JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU
JITIHADA ZINAZOFANYWA NA SERIKALI/TANESCO KUKABILIANA
NA MGAWO WA UMEME NCHINI
1. Ndugu Wanahabari, tumewaiteni hapa leo tarehe 26/06/2011 ili mtusaidie kuuarifu umma wa Watanzania kuhusu jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali pamoja na TANESCO kukabiliana na upungufu wa uzalishaji wa umeme uliosababisha mgawo wa umeme unaoendelea nchini kwa sasa. Aidha, taarifa hii ni mwendelezo wa taarifa iliyotolewa na TANESCO tarehe 23/06/2011.
2. Ndugu Wanahabari, tunapenda kuwakumbusha Watanzania kwamba mgawo huu wa umeme kwa kiasi kikubwa umesababishwa na upungufu wa maji kwenye mabwawa yetu yanayotumika kuzalisha umeme (Mtera, Kidatu, Kihansi, Hale na Nyumba ya Mungu). Upungufu huu wa maji umesababishwa na kiasi kidogo cha mvua kilichonyesha mwaka huu. Kwa mfano kina cha maji cha bwawa la Mtera ambalo ndiyo bwawa mhimili kwa jana tarehe 25/06/2011 kilikuwa meta 690.87 juu ya usawa wa bahari. Kina cha chini kabisa kinachowezesha kuzalisha umeme ni meta 690.00. Wakati kina cha juu kabisa maji yanapojaa ni meta 698.50.
3. Ndugu Wanahabari, tunapenda kuendelea kuwakumbusha Watanzania kwamba upungufu huu wa maji katika mabwawa yetu umeathiri sana uwezo wetu wa kuzalisha umeme kwa sababu kwa sasa hivi asilimia 55 ya umeme wetu unatokana na maji, 34% gesi asili na 11% mafuta.
Mpangilio huu wa vyanzo vya kuzalisha umeme unaakisi hali halisi ya uwekezaji iliyofanywa na Serikali/TANESCO kwa miaka mingi iliyopita kabla hata ya Shirika la TANESCO halijawekwa kwenye orodha ya kubinafsishwa mwaka 1997-2005.
4. Ndugu Wanahabari, baada ya Serikali kubatilisha uamuzi wa kulibinafsisha Shirika la TANESCO mwezi Septemba, 2005 na baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani, mwaka 2006 ilibuni miradi minne (4) ya uzalishaji wa umeme usiotegemea maji, lengo ikiwa ni kuiondoa nchi kutoka kwenye utegemezi wa umeme unaotokana na maji na kuifanya nchi itegemee vyanzo vingine vya uhakika zaidi visivyoweza kuathiriwa na uhaba wa mvua.
5. Ndugu Wanahabari, miradi hiyo minne (4) iliyobuniwa na Serikali ya Awamu ya Nne na iliyokusudiwa kuongeza kiasi cha umeme unaozalishwa kwenye gridi ya Taifa (MW 645) ni ifuatayo:-
(i) Kiwira (Mbeya) – makaa ya mawe (MW 200), uliotarajiwa kukamilika mwaka 2009/2010.
(ii) Mnazi Bay (Mtwara) – gesi asili – (MW 300) uliotarajiwa kukamilika mwaka 2010.
(iii) Mitambo ya kuzalisha umeme (gesi asili) MW 100 ulionunuliwa na Serikali/TANESCO na kufungwa Ubungo, ulianza kazi mwaka 2008.
(iv) Mitambo ya kuzalisha umeme kutokana na gesi asili (MW 45) iliyonunuliwa na Serikali/TANESCO na kufungwa Tegeta – Dar es Salaam, ilianza kazi mwaka 2009 mwishoni.
Hivyo, dhamira ya Serikali ilikuwa kuongeza kwenye gridi ya Taifa MW 645 kwa kipindi cha mwaka 2006-2010.
