September 25, 2020

"UMEME SASA NI KITONGOJI KWA KITONGOJI" DKT. KALEMANI

 


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini fungu la pili A katika Kijiji cha Bukene, Wilayani Nzega Mkoani Tabora, amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 190.7 kufikisha Umeme kitongoji kwa kitongoji katika vitongoji 1,103 vya Mikoa 9.

Waziri Kalemani aliitaji Mikoa hiyo ambayo vitongoji vyake vitanufaika moja kwa moja na mradi huo kwa sasa kuwa ni, Mikoa ya Dodoma, Tabora, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Mbeya pamoja na Tanga.

“Uzinduzi huu wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la pili A ni muendelezo wa usambazaji Umeme kwa Wananchi wote. Kazi hii bado inaendelea, ndani ya miaka miwili toka sasa, tutakuwa tumevifikia Vijijini vyote takriban 12,304 na Vitongoji vyake vyote 64,839 Nchini” Alisema Dkt. Kalemani

Waziri Kalemani aliendelea kwa kuwataka Watanzania ambao hawajafikiwa na huduma ya Umeme kuwa watulivu kwani lengo na mipango ya Serikali ni kuwafikishia Wananchi wote umeme ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo ndani ya kipindi cha miaka miwili toka sasa.

“Tumepeleka umeme kijiji kwa Kijiji na sasa tunakaribia kumaliza vijiji vyote Nchini, sasa tunakwenda kitongoji kwa kitongoji, kaya kwa kaya mpaka tutakapowafikia Wananchi wote” Alieleza Dkt. Kalemani

Kwa upande wa Wananchi wa Bukene, waliohudhuria katika uzinduzi huo walionesha kufurahishwa na kufarijika sana na mradi huo wa ujazilizi kuanzia na kuzinduliwa kitaifa katika kijiji na vitongoji vyao vya kijiji cha Bukene Migombani.

Naye Mwandu Igusule, mkazi wa eneo la Bukene, alisema kuwa wanatarajia kuutumia umeme huo kwa maendeleo yao ya kijamii pamoja na kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali zinazotegemea Nishati ya Umeme.

 






September 18, 2020

GEITA YAANZA KUNUFAIKA NA KITUO KIPYA CHA UMEM

 


 Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani yameanza kunufaika na Mradi mkubwa wa Umeme wa Geita-Bulyanhulu baada ya kukamilika rasmi kwa mradi huo wenye laini ya kusafirisha Umeme mkubwa katika msongo wa Kilovolti 220 sambamba na Vituo viwili vya kupoza na kusambaza Umeme.

Akifanya ziara na kushuhudia uwashwaji Umeme kwa mara ya kwanza katika mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, amesema kuwa, kwa muda mrefu Mkoa wa Geita ulikuwa na umeme usio tosheleza mahitaji.

“Hali iliyopelekea Serikali  kufanya jitihada za kujenga mradi huu Mkubwa ulio gharimu zaidi ya shilingi Bilioni 50 ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na gharama nafuu” alisema Mhandisi Gabriel.

Aliongeza kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Geita hivi sasa kumewezesha Mkoa wa Geita kuwa na umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji katika sekta mbali mbali hususan  uchimbaji wa Madini na Viwanda.

Mhandisi Gabriel aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Geita baada ya ujio wa Umeme wa uhakika na gharama nafuu wa TANESCO.

“Hali sasa ni shwari , umeme upo wa kutosha na wa uhakika. kukamilika  kwa ujenzi wa kituo cha Geita kumewezesha mkoa kuwa na zaidi ya Megawati 85 wakati matumizi ya sasa ya  ni Megawati 16  pekee” aliongeza Mhandisi Gabriel.

Aidha, Mhandisi Gabriel amewaasa wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani ambapo  miundombinu ya umeme imepita kuilinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho. 

Mhandisi Gabriel pia ametoa onyo kuhusu tabia ya wananchi kuchoma moto mashamba kiholela, hali inayohatarisha miundombinu ya umeme. 

Aliongeza kuwa kwa mwananchi yoyote atakaye bainika kufanya uharibifu huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wote wenye nia za namna hiyo.

Kwa upande wa TANESCO, Mhandisi Emanuel Manirabona ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Miradi -TANESCO  amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme ni miongoni mwa miradi mikubwa ya umeme inayojengwa katika Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi Kaskazini mwa Nchi.

Mhandisi Manirabona ameitaja miradi hiyo kuwa ni  njia ya umeme ya Geita-Nyakanazi yenye uwezo wa Kilovolti 220,  utakao gharimu zaidi ya shilingi Bilioni 100 pamoja na ule wa Kigoma hadi Nyakanazi msongo wa Kilovolti 400.

“yote hii ni kuhakikisha kuwa maeneo ya Uwekezaji katika Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi Kaskazini mwa Nchi yanapata umeme wa uhakika na wakutosha” Alisema Mhandisi Manirabona.

Manirabona aliongeza kuwa, kuungwa kwa njia ya kusafirisha umeme ya Bulyanhulu-Geita, kunawezesha wananchi wa mkoa wa Geita na Maeneo ya jirani na Migodi ya Bulyanhulu pamoja na Geita kuwa na umeme wa uhakika.