February 17, 2011

EMPLOYMENT OPPORTUNITIES - TANESCO

Click here to download a document that shows different Employment Opportunities
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI




KAULI YA SERIKALI KUHUSU HALI YA UMEME NCHINI NA UTEKELEZAJI
 WA MIRADI YA UMEME KATIKA KIPINDI KIFUPI NA CHA KATI ILIYOWASILISHWA NA MHE. WILLIAM M. NGELEJA (MB.),
 WAZIRI WA NISHATI NA MADINI


Mheshimiwa Spika, kufuatia maelekezo yako uliyoyatoa tarehe 11 Februari, 2011 kwa Wizara ya Nishati na Madini wakati wa majibu ya maswali ya nyongeza ya Swali Namba 39 na kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007, Kanuni Na. 49, naomba kutoa Kauli ya Serikali kuhusu HALI YA UMEME NCHINI NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UMEME KATIKA KIPINDI KIFUPI NA CHA KATI kama ifuatavyo:-


UTANGULIZI

1.    Mheshimiwa Spika, uwezo halisi wa mitambo yote ya kuzalisha umeme (installed capacity) katika gridi ya Taifa ni MW 1006, mitambo ya maji ikiwa na uwezo wa MW 561 na mitambo ya gesi asili na mafuta ikiwa na uwezo wa MW 445.  Kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi na umri wa mitambo uwezo wa kuzalisha umeme hapa nchini katika mfumo wa gridi ya Taifa bila kuwepo mgawo wa umeme ni MW 935, ambapo MW 523 (56%) hutokana na maji, MW 322 (34.4%) hutokana na gesi asili na MW 90 (9.6%) kutokana na mafuta mazito.

Kina cha maji katika bwawa mhimili la Mtera kufikia tarehe 14/2/2011 kilikuwa kimeshuka hadi kufikia mita 691.31 juu ya usawa wa bahari, hii ikiwa ni mita 1.31 tu juu ya kina cha chini kinachoweza kuruhusu uzalishaji wa umeme katika bwawa hilo ambacho ni mita 690.0. Kutokana na hali hii ya uhaba wa maji kwa sasa, mitambo ya maji inazalisha kwa sasa wastani wa MW 180 tu, wakati mitambo ya mafuta na gesi asili ikizalisha wastani wa MW 290. Hii inafanya jumla ya umeme wote unaopatikana kwenye gridi ya Taifa kuwa wastani wa MW 470 tu ambayo ni asilimia 67 tu ya mahitaji ya wastani ya umeme au asilimia 57 tu ya mahitaji ya juu katika gridi ya Taifa (MW 833).  Hii inaleta upungufu wa wastani wa MW 230 kwenye gridi ya Taifa. Upungufu huu ndio unaosababisha mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa. Serikali imenunua mafuta ya kuendesha mtambo wa IPTL ili kuzalisha MW 80 kwa siku kutoka MW 10 kwa siku kama ilivyokuwa awali kabla ya kununua mafuta.

2.    Mheshimiwa Spika, mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa kasi ya wastani wa kati ya MW 80 -120 kwa mwaka. Kasi ya uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme imekuwa haimudu ongezeko hili kiasi kwamba mfumo wa uzalishaji umeme unaendeshwa pasipokuwa na umeme wa akiba (reserve margin). Hali hii imesababisha kuwepo kwa mgawo wa umeme wa mara kwa mara hata itokeapo hitilafu kidogo tu kwenye mfumo wa gridi ya Taifa.  Pamoja na upungufu wa maji katika mabwawa yetu, kutofanyika uwekezaji wa kutosha katika miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kipindi kirefu, hususan kipindi kati ya mwaka 1997 hadi 2005 ambapo TANESCO iliwekwa chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Kubinafsisha Mashirika ya Umma (Public Sector Reform Commission) ikisubiri kubinafsishwa ni moja ya sababu zilizosababisha uwezo wa mfumo wa gridi ya Taifa kuzidiwa na mahitaji leo hii. 

