September 9, 2019

WAZIRI DKT. KALEMANI ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI MRADI WA UMEME WA MAJI WA JULIUS NYERERE (JNHPP) WA MTO RUFIJI


 
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akitoa tathmini yake mbele ya sehemu ya kuingilia kwenye handaki la kuchepusha maji (diversion tunnel) la ujenzi wa mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere kwenye mto Rufiji Mkoani Pwani Septemba 8, 2019 wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao ukikamilika utazalisha umeme wa Megawati 2115.


Kasi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji Mkoani Pwani “imemkuna” Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani baada ya kutembelea eneo la mradi huo Septemba 8, 2019 na kukuta hatua muhimu ya ujenzi wa ADIT (njia ya kufika kwenye handaki la kuchepusha maji) (diversion tunnel) ikiwa imekamilika.

“Hii ni mara yangu ya nane kutembeela mradi huu tangu uanze, leo nimetembelea ili kuangalia masuala makubwa matatu, kasi ya ujenzi, usimamizi na utawala na masuala yote ya ujenzi wa miundombinu wezeshi ili kuona kama imekaa sawasawa.” Alisema Dkt. Kalemani.

Alisema baada ya kuangalia masuala hayo amefurahishwa na hatua iliyofikiwa ambapo amewapongeza wasimamizi wa mradi huo TANESCO na TANROADS ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo kuwa lazima ujenzi huo usimamiwe na Watanzania wenyewe na ukamilike katika muda uliopangwa ambao ni miezi 42, ambapo miezi 36 ni ya ujenzi na miezi 6 ya mobilization kwa maana ya maandalizi ya vifaa na watumishi ambapo kazi ilianza Juni 15, 2019 na kazi inakwenda vizuri.” Alifafanmua Dkt. Kalemani.

Akifafanua zaidi Dkt. Kalemani alisema hadi sasa tayari wakandarasi wamekwishatumia miezi nane 8 kati ya 42 na kazi ambazpo zilikuwa zinaendelea kufanyika ni ujenzi wa njia za kuchepusha maji (diversion tunnel), nilikuja Julai 22, 2019 na nikaelekeza kazi hii ifanyike ndani ya siku 45 na ikamilike umbali wa Mita147.6 nashukuru wamemaliza na wameokoa siku 7 kabla ya muda niliotoa.

“Nimatarajio yetu mkataba unaisha Juni 14, 2022 na nimatumaini yetu kwamba watatukabidhi mradi huo siku hiyo saa 9;30 alasiri wataukab idhi na mimi niukabidhi kwa Watanzania na asitokee mtu atakaejaribu kuuchelkewesha mradi huo, sisi kama serikali tutahakikisha tunaanza kumchelewesha yeye kwanza kabla hajatuchelewesha sisi kukamilisha mradi huo.” Alionya.
Awali akitoa taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo yaliyofikiwa hadi sasa, Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Steven Manda ambaye pia ni Meneja Miradi wa TANESCO alisema, pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa handaki la kuchepusha maji, pia daraja namba mbili kwa maana ya miundombinu wezeshi nalo limekamilika na sasa mashine kubwa na vifaa vya ujenzi vinavushwa kutoka upande mmoja wa mto kwenda upande wa pili kupitia daraja hilo.

Daraja namba mbili  la kukatisha mto Rufiji eneo la ujenzi wa mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) likiwa limekamilika.