6. Ndugu Wanahabari, hata hivyo, pamoja na dhamira hiyo njema ya Serikali, ni bahati mbaya kwamba kati ya MW 645 zilizotarajiwa kuzalishwa kwa kipindi cha mwaka 2006-2010, ni MW 145 tu (Ubungo MW 100 na Tegeta MW 45) ndizo zilizopatikana baada ya mradi wa Kiwira (MW 200) kukwama kukamilika ndani ya wakati kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kasoro za mchakato wa ubinafsishaji wake. Aidha, mradi wa Mnazi Bay Mtwara (MW 300) ulichelewa kukamilika kama ilivyokusudiwa awali kutokana na mdororo wa kiuchumi ulioikumba dunia miaka ya 2007-2009.
7. Ndugu Wanahabari, kama ambavyo Serikali/TANESCO, tumekuwa tunautaarifu umma mara kwa mara, ili kukabiliana na mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa Serikali imejielekeza katika mipango ya dharura na muda mfupi, wakati utekelezaji wa miradi ya muda wa kati na mrefu ukiendelea.
8. Ndugu Wanahabari, kuhusu mpango wa dharura, tayari TANESCO wameishapata kampuni ya Symbion (MW 112.5) ambayo tayari imeshaanza uzalishaji hadi kufikia MW 80 kwa sasa. Aidha, TANESCO wamefunga mkataba na kampuni ya Aggreko (MW 100) ambayo kufikia mwishoni mwa mwezi wa Agosti itakuwa inazalisha MW 100 (dizeli).
Aidha, Wizara yangu imehakikishiwa na Wizara ya Fedha kwamba fedha za kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL (MW 100) zimeishapatikana, hivyo kiwango cha uzalishaji umeme cha mitambo hiyo kitaongezeka kutoka MW 10 kwa sasa hadi MW 100 wiki ijayo.
9. Ndugu Wanahabari, miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ni:-
(a) Ufungaji wa mitambo ya kuzalisha MW 100 (gesi asili) jijini Dar es Salaam ifikapo Desemba, 2011; na
(b) Ufungaji wa mitambo ya kuzalisha MW 60 (dizeli) jijini Mwanza mwanzoni mwa mwaka 2012.
10. Ndugu Wanahabari, miradi itakayotekelezwa katika kipindi cha muda mfupi ni:-
(i) Kinyerezi – MW 240 (2013/2014) - gesi asili
(ii) Somanga Fungu – MW 230 (2013/2014) - gesi asili
(iii) Mnazi Bay – MW 300 (2013/2014) - gesi asili
(iv) Kiwira – MW 200 (2013/2014) - makaa ya mawe.
Utekelezaji wa miradi hii niliyoitaja ni sehemu ya mkakati wa kufikia lengo la kuzalisha MW 2780 au zaidi ifikapo mwaka 2015 kama ilivyobainishwa kwenye Mpango wa miaka 5 wa Maendeleo wa Taifa uliozinduliwa na Serikali na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni. Miradi mingine ya uzalishaji wa umeme itakayotekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo ni pamoja na Mchuchuma/Linganga MW 600 (makaa ya mawe); Ngaka MW 400 (makaa ya mawe); Ruhudji MW 358 (maji); Mpanga MW 165 (maji) na miradi ya upepo Singida.
Aidha, utekelezaji wa miradi hii utachangia kutuwezesha kufikia lengo la kuwafikishia asilimia 30 ya Watanzania huduma ya umeme ifikapo mwaka 2015. Sambamba na miradi ya uzalishaji umeme Serikali kupitia TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo mfano MCC, Sida, AfDB, JICA, Benki ya Dunia, n.k. inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usafirishaji na usambazaji umeme nchini.
HITIMISHO
(1) Serikali na TANESCO tunaguswa na kukerwa na adha na usumbufu unaosababishwa na mgawo wa umeme kama wanavyokerwa wananchi wote wa Tanzania.
(2) Tunaendelea kuwaomba wananchi waelewe kwamba mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa umesababishwa na upungufu wa mvua zilizonyesha mwaka huu, hivyo kutojaza mabwawa yetu yanayozalisha umeme kwa kuzingatia kwamba takribani asilimia 55 (55%) ya umeme wetu kwenye gridi ya Taifa unatokana na maji.
(3) Tunawaomba Watanzania waelewe kwamba utegemezi wetu wa umeme kwa asilimia 55 kutokana na maji si dhambi, kosa la makusudi wala uzembe bali ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa nia njema kama zilivyofanya nchi nyingi duniani. Mabadiliko ya tabia nchi miaka ya hivi karibuni duniani yamekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi zinazotegemea, kwa kiasi kukubwa, umeme wa maji.