3.    Mheshimiwa Spika, aidha, chini ya uendeshaji (management contract) wa Net Group Solutions mwaka 2004 – 2006 hapakuwa na uwekezaji kwenye miundombinu na hivyo kufanya upatikanaji wa umeme kutokuwa wa kuaminika kutokana na uchakavu wa miundombinu hiyo. Pamoja na kutokuwa na uwekezaji wa kukidhi mahitaji ya sekta, upatikanaji wa nishati ya umeme katika mfumo wa gridi ya Taifa pia umekuwa ukiathiriwa na uhaba wa mvua kwa kipindi kirefu. Kwa mfano, mwaka 2006 uzalishaji wa umeme uliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na uhaba wa mvua  katika nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2003 hadi 2005. Katika kipindi hicho, uzalishaji umeme katika  vituo vinavyotumia nguvu za maji ulishuka kwa zaidi ya asilimia 60 baada ya kina cha maji katika bwawa la Mtera kushuka chini ya kina cha chini cha mita 690.0 juu ya usawa wa bahari. Upungufu mkubwa wa maji kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme ulilazimisha TANESCO kutoa umeme kwa mgawo katika mikoa yote iliyounganishwa kwenye mfumo wa gridi ya Taifa.

4.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 Serikali ilichukua hatua za dharura za (i) kukodisha mitambo yenye uwezo wa kuzalisha MW185 kutoka Richmond/Dowans (MW 105), Alstom (MW 40) na Aggreko (MW 40); na ii) kununua na kujenga mitambo ya kudumu ya kuzalisha umeme wa MW145 – Ubungo MW 100 na Tegeta MW 45.  Zaidi ya hapo, Serikali ilichukua tahadhari ya kuzuia mgawo usijirudie tena kwa kuchukua hatua zifuatazo:- (i) kuhamasisha uzalishaji umeme wa MW 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira; na (ii) kuhamasisha uzalishaji wa MW 300 kwa kutumia gesi asili ya Mnazi Bay - Mtwara. Miradi hii ambayo ilitarajiwa kuanza uzalishaji kabla ya mwisho wa mwaka 2010 haikutekelezwa kama ilivyopangwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mdororo wa uchumi duniani mwaka 2008 ulioathiri mradi wa umeme wa Mtwara ambapo  mwekezaji alilazimika kuahirisha uendelezaji wa mradi huo. Mradi wa kuzalisha umeme wa Kiwira ulisitishwa kufuatia dosari zilizojitokeza wakati wa ubinafsishaji wa mgodi.  

5.    Mheshimiwa Spika, mgawo wa umeme huleta hasara kubwa kiuchumi na usumbufu mkubwa kwa jamii. Tathmini kuhusu athari za mgawo wa mwaka 2006 ilionesha kwamba Serikali ilipata hasara ya Dola za Marekani milioni 331.309 kutokana na TANESCO kutokutoa huduma ya umeme (unserved energy) ya jumla ya uniti 287,539,296.

6.    Mheshimiwa Spika, upungufu wa umeme ulijirudia tena mwaka 2009 katika miezi ya Septemba na Novemba ambapo takriban MW 160 zilikosekana kwenye mfumo wa gridi kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme pamoja na kuharibika kwa mitambo ya TANESCO na Songas kwa wakati mmoja. Katika kipindi cha mwishoni mwa Desemba 2010 na Januari 2011, upungufu uliongezeka kutokana na matatizo ya kiufundi katika moja ya visima vya gesi asili huko Songo Songo kisiwani, pamoja na matengenezo ya mitambo ya umeme wa gesi hapa Dar es Salaam. Aidha, Kwa sasa matatizo hayo yamepatiwa ufumbuzi na mitambo inafanya kazi vizuri. Serikali ilichukua hatua za haraka kwa kupendekeza mitambo ya IPTL itumike kufua umeme kwa Mkataba wa kipindi cha mpito (Interim Power Purchase Agreement – IPPA kati ya TANESCO na IPTL) wa miezi sita kuanzia mwezi Novemba, 2009 hadi Aprili, 2010.

7.    Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kuendesha mitambo ya IPTL ulifanyika kwa makubaliano ya msingi ya kuiomba Serikali kununua mafuta pamoja na kulipia sehemu ya gharama za kuendesha mitambo hiyo. Aidha, Serikali ililazimika kutenga kiasi cha Sh bilioni 46.4 kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa mafuta mazito ya mitambo ya IPTL kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Novemba, 2010 hadi Februari, 2011 ili kuimarisha kiwango cha uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa.

