January 31, 2022

MAHARAGE AWATOA HOFU WATANZANIA KUHUSU UPATIKANAJI WA UMEME KATIKA KIPINDI CHA MATENGENEZO YA VISIMA VYA GESI ASILIA


Shirika la umeme Tanzania TANESCO limewatoa hofu wateja wake kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini wakati wa uboreshaji wa mfumo wa gesi asilia kwenye visima vya gesi vya TPDC(Tanzania Petroleum Development Company) na PAET(Pan African Energy Tanzania) kama yalivyotangazwa kuanza tarehe 1 hadi 10 mwezi huu.


Akifafanua kuhusu matengenezo hayo leo Januari 30,2022 wakati wa ziara aliyoifanya na waandishi wa habari kwenye kituo cha kupoza umeme cha kunduchi jijini Dar es salaam Maharage amesema nchi haitakua gizani na kwamba hakuna maeneo yatakayoathirika kwa siku zote kumi mfululizo kwa kukosa umeme.

‘‘Visima vile vya gesi asilia si vya TANESCO ni vya TPDC, SONGAS na PAET sisi ni wateja tunaochukua gesi kutoka kwao na ili wao watupatie nishati hiyo zaidi ni lazima kufanya maboresho ndani ya siku hizo 10 tulizozitangaza, hakuna eneo litaathirika zaidi ya siku 3 kwa kukosa umeme ndani ya siku hizo kumi za kupisha matengenezo na tayari tumeshatoa ratiba kwa maeneo yote yatakayoathirika kwa kila mikoa husika nchi nzima.’’amefafanua Maharage.

Aidha amesema sambamba na matengenezo ya visima hivyo Shirika litaendelea na maboresho yake na matengenezo mbalimbali  kwenye miundombinu yake ndani ya  muda wa siku 10 katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha matengenezo yatakapokamilika huduma ya umeme inarejea katika hali yake ya kawaida.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema kazi ya kuongeza uwezo wa kupokea na kupoza umeme katika kituo  cha kunduchi kilichoko eneo la Salasala jijini Dar es salaam iko ukingoni na tayari transforma mpya yenye ukubwa wa MVA 195 imekamilika kufungwa.

‘‘Transforma hii inategemewa kuwashwa ili kuanza kutumika wakati wa kipindi cha matengenezo ya visima vya gesi na umeme kama nilivyozungumza wiki ya jana’’ amesema Maharage.

Akieleza kwa undani faida za transforma hiyo kwa wateja wanaohudumiwa na kituo hicho Meneja mkoa wa Kinondoni kaskazini Mhandisi Regina Mvungi amesema  transforma hiyo itasaidia kuondoa matatizo ya umeme kucheza, kuwa mdogo na kuboresha hali ya upatikanaji umeme kuwa ya kutabirika na ya uhakika.

Vilevile faida zingine ni itasaidia wateja kutokosa huduma pindi transforma moja itakapopata hitilafu tofauti na hali ilivyokua hapo awali na kuwezesha mikoa mingine ya Kitanesco kama Kinondoni kusini kuwapa wateja huduma wanapokuwa na matengenezo  mbalimbali ya umeme.

Kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha kunduchi kilianzishwa mwaka 1995 ambapo kutokana na ongezeko la mji kukua kwa kasi na uhitaji wa umeme lilazimu TANESCO kununua transforma mpya kubwa itakayosaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.

January 28, 2022

TANESCO KUFANYA MABORESHO KWENYE VITUO VYAKE VYA UZALISHAJI UMEME VYA KINYEREZI I NA UBUNGO III


Katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa umeme nchini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linaendelea na maboresho kwenye vituo vyake vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I itakayozalisha megawati 185 na Ubungo III megawati 112.


