Pages

February 25, 2019

HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawaomba radhi Wateja wake wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kukosa huduma ya umeme kwa siku za hivi karibuni kutokana na maboresho makubwa yanayohusisha matengenezo kinga ya mashine 3 za Kituo cha Ubungo II, pamoja na uwekaji wa transfoma kubwa la MVA 300 kwenye Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo ili kukiongezea uwezo na kwenda sambamba na ukuaji wa mahitaji ya jiji la Dar es Salaam.

 Kabla ya matengenezo kuanza mnamo Januari 2019 Kituo hiki cha kupoza umeme cha Ubungo kimekuwa kinapokea umeme kutoka katika vituo vya Uzalishaji umeme vilivyopo upande wa msongo wa kilovolti 220 kupitia transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 150 kila moja, zenye kupokea umeme wa msongo wa Kilovolti  220 na kuushusha hadi kuwa msongo wa Kilovolti 132  katika transforma namba sita na namba  saba za kituo cha Ubungo na  vituo vya uzalishaji umeme vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovolti 132 ambavyo vimeungwa moja kwa moja kwenye mfumo mkuu wa usambazaji umeme  kwa Dar es Salaam na Zanzibar.

Kutokana na matengenezo yanayoendelea vituo vya uzalishaji umeme vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovoti 132 na 33 vimekuwa nguzo kubwa ya upatikanaji wa umeme. Vituo hivyo ni Ubungo II na Tegeta.

Shirika kupitia wataalamu wake tayari limefanya jitihada kubwa za kupunguza athari za upungufu wa upatikanaji wa umeme kwa wakaazi wa Dar es salaam na Zanzibar kwa kufanya yafuatayo:

Mosi, Kufungua laini ya msongo wa kilovoti 132 kati ya Kilimanjaro na Hale: Hili hufanyika ili kutoruhusu umeme wa kutoka Dar es Salaam na Morogoro kwenda Kilimanjaro hivyo Mkoa huu kuchukulia kwenye upande wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Arusha.

Pili , Kuwezesha upatikanaji wa umeme katika baadhi ya  maeneo ya Mkoa wa Dar es salaam, kwa kuunga baadhi ya njia za Usafirishaji  umeme kutoka Kituo cha Kinyerezi, Gongolamboto hadi Mbagala ili kuwezesha maeneo hayo kupata umeme bila kupitia kituo cha Ubungo  ambacho kipo katika matengenezo.

Tatu, Kufungua njia ya umeme ya kilovolti 132 itokayo Kituo cha Kunduchi   hadi Mlandizi na kuunga maeneo hayo katika njia ya umeme ya kilovolti 132 itokayo Morogoro ili kuwezesha jiji la Dar es salaam kuwa na umeme wa uhakika.

Nne, Kufungua laini ya msongo wa kilovolti 132 kati ya Ubungo na Chalinze upande wa Ubungo ili kutozihusisha transfoma za Ubungo kwenye mzigo wa mikoa mingine na hivyo kutumika kuhudumia  wateja wa  Dar es Salaam na Zanzibar pekee.
 Tunatarajia matengenezo haya yanayokwenda kwa awamu yatakamilika ifikapo mwezi Juni 2019.

TANESCO itaendelea kutoa taarifa ya Maendeleo ya kazi ya matengenezo ya kituo cha Ubungo yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika Dar es salaam na Zanzibar kwa siku zijazo.


Imetolewa na:  Ofisi ya Uhusiano
                                TANESCO-Makao Makuu


No comments:

Post a Comment