8.    Mheshimiwa Spika, tathimini (iliyofanywa na watalaamu wa TANESCO na Wizara) inaonesha kwamba patakuwepo na upungufu wa wastani wa MW 264 katika mwaka wa 2011 kwenye mfumo wa gridi ya Taifa ikiwa hali ya ukame itaendelea kuwa kama ilivyo sasa. Aidha, kufuatia taarifa za hivi karibuni za Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa, hata mvua zikinyesha kwa wingi bado nchi yetu itakumbwa na upungufu wa umeme wa wastani wa MW 67 mwaka wa 2011 kutokana na sababu zifuatazo:-

(a)      Mahitaji ya umeme kuongezeka kwa kasi kuliko uwekezaji katika miradi mipya ya kuzalisha umeme ambapo mwaka 2008 mahitaji ya juu (Peak Demand) yalikuwa MW 729 na mwaka jana 2010 mahitaji ya juu yalifika MW 833; na
(b)      Kupungua kwa maji katika bwawa la Mtera kulikosababisha uwezo wa kuzalisha umeme kuwa chini ya nusu. Hadi kufikia tarehe 14/02/2011 kina cha maji katika bwawa la Mtera kilikuwa mita 691.31 juu ya usawa wa bahari au mita 1.31 tu zilizosalia kwenye bwawa hilo ili kufikia kina cha chini (mita 690.0). Likiwa limejaa bwawa hilo linakuwa na maji ya mita 698.50.

9.    Mheshimiwa Spika, hata hivyo, pengo la MW 67 linaweza kuzibwa endapo Serikali itaendelea kutoa fedha za kutosha na kwa wakati za kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL kwa uwezo wake wote (MW 80) na kama mvua za kutosha zitanyesha kujaza mabwawa yetu.

HATUA ZA DHARURA ZA KUONDOKANA NA MGAWO WA UMEME NCHINI
10. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa umeme uliosababisha mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na TANESCO imechukua hatua zifuatazo:-
(a)      Kuhakikisha fedha za kununulia  mafuta ya kuendesha kituo cha kuzalisha umeme cha IPTL zinaendelea kupatikana kwa wakati ili kituo kiweze kuzalisha katika kiwango chake cha juu cha MW 80.
(b)      Kuhakikisha kwamba miradi ya kudumu ya kuzalisha umeme, MW 100 itakayofungwa Ubungo, Dar es Salaam ya kutumia gesi asili na mitambo ya MW 60 itakayofungwa Mwanza ya kutumia mafuta mazito  (HFO) inakamilishwa ndani ya wakati kama ilivyopangwa mwezi Desemba 2011 au Januari, 2012.
(c)       Kuharakisha mchakato wa kukodi mitambo ya dharura yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya MW 260, endapo mvua za kutosha hazitanyesha kuwezesha ongezeko la umeme utokanao na maji.
(d)      Kutekeleza mpango wa kupanua miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi kutoka kweye visima vya Songo Songo hadi Dar es Salaam.
(e)      Kuendelea kutekeleza miradi ya kupunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 ilivyo sasa  hadi asilimia 15 kati ya mwaka 2011 – 2015.
(f)       TANESCO kusimamia mgawo wa umeme kwa makini zaidi na kuhakikisha kwamba umeme kwenye shughuli za uzalishaji na sehemu nyingine nyeti za huduma za jamii, ulinzi na usalama unaendelea kupatikana.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UMEME KWA KIPINDI CHA MUDA MFUPI (2011 – 2015)

          Miradi ya Uzalishaji (Generation)
11.   Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na TANESCO inaendelea kusimamia utekelezaji wa programu ya  kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme katika kipindi kifupi cha 2011-2015, ili kuepusha tatizo la mgawo wa umeme siku za usoni kama ifuatavyo:-
(a)       Ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme MW 160 ambapo mitambo ya MW 100 ya kutumia gesi asili itafungwa Ubungo, Dar es Salaam na mitambo ya MW 60 ya kutumia mafuta mazito (HFO) itafungwa Mwanza.
(b)       Ujenzi wa mitambo ya kutumia gesi asili ya Songo Songo na Mnazi Bay (MW 870) kwa mpangilio ufuatao:-

·         Kinyerezi MW 240 (2013, Sumitomo Corporation), mradi utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 510 na mchango wa Serikali ni Dola za Marekani milioni 10;

·         Mnazi Bay MW 300 (2013, CMEC, Mkataba wa EPC umesainiwa), mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 660 na mchango wa Serikali ni Dola za Marekani milioni 132; na

·         Somanga Fungu, Kilwa MW 230 (2013, ProEnergy Services), mradi utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 350;

