeme kwenye mto mpiji na ni matarajio yetu kuwa hata mvua zikinyesha
nguzo hizo haziwezi kuanguka tena au kufikiwa na maji” alisema Mhandisi
Madullu.
Kuhusu sababu ya
pili, Mhandisi Madullu alisema mafundi wa TANESCO Mkoa wa Pwani kwa
kushirikiana na wa Tegeta na wataalamu kutoka Makao makuu wamejenga njia maalum
“dedicated line” kwa ajili ya Wilaya ya Bagamoyo tu ambayo haitaunganishwa na
wateja wengine.
“Bagamoyo tumeitafutia
njia ya peke yake ya kupeleka umeme ambayo itakuwa inatoa umeme mkubwa kutoka
Kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Kunduchi hadi Bagamoyo. Hii itaondoa
matatizo yote ya kukatika umeme mara kwa mara ambayo yalikuwa yanasababishwa na
hitilafu za wateja wengine waliokuwa wameungwa njiani” aliongeza Mhandisi
Madullu.
Aidha Mhandisi
Madullu alisisitiza kuwa wateja wa Wilaya ya Bagamoyo na viunga vyake wategemee
umeme wa kutosha na wauhakika kwa sasa kwani pamoja na njia hiyo inayotokea
Kunduchi pia njia inayoleta umeme kutokea Kituo cha kupooza na kusambaza umeme
cha Mlandizi kuja Bagamoyo nayo imeimarishwa.
Bagamoyo ni moja ya
miji mikongwe nchini yenye historia ya
Taifa letu na inayotembelewa na wageni wengi kujionea makumbusho ya taifa hasa
magofu ya Kaole ambayo yaliyokuwepo tangu karne ya 13 na 15.
No comments:
Post a Comment