Akizungumza na wanahabari leo Januari 28, 2022 Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo, Maharage Chande amesema mpaka sasa uzalishaji kutoka mitambo ya Ubungo III umefikia Megawati 60 ambazo tayari zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Amesema kwa sasa kazi ya kupanua kituo cha Kinyerezi I inaendelea na megawati 70 za awali zitaingia kwenye mfumo wa gridi mwezi Aprili 2022 na ifikapo mwezi Agosti 2022 kazi hiyo itakuwa imekamilika na kupelekea Kituo cha Kinyerezi I ambacho sasa kinazalisha megawati 150 kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 335.

‘‘Mitambo hii inayoongezwa ili iweze kuzalisha umeme, inapelekea mahitaji ya gesi asilia kuongezeka ambapo inalazimu kufanya uboreshaji wa mfumo wa gesi kwenye mifumo ya TPDC (Tanzania Petroleum Development Company) na PAET (Pan African Energy Tanzania)’’ amesema Maharage.

Aliongeza kuwa zoezi la uboreshaji litafanyika kwenye visima vya gesi vilivyopo Songosongo kuanzia tarehe 01 hadi 10 Februari 2022, ambapo kukamilika kwake kutahakikisha gesi  ya ziada inayohitajika inapatikana.

Hivyo utekelezaji wa maboresho hayo utapelekea mapungufu ya gesi kwenye mitambo ya kuzalishia umeme wa gesi asilia na kulazimika kuzimwa kwa baadhi ya mitambo ili kupisha zoezi hilo muhimu.

Sambamba na matengenezo hayo, hali hiyo itasababisha upungufu wa uzalishaji umeme na kuathiri baadhi ya maeneo, amesema wananchi watapata taarifa za makatizo ya umeme kama zitakavyotolewa na mikoa husika.

Maboresho hayo kwenye vituo vya vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I na Ubungo III yatasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza malalamiko ya wateja ya kutokuwa na umeme wa uhakika na unaotabirika.



January 15, 2022

TANESCO KUENDELEA KUUNGANISHA UMEME KWA GHARAMA YA ELFU 27,000 MAENEO YA VIJIJINI

 

                             Meneja Mwandamizi Kanda ya Kati, Mhandisi Frank Chambua

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahakikishia wananchi wa maeneo ya vijijini kuendelea kupata huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi elfu 27.


Hayo yamesemwa na Meneja Mwandamizi Kanda ya Kati, Mhandisi Frank Chambua leo Januari 15, 2022 katika Kijiji cha Kigwe Mkoani Dodoma, alipokuwa katika ziara ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa eneo hilo kuunganisha huduma ya umeme.

"Tumekuja hapa kuwahakikishia wananchi wa vijijini tunaendelea kuwaunganisha kwa bei ya shilingi elfu 27 kupitia miradi inayotekelezwa na TANESCO" amesema Mhandisi Chambua.

Alifafanua kuwa,Serikali  imefadhili miradi ya umeme kwenye maeneo ya vijijini hivyo wananchi wanatakiwa kulipia elfu 27 ambayo inajumuisha kodi ya ongezeko la thamani yaani (VAT).

Mkutano huo pia ulienda sambamba na elimu kwa wateja iliyohusu kuelimisha uma taratibu sahihi zinazotakiwa kufuatwa kwenye kupata huduma ya umeme.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kusaidia kulinda miundombinu ya umeme hasa kipindi wanapoandaa mashamba na kuacha kuchoma nguzo moto.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Bahi, Hassan A. Hassan amesema wanaendelea kuwaunganisha wateja wote wa maeneo ya vijijini kwa shilingi elfu 27.

"Tunaendelea kuwaunganishia wateja kwa elfu 27, leo tuna idadi ya wateja 16 ambao tutawaunganishia umeme, lakini pia tunahamasisha wananchi kuzidi kuomba kupata huduma ya umeme" amesema Hassan.

Kwa Mkoa wa Dodoma Serikali imewekeza jumla ya shilingi bilioni 195.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuunganisha umeme. Mkoa huo una jumla ya vijiji 581 ambapo mpaka sasa takribani vijiji 422 vimefikiwa na huduma ya  umeme na vilivyobaki ni 159 ambavyo wakandarasi wanaendelea na kazi ya kuunganisha huduma hiyo.