(c)      Makaa ya mawe ya Kiwira, Mchuchuma na Ngaka (MW 1200) kwa mpangilio ufuatao:-

·         Kiwira MW 200 (2013, China Exim Bank/Serikali/NSSF, mradi utagharimu takribani Dola za Marekani milioni 400;

·         Mchuchuma MW 600 (2015, NDC, mwendelezaji ameshapatikana), mradi utagharimu takribani Dola za Marekani milioni 1000, mchango wa Serikali Dola za Marekani milioni 250; na

·         Ngaka MW 400  (2015, TANCOAL Energy Ltd, tathmini ya kitaalam inaendelea), gharama zinakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni moja.

(d)      Miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya upepo mkoani Singida MW 100 (2012, Wind East Africa Ltd, mradi utagharimu takribani Dola za Marekani milioni 250 na utaendelezwa na sekta binafsi bila mchango wa Serikali, na ule unaoendelezwa na Power Pool E. A. Limited (MW 50, mwaka 2013) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 123.

(e)      Miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji (hydro) inayohusisha kuongeza umeme wa MW 600 kupitia miradi ifuatayo kwa kipindi cha mwaka 2011 - 2018:-

·         Rusumo MW 20 (2015); (Serikali za Tanzania, Rwanda na Burundi), Upembuzi yakinifu unaendelea; kituo cha uzalishaji kitagharimu Dola za Marekani milioni 85.65 na njia za usafirishaji umeme zitagharimu Dola za Marekani milioni 77.4;
           
·         Ruhudji MW 358 (2016, Aldwych, majadiliano na mwendelezaji mradi yanaendelea), mradi utaendelezwa na sekta binafsi kwa gharama ya takribani Dola za Marekani milioni 900; na

·         Rumakali MW 222 (2018, Zarubezhstory OJSC, MoU imesainiwa mwezi Septemba, 2010), mradi utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 450.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ni pamoja na:-

·         Miradi ya Mpanga (MW 144) na Stiegler’s Gorge (MW 2100) ambayo Serikali inaendelea kutafuta wafadhili/waendelezaji.

·          Miradi ya EWURA ya kuzalisha umeme usiozidi MW 10
Kufuatia uanzishwaji wa utaratibu wa kurahisisha uwekezaji katika miradi midogo ya kuzalisha umeme isiyozidi MW 10 chini ya utaratibu ujulikanao kama Small Power Purchase Agreement (SPPA) unaosimamiwa na EWURA, EWURA imetoa leseni kwa wawekezaji watano (5) ambao watazalisha MW 10 kila mmoja na wengine 21 wameomba leseni ambapo maombi yao yanashughulikiwa. Kampuni tano (5) zimeshasaini Small Power Purchase Agreement (SPPA) na TANESCO. Kampuni hizo ni Tanwat (Biomass, MW 2.5, TANESCO MW 1.4) na TPC Moshi (co-generation, MW 17.5, TANESCO MW 9.0) ambazo zimepewa leseni za mwaka mmoja ili EWURA ikamilishe licence template. Kampuni za Sao Hill Energy Ltd (Biomass, MW 15.7), Mwenga Hydro Ltd (Mini hydro, MW 4.00) na Ngombeni Power Ltd (Mafia-Biomass, MW 1.4) zimepewa provisional licence kwa miezi 30 ili zikamilishe miradi yao. Ifikapo mwaka 2012 kampuni hizo tatu zitaanza kuzalisha umeme.
·         Miradi chini ya ufadhili wa ORIO (taasisi ya Uholanzi)
Serikali itafunga mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 2.5 katika kila miji ya Ngara, Biharamulo na Mpanda ifikapo mwaka 2013 ili kuimarisha huduma za umeme katika miji hii wakati juhudi za Serikali kuiunganisha Mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa kwenye gridi ya Taifa zinaendelea.

