Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA) kutumia Wazawa wanapokuwa wakitekeleza miradi hiyo.
Dkt. Kalemani aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Rugunga , Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma.
Aliongeza, Wananchi wanauwezo wa kufanya kazi katika Miradi ya REA kwani kuna kazi ambazo hazihitaji ujuzi wowote, akitolea mfano kazi za kubeba Nguzo.
“Mkandarasi usije hapa na vibarua, vibarua wanapatikana hapa hapa, kunavijana wengi na wanawezaa kufanya kazi, chukua vijana hapa, uwalipe ujira wao, na kazi ifanyike haraka bila kupoteza muda “, alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, ameiagiza TANESCO kuanzisha Ofisi Vijijini ili kuepusha usumbufu kwa Wananchi kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kilipia huduma ya umeme.
“TANESCO anzisheni Ofisi ndogondogo hapa kijijini, iwe ni chumba cha shule , iwe ni chini
ya mti, vyovyote vile lakini Wananchi walipie huduma ya umeme hapahapa Vijijini “, alisema Dkt.Kalemani.
Katika ziara yake, Dkt. Kalemani aliwasisitiza Wananchi kuchangamkia fursa ya umeme, na kwa kulipia kiasi cha shilingi elfu 27.
Aidha, alisisitiza kuwa umeme utafika kitongoji kwa kitongoji, nyumba kwa nyumba na Kaya kwa kaya, ili kuhakikisha Wananchi wote wa Rugunga, Vitongoji vyake 10 na vijiji vyote 37 vya Wilayani Kibondo vinapata hadi kufikia mwezi June 2019 vinapata huduma ya umeme.