(4) Kwa kutambua athari za utegemezi, kwa kiasi kikubwa, wa umeme utokanao na chanzo kimoja cha umeme, Serikali ya Awamu ya Nne kupitia shirika la TANESCO imebuni na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa kipindi cha muda mfupi ya kuzalisha umeme utokanao na gesi asili na makaa ya mawe ili kukabiliana na mgawo wa umeme kama ilivyobainishwa hapo juu.
(5) Tunapenda kuwakumbusha wananchi kwamba isingekuwa mdororo wa kiuchumi duniani ulioathiri utekelezaji wa mradi wa Mnazi Bay (MW 300) na kuchelewa utekelezaji wa mradi wa Kiwira (MW 200), mambo ambayo yalitokea bila kutarajiwa, tatizo la umeme nchini leo hii lisingekuwepo, maana miradi hii ingekuwa imetuondoa kwenye utegemezi wa umeme wa maji wa zaidi ya asilimia 50.
(6) Kwa vile mgawo wa umeme ni janga la kitaifa linaloathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Taifa, na kwa vile mipango ya Serikali/TANESCO kukabiliana na mgawo wa umeme kupitia miradi iliyotajwa hapo juu ni dhahiri, yenye tija na inayotekelezeka, tunawaomba wananchi waivumilie Serikali/TANESCO wakati inaendelea kutekeleza miradi hiyo na wapuuze kabisa dhihaka, kejeri na kebei zozote zinazofanywa na baadhi ya watu wasiothamini juhudi na jitihada za kweli zinazofanywa na Serikali/TANESCO kumaliza tatizo la mgawo wa umeme nchini. Serikali inaamini kwamba watu wote wanaopuuza na kubeza jitihada hizi za Serikali na TANESCO wakati wanajua historia liliyopitia shirika la TANESCO (kutofanyika uwekezaji kwa kipindi ambacho liliwekwa kwenye orodha ya kubinafsishwa – 1997-2005) wanafanya hivyo kwa makusudi na kwa maslahi yao binafsi, ikiwemo maslahi binafsi ya kupata umaarufu wa kisiasa. Tunawaomba wananchi wawapuuze watu wa namna hii!!!!
(7) Tatizo la mgawo wa umeme kwa nchi yetu ni tatizo halisi kama vile tatizo hilo lilivyoikumba nchi ya Japan kwa sasa kutokana na matatizo halisi ya kuathirika kwa vyanzo vya umeme (kuharibika kwa mitambo ya nuklia kutokana na tetemeko la ardhi). Pamoja na tatizo lililowakumba Wajapan ambalo kimsingi limechangiwa na utegemezi kwa kiasi kikubwa, wa umeme wa nuklia, bado taifa hilo limeendelea kushikamana wakati wote. Ikumbukwe kwamba Japan ni miongoni mwa nchi tatu tajiri sana na zenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani. Suluhu ya tatizo hili siyo kubeza juhudi zinazofanywa na Serikali/TANESCO bali ni kuunganisha nguvu za wadau wote kuitia moyo Serikali/TANESCO kwa hatua za dharura zinazochukuliwa na miradi inayoendelea kutekelezwa kukabiliana na mgawo wa umeme nchini.
(8) Tunawaomba wananchi waendelee kuvumilia, tuimarishe mshikamano, utulivu na amani na tuwaepuke wote wanaobeza juhudi za Serikali na TANESCO kutatua tatizo la mgawo wa umeme kwa maslahi yao binafsi ikiwa ni pamoja na maslahi ya kisiasa.
(9) Sambamba na utekelezaji wa miradi ya dharura na ile ya muda mfupi unaoendelea, Serikali na taasisi zake za TPDC na TANESCO na kwa kushirikiana na China inaendelea na mpango wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara-Dar es Salaam-Tanga. Upatikanaji wa gesi nyingi zaidi utaharakisha kufikia lengo letu la kutegemea zaidi umeme unaotokana na gesi asili badala ya maji.
Mungu ibariki Tanzania.
Asanteni.
William M. Ngeleja (Mb.)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI