Pages

June 23, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MPR/PR/12                                                                                     23/06/2011


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linasikitika kuwajulisha wateja wake na wananchi kwa ujumla kuwa limelazimika kuongeza mgawo wa umeme kwa mikoa yote iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa ikiwa ni pamoja na Zanzibar.
Hadi kufikia jana (Juni 22), 2011 kina cha maji ya Mtera ni mita 690.88 tu juu ya usawa wa bahari. Kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 wakati kina cha chini kisichoruhusu ufuaji umeme ni mita 690 juu ya usawa wa bahari.
Ongezeko la mgawo wa umeme linatokana na sababu zifuatazo:
1.  Upungufu mkubwa wa maji katika mabwawa yetu ya kufua umeme hususani mabwawa ya Mtera, Kidatu, Hale, Kihansi na Nyumba ya Mungu. Uhaba huo umetokana na uhaba wa mvua katika vyanzo vya maji vinavyojaza mabwawa hayo hivyo kuathiri ufuaji umeme.
2.  Uhaba wa mafuta wa kuendeshea mitambo ya kufulia umeme ya IPTL na hivyo kusababisha upungufu wa ufuaji umeme kutoka Megawati 100 had Megawati 10 kwa sasa.

Jitihada zinazofanyika ili kukabiliana na tatizo hili:
1.  Serikali kupitia Wizara za Fedha na Uchumi na Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kwa ajili ya manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL.
2.  Kampuni ya kufua umeme ya Symbion kuanza uzalishaji wa MW 80 amabazo zimeingizwa kwenye gridi ya Taifa.
3.  Shirika limekwisha ingia mkataba wa kufua umeme wa MW 100 na Kampuni ya Aggreko na inategemewa kuwa Mwezi wa Nane mwaka huu uzalishaji utaanza rasmi.
4.  Mipango inaendelea ya kuongeza mitambo mingine ya kufua umeme ikiwa ni pamoja na mtambo wa Ubungo wa MW 100 na ule wa Mwanza wa MW 60 ambayo ujenzi wake umeshaanza.
HITIMISHO
Shirika linawaomba radhi wateja wake na wananchi kwa ujumla kutokana na usumbufu wote uliosababishwa na tatizo hili la mgawo wa umeme.
Hivyo basi tunawaomba wateja wetu na wananchi kwa ujumla watuvumilie na kutupa ushirikiano katika kipindi hiki kigumu kwa taifa letu.
Vilevile tunawashauri wateja wetu kuwa waangalifu kwa kuepeuka matumizi ya umeme yasiyo ya lazima katika kipindi hiki cha upungufu wa umeme.

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO –MAKAO MAKUU.

1 comment:

  1. WEWE UKIOMBA VIATU WENZIO WANAOMBA MIGUU.HUKU KWETU KITUNDA MZINGA -TSUNAMI MKOA WA ILALA WILAYA YA GONGO LA MBOTO KWA MZEE NJOVU HATUUFAHAMU HATA HUO UMEME WA MGAWO.
    LAKINI JANA KAMA NDOTO TANESCO WAMEANZA KUSAMBAZA NGUZO.HILI JAMBO LA KUTIA MOYO NA LINASTAHILI SHUKRANI KWA WATOA HUDUMA WETU WA TANESCO.KARIBUNI SANA KITUNDA MZINGA-TSUNAMI
    KWA MZEE NJOVU MUYAANGAZIE MAISHA YETU KUPITIA NISHATI YA UMEME.KILA KUENDAKO HISANI HAKURUDI
    NUKSANI BALI SHUKRANI.

    Ray E.Njau
    Kitunda Mzinga -Tsunami kwa Mzee Njovu

    ReplyDelete