Miradi  ya Usafirishaji na Usambazaji (Transmission & Distribution) Umeme
12.     Mheshimiwa Spika, sambamba na utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na TANESCO inaendeleza miradi ya kuimarisha na kupanua miundombinu ya kusafirisha umeme kwa lengo la kufikisha kwa wateja umeme utakaozalishwa chini ya programu niliyoieleza na kuipatia umeme wa gridi Mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa, kama ifuatavyo:-

(a)      Tanzania Energy Development and Access Expansion Project (TEDAP) - Dar Es Salaam, Arusha na kilimanjaro, 132kV, (2015, WB (IDA), utekelezaji unaendelea); Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 55 kwa usambazaji wa umeme na Dola milioni 34.252 kwa miradi ya usafirishaji umeme;

(b)      Mkataba wa ujenzi wa laini ya Mtwara-Singida DC line 330kV (2013, CEMC, EPC imesainiwa);

(c)Bulyanhulu-Geita 220kV (2014, BADEA/OFID, fedha zimepatikana); mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 28.8;

(d)      Geita–Nyakanazi kV 220 (2014, BADEA/OFID,  mazungumzo yanaendelea kuhusu ufadhili); gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 4.5;

(e)      Morogoro–Tanga–Moshi –Arusha kv 400 (2015, Exim  Bank ya China, MoU imeshasaniwa, Technical proposal zinapitiwa na TANESCO); mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 75;

(f)       Singida - Arusha kV 400 (2015, RSMI/GENIVAR, upembuzi yakinifu unaendelea na utakamilika Februari, 2012); gharama za mradi ni Dola za marekani milioni 190, Serikali itachangia Dola za Marekani milioni 28.5;

(g)      North – West Grid extension – kuunganisha Mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa kwenye gridi ya Taifa kV 220 (2015, Exim Bank ya China, MoU imeshasainiwa, matayarisho ya upembuzi yakinifu yanaendelea); mradi utagharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 226, mchango wa Serikali ni Dola za Marekani milioni 34; na

(h)      Serikali za Zambia, Tanzania na Kenya zinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuunganisha miundo mbinu ya usafirishaji umeme katika nchi hizi (ZTK - Interconnector Project).

13.     Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa mradi wa Iringa-Shinyanga Backbone Transmission Investment ambao mchakato wa ujenzi wake umepangwa kuanza robo ya kwanza ya mwaka 2011 baada ya Serikali kukamilisha zoezi la kupata fedha kiasi cha Dola za Marekani milioni 550 mwezi Desemba, 2010 kwa ajili ya  ujenzi wa mradi. Mradi huu umefadhiliwa kwa pamoja na World Bank (WB), JICA, EIB, AfDB na Korea EDCF.
14.    Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya usafirishaji na usambazaji umeme na hatua iliyofikiwa ni kama ifuatavyo:-
(a)      Makambako-Songea: Mradi huu unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 70.4  kutoka Serikali ya Uswidi kupitia Shirika lake la Maendeleo (Sida). ‘Specific  Agreement’ na ‘Credit Agreement’ za mradi  zilisainiwa tarehe 16 Decemba, 2008 na tarehe 10 Agosti, 2010 sawia. Kwa sasa taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Februari, 2011. Mradi unatarajiwa kuanza kutekelezwa  mwezi Oktoba 2011 na  kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014 na utahusisha kazi zifuatazo:

·           Ujenzi wa laini ya umeme ya msongo wa kilovolti 132  ya urefu wa kilometa 250 kutoka Makambako hadi Songea; na
·           Ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya kV 132/33 katika maeneo ya Madaba na Songea.

(b)      Mradi wa Electricity V: Huu ni mradi wa kuboresha na kuendeleza miundombimu ya umeme kwa ajili ya huduma za kiuchumi na kijamii maeneo ya vijijini, makao makuu ya wilaya na pembezoni mwa miji katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Shinyanga na Dar es Salaam. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania bilioni 60, chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mshauri atapatikana mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, 2011, ili makabrasha ya zabuni yaandaliwe.

(c)       Mradi unaofadhiliwa na Millenium Challenge Corporation(MCC) : Mradi huu umegawanyika katika sehemu zifuatazo:-

·       Mradi wa Zanzibar Interconnector Project. Katika mradi huu inajengwa njia mpya ya pili ya kupeleka umeme Zanzibar. Mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 63.125. Kwa sasa Mkandarasi ameishapatikana na anafanya route survey ya mwisho na matarajio ni kukamilika kwa ujenzi wa mradi mwishoni mwa mwaka 2012;

·       Malagarasi Hydropower and Kigoma Distribution Project – Mradi wa kupata umeme wa MW 8 kutokana na nguvu za maji ya Mto Malagarasi na kujenga miundombinu ya kusambaza umeme Kigoma, Uvinza na Kasulu. Mradi huu unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 53.68. Upembuzi yakinifu wa mradi wa kuzalisha umeme wa mto Malagarasi ulikamilishwa mwezi Machi, 2010 na kubainisha kuwepo kwa konokono adimu. Kulingana na taratibu za masuala ya mazingira utekelezaji wa mradi ulisimama. Hata hivyo, MCC wamekubali  kufadhili upembuzi yakinifu mpya katika eneo lingine kwenye mto Malagarasi (Igamba III); na

