Pages
▼
February 26, 2018
"Zoezi la msako wezi wa umeme ni endelevu" Mhandisi Njavike
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kupitia kikosi kazi maalumu limeendesha Kampeni kabambe ya kubaini na kutokomeza matukio ya wizi wa umeme pamoja na uhujumu miundombinu y Mkoani Njombe ikiwa ni mwendelezo wa jitihada endelevu za TANESCO katika kudhibiti upotevu wa mapato ya Shirika.
Akiongea katika kampeni hiyo, Mhandisi Fredrick Njavike ambaye ni Meneja wa Kitengo cha udhibiti Mapato (RPU) alisema, ndani ya siku tano (5) kupitia kampeni hiyo tayari wamekagua takribani Wateja 2000 katika Wilaya ya Makambako pekee huku Njombe Mjini wakitarajia kukagua Wateja 1000.
Aliongeza, katika idadi ya Wateja waliokaguliwa, baadhi waligundulika kujihusisha na vitendo vya wizi wa umeme hivyo kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Njombe wahalifu hao walichukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa gharama za kiasi chote cha umeme walichokuwa wakiliibia Shirika baada ya kupigiwa mahesabu.
"Zoezi hili la ukaguzi na msako wa wezi wa umeme ni zoezi endelevu linalofanyika nchi nzima, niwatahadharishe wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja, kwani ni lazma watagundulika na hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na malipo ya fidia ya kiasi cha umeme walicholiibia Shirika". Alisema Mhandisi Njavike.
Alitoa rai kwa Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kufichua watu wenye viashiria vya wizi wa umeme.
" Lakini pia niwaombe wateja wetu kutoa taarifa TANESCO pale wanapona hitilafu zozote katika mita zao pamoja na kuepukana na vishoka wanaowashawishi waibe umeme kwani kupitia zoezi hili wezi wote watabainika." Alisisitiza Mhandisi Njavike
Kwa upande wake Meneja TANESCO Mkoa wa Njombe, Mhandisi Emmanuel Kachewa ametoa Wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Njombe kuendelea kushirikiana na TANESCO katika kuwafichua wezi wa umeme popote walipo ili waweze kuchukuliwa hatua na kuokoa upotevu wa mapato ya Shirika kwa ujumla.
Baadhi ya Wananchi waliozungumza na Afisa Uhusiano wetu wameipongeza TANESCO kwa kuendesha zoezi hili na kuongeza matukio ya wizi wa umeme yapo mtaani na wakati mwingine yamekuwa yakisababisha hata vifo kwa wahusika kunaswa na umeme wakati wakijaribu kuiba umeme hivyo ni vyema TANESCO pia wakatoa na Elimu juu ya madhara ya Wizi wa umeme kwa Wananchi wote wafahamu.
Aidha, TANESCO imekuwa ikiingia hasara kutokana na vitendo vya Wateja wachache ambao kwa makusudi kabisa wamekuwa wakiliibia Shirika umeme kwa katika maeneo mbalimbali na hivyo kulikosesha Shirika mapato stahiki na kurudisha nyuma jitihada za TANESCO na Serikali Katika kusambaza umeme nchi nzima na hivyo kufifisha kasi ya Uimarishaji wa Miundombinu ya Uzalishaji, Ufuaji na Usambaza umeme Nchini.
No comments:
Post a Comment