Meneja Kodi na Uzingatiaji Kanuni (Tax and Compliance
Manager) TANESCO Makao Makuu Bw. Sepetu Nyembo, amechaguliwa kuwa Mfanyakazi
Bora TANESCO kwa mwaka 2019 ambapo amepata zawadi ya fedha na cheti.
Bw. Nyembo ametangazwa kuwa mfanyakazi bora katika
maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo yamefanyika
kitaifa kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Sokoine jijini Mbeya na kuwa miongoni
mwa wafanyakazi hodari waliopongezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwakabidhi vyeti.
Sherehe za mwaka huu kitaifa zimefanyika jijini humo ambapo
inakadiriwa kiasi cha Wafanyakazi 6000 walishiriki kwenye sherehe hizo.
Wafanyakazi walipita kwa maandamano mbele ya
Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mhe.
Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa juu wa Serikali.
Aidha, Mheshimiwa Rais na viongozi hao wa juu wa Serikali
walipata fursa ya kuona misafara ya magari ya Taasisi mbalimbali za Umma na
Binafsi yakionesha shughuli mbalimbali wanazofanya.
Sherehe za Mei Mosi, hutumika kama siku ya kukumbushana,
kutafakari, kutathmini lakini pia kuzingatia wajibu kati ya wafanyakazi,
waajiri na serikali ili kuleta matokeo chanya katika ujenzi wa taifa.