·      Distribution Systems, Rehabilitation and Extension (T&D) Project - Huu ni mradi wa ukarabati na ujenzi wa laini za umeme kwenye mfumo wa usambazaji umeme kwa mikoa ya Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mwanza and Mbeya. Mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 89.666. Wakandarasi wa mradi wameishapatikana na wameishaanza  kazi ya mobilization na matarajio ni mradi kukamilika mwishoni mwa mwaka 2012.

(d)      Mradi chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mikoa 16
15.   Mheshimiwa Spika, mradi huu unafadhiliwa na Serikali kupitia mfuko wa Nishati Vijijini ulio chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Mbeya, Rukwa, Tabora, Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara na Shinyanga.  Mradi huu utagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 100.
16.   Mheshimiwa Spika, mradi utahusisha ujenzi wa njia  za umeme msongo wa kilovolti 33 na 11 jumla ya urefu wa kilometa 1600, ufungaji wa transfoma 350 za ukubwa tofauti, ujenzi wa njia za umeme msongo wa kilovolti 0.4 zenye jumla ya kilometa 900, na uunganishaji  wa wateja wapya wanaokadiriwa kufikia 20,000.  Utekelezaji wa mradi huu umeshaanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu 2011.

(e)      Mradi wa ununuzi wa jenereta katika Makao Makuu ya Wilaya za Sumbawanga, Kasulu, Kibondo, Nkasi na Namtumbo
17.   Mheshimiwa Spika, mradi huu unajumuisha ununuzi na ufungaji wa jenereta zenye uwezo wa kuzalisha MW 1.25 kila moja kutoka kwa mzabuni ambaye ni Kampuni ya Zwart Techniek ya Uholanzi. Utekelezaji wa mradi huu ni kama ifuatavyo:-

                                           (i)        Sumbawanga
Jenereta nne zenye uwezo wa kuzalisha MW 1.25 kila moja zitakamilika kufungwa mwezi Mei, 2011.
                                          (ii)        Namanyere (Nkasi)

Makao Makuu ya wilaya ya Nkasi (Namanyere) yanategemewa kupata huduma ya umeme kutoka mjini Sumbwanga baada ya kukamilika mradi wa ufungaji jenereta mjini Sumbawanga.

                                        (iii)        Loliondo (Ngorongoro)
Jenereta nne zenye uwezo wa kuzalisha MW 1.25 kila moja zitakamilika kufungwa mwezi Septemba, 2011.

                                        (iv)        Kasulu na Kibondo
Ilipangwa kuwa na jenereta 2 zenye uwezo wa kuzalisha MW 2.5 kwa kila wilaya; na
                                          (v)        Kazi ya ujenzi na ufungaji mashine imeishakamilika. Ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme (distribution) inaendelea kwa sasa na umeme utawashwa kuanzia mwezi Machi, 2011.
                                        (vi)        Mradi wa Namtumbo
Ufungaji wa jenereta yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 1.9 katika makao makuu ya Wilaya ya Namtumbo utakamilika mwezi Desemba, 2011.
                                       (vii)        Somanga Fungu
Kituo hiki kinazalisha umeme utokanao na gesi MW7.5 kwa ajili ya matumizi ya wilaya za Kilwa na Ikwiriri ambazo zinatumia kiasi ambacho hakizidi MW 2.5.
18.  Mheshimiwa Spika, Mpango Kabambe wa Umeme wa mwaka 2008 uliofanyiwa durusu mwaka 2009 (Power System Master Plan - PMSP 2009) unaonesha kwamba mahitaji ya juu ya umeme ya MW 833 yatakua na kufikia MW 1482 mwaka 2015, MW 2,218 mwaka 2020 na MW 6,091 mwaka 2033. Ili kuhimili ukuaji huo, hatua madhubuti  zinaendelea kuchukuliwa ili kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme hatua kwa hatua, kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya umeme inahimili na kukidhi mahitaji ya umeme katika kipindi kifupi, cha kati hadi kirefu, kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 63 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010.

          MIKAKATI YA KUENDELEZA SEKTA YA UMEME
19.  Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa vipaumbele 13 vya Dira ya Maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama ilivyoainishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake wakati akizindua Bunge la 10 pamoja na makisio ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii wa nchi yetu  utategemea upatikanaji wa nishati ya umeme ulio wa uhakika na unaokidhi mahitaji ya sekta zote za kiuchumi na kijamii. Ufanikishaji wa vipaumbele na utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kushamirisha uchumi na kupunguza umaskini nchini kama vile MKUKUTA II, Kilimo Kwanza na Malengo ya Maendeleo ya Milenia kwa pamoja unategemea uimarishaji wa sekta ya umeme kwa kujenga kwa wakati miradi iliyoainishwa katika Kauli hii.
20.  Mheshimiwa Spika, miradi ya kipaumbele iko katika makundi mawili yaani miradi itakayotekelezwa na sekta binafsi bila mchango wa Serikali na miradi itakayohitaji mchango wa Serikali katika hatua za mwanzo kulingana na masharti ya wakopeshaji fedha. Aidha, miradi ambayo inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia mia moja inabidi itengewe fedha za kutosha katika bajeti za Serikali.  Mahitaji hayo ni:-
(a)     Dola za Marekani, takribani, milioni 4,721 zinazohitajika kugharamia uwekezaji  wa miradi ya uzalishaji wa umeme  kwa kipindi cha 2010-2018. Kati ya hizo dola za Marekani, takribani, milioni 725 zitahitajika kutolewa na Serikali kama mchango wake katika kugharamia  uwekezaji  wa  miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kipindi cha 2010-2018; na

(b)    Dola za Marekani, takribani milioni 946  zitahitajika kugharamia uwekezaji katika upanuzi na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme kwa kipindi cha 2010-2018.  Kati ya hizo dola za Marekani, takriban milioni 142 zitahitajika kutolewa na Serikali  kama mchango wake katika kugharamia  uwekezaji  katika upanuzi na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme kwa kipindi cha mwaka 2010-2018.
21.  Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa miradi ya kipaumbele yataiwezesha nchi:
(a)     Kupata uwezo wa kuzalisha nishati ya umeme yenye viwango bora  inayokidhi mahitaji ya nchi;
(b)     Kuwa na mfumo wa umeme wenye umeme wa akiba   (reserve margin);
(c)      Kupunguza utegemezi wa uzalishaji wa umeme unaotokana na vyanzo vya nguvu za maji (optimized hydro-thermal mix);
(d)     Kuweka mazingira mazuri ya kushiriki kwenye biashara ya umeme  katika nchi za jirani na za kanda kupitia Taasisi za   Southern African Power Pool (SAPP) na  Eastern African Power Pool (EAPP);
(e)     Kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini kwa  kutekeleza kwa ufanisi mikakati na mipango ya maendeleo ya Serikali; na
(f)      Kuleta utengamavu na imani kwa wawekezaji katika sekta za  kiuchumi na kijamii.


       
          HITIMISHO
22.    Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu yanategemea kuwepo kwa huduma ya umeme iliyo bora. Juhudi za makusudi zilizoanza kuchukuliwa toka mwaka 2006 zinalenga:-
(a)      kuhakikisha kupanuliwa kwa wigo wa vyanzo vya kuzalisha umeme ili kuondoa utegemezi; kwenye umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji;
(b)      kukwepa mgawo wa umeme wa mara kwa mara;
(c)       kuboresha hali ya kifedha ya TANESCO;
(d)      utekelezaji wa marekebisho katika sekta ya umeme (Power Sector Reforms); na
(e)      utekelezaji wa Mpango kabambe wa sekta ya umeme 2009 – 2033.
23.    Mheshimiwa Spika, mipango ya kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme ipo, ila fedha nyingi zinahitajika. Miradi hii inawezeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali yetu, sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo.   
24.    Mheshimiwa Spika, ili mipango niliyoifafanua hapo juu itekelezwe kikamilifu na kwa wakati, ni lazima fedha zote zipatikane kwa wakati. Miradi yote mikubwa huchukua muda mrefu kuanzia ununuzi wa vifaa, makandarasi na washauri mbali mbali. Kwa uzoefu tuliopata inatulazimu tuchukue tahadhari kubwa ili kuepuka matukio kama yaliyotokea kwenye baadhi ya miradi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.





15 Februari, 2011