August 28, 2018

TANESCO YAZALISHA UMEME WA KUTOSHA


Imebainishwa kuwa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO) kwa sasa linazalisha umeme wa kutosha mahitaji ya nchi huku ziada ikiwa ni zaidi ya megawati 200 na hivyo kupelekea kupungua kwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi  Mtendaji wa TANESCO,  Dkt. Tito Mwinuka,  leo tarehe 28/08/2018 wakati akiwasilisha Taarifa ya Shirika hilo kwa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Ameeleza kuwa, umeme unaozalishwa sasa ni takribani megawati 1517.47 huku matumizi yakiwa ni takribani ni megawati 900.

Aidha, Dkt. Mwinuka ameeleza kuwa Shirika hilo linaendelea na juhudi za kuwaunganishia umeme wananchi, kazi ambayo inaenda  sambamba na kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza  matukio ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Ameeleza kuwa, kutokana na jitihada hizo, mapato ya Shirika yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kuliwezesha Shirika kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini tangu mwaka 2015/16.

“Mapato ya Shirika yameendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18, makusanyo yamekuwa ya wastani wa  shilingi bilioni 38 hadi 39 kwa Wiki kutoka wastani wa shilingi bilioni  34 katika mwezi Aprili, 2018,” amesema Dkt. Tito Mwinuka.

Akizungumzia suala la deni la TANESCO, Dkt. Mwinuka amesema kuwa  kuna sababu mbalimbali zinazopelekea deni la Shirika kuongezeka ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uzalishaji wa umeme katika maeneo yaliyopo mbali na gridi ya Taifa ambapo TANESCO hulazimika kuzalisha umeme kwa wastani wa shilingi 763 kwa uniti moja.

Akizungumzia mikakati ya Shirika katika kulipa madeni kwa wadai wake, Dkt.  Mwinuka alisema kuwa wameweka mipango mahsusi ili kulipa gharama hizo kila mwezi ili deni lisiendelee kukua, kuwalipa deni lote wadai wadogowadogo kwa wakati na kujadiliana na wadai ili kuondoa riba.

Aliongeza kuwa,  juhudi nyingine zinazofanywa na TANESCO ili kupunguza madeni kwa Shirika ni  kutafuta mikopo yenye masharti nafuu,  kuongeza na mapato.


August 17, 2018

Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari kutangaza operesheni maalum ya wahalifu wa miundombinu ya umeme na maji.


Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari kutangaza operesheni maalum ya wahalifu wa miundombinu ya umeme na maji.
Dar es salaam.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limezindua operesheni itakayowezesha kutokomeza wanaohujumu miundombinu ya maji na umeme.

Operesheni hiyo imezinduliwa leo Agosti 17, 2018 na Kamanda wa polisi Kanda Maalum Lazaro Mambosasa alipokutana na wadau kutoka shirika la umeme (TANESCO) pamoja na shirika la maji safi (DAWASCO)

Kamanda Mambosasa amesema siku zahivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaojiunganishia miundombinu hiyo bila kufuata utaratibu na kuzisababishia hasara kampuni hizo

Kaimu Meneja uhusiano wa Tanesco Leila Muhaji amesema watashirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha wote wanaohujumu miundombinu hiyo wanakamatwa.

 “Tutashirikiana na jeshi la polisi Kanda maalum kuhakikisha wote wanaohujumun miundombinu hii tunawakamata kwakuwa wamekuwa wakiliingizia shirika hasara hasa wanapoiba mafuta kwenye transfoma kwaajili ya kupikia”amesema Muhaji.

Ameongeza kuwa kwa sasa umeme unapatikana kwa urahisi kwenye maeneo yote na shirika linaende kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo haujafika.

August 16, 2018

Waziri kalemani awasha rasmi umeme katika Mahakama ya mwanzo ya Somanda

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalema akikata utepe.

Mahakama ya mwanzo ya Somanda
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasha rasmi umeme katika Mahakama ya Mwanzo ya Somanda Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA 111).

Waziri Kalemani amefanya uzinduzi huo jana, Agosti 15, 2018 katika eneo la Mahakama ya Mwanzo ya Somanda mkoani Simiyu akiwa katika ziara yake katika Kanda ya Ziwa.

Waziri Kalemani alieleza kuwa ni faraja kwake kuona taasisi za umma zikiwemo Mahakama zikipata umeme.

“Mahakama nyingi zilikuwa hazina umeme, na hii ni mojawapo ya changamoto ambayo inapekea kesi nyingi mahakama kuchelewa, hivyo Mahakama ya Somanda mtaharakisha kutoa hukumu ya kesi ili kutenda haki kwa wananchi” alisema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani alisema kuwa, kipaumbele cha Serikali ni kupeleka nishati ya umeme katika Taasisi zote za umeme ili kuwafikia wananchi wengi kwa wakati moja.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kalemani alisema kuwa sasa mahakama ya Somanda watafanya kazi zao muda wowote na pia wanaweza kuweka vinasa sauti ili kupata ushahidi wa uhakika kutoka kwa mashahidi wao.

Aidha, Waziri Kalemani alikumbusha Mahakama hiyo kulipia bili zao za umeme kwa wakati ili kuepuka kukatiwa umeme na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Pia, Waziri Kalemani aliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweka Transforma moja katika mahakama hiyo special kwao wao wenyewe ili kuepuka usumbufu wowote utakaojitokeza kama vile kukatika kwa umeme.

“Wekeni Transfoma ya Mahakama hii wao peke yake ili ikitokea umeme umekatika maeneo mengine wao wasipate usumbufu ili wafanye kazi yao kwa ufanisi,”alisema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani pia, alikabizi vifaa cha Umeme Tayari (UMETA) 20 kwa Mahakama hiyo lengo likiwa ni kuhamasisha matumizi ya vifaa hivyo vya UMETA katika Taasisi za umma ambavyo havihitaji gharama kubwa kuviunganisha na vinawasha vyuma viwili hadi vinne.


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa tatu kulia) akishangilia mara baada ya kukata utepe ikiwa ni ishara ya kuwasha rasmi umeme katika Mahakama hiyo. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mktaka na wa tano kulia ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo David Peter.


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja mara bada ya kuwasha umeme rasmi katika Mahaka ya Mwanzo ya Somanda wilayani Bariadi. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Serekalini.



August 2, 2018

Rufiji Hydropower Project MW 2100 kuendesha treni ya umeme

Wazi Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akifungua kikao hicho, kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ma kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba 

MOROGORO 

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema kuwa umeme utakaozalishwa kwenye mradi wa Rufiji Hydropower Project  (Strigler’s Gorge)ndio utakaotumika katika uendeshaji wa treni ya kisasa ya umeme.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa Serikali itakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo kwa wakati ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hayo aliyasema jana mjini Morogoro, alipokuwa akifungua kikao cha mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na wataalamu mbalimbali zikiwamo Wizara 11 ambao wanatekeleza mradi huo.

Alisema mradi huo pindi utakapokamilika unatarajiwa kuzaliwa megawati 2,100 pindi utakapokamilika mwaka 2010.

 “Hivyo tumekutana hapa kujadili taarifa ya wataalamu kuhusu mradi, kutafakari changamoto na kuzifanyia kazi pamoja na kutembelea eneo la mradi.

“Hivi pamoja na hali hiyo kutakuwa na kazi ya kujenga transmi,” alisema Dk. Kalemani.
Kutokana na umuhimu mkubwa wa mradi huo kwa Taifa, Dk. Kalemani, alisema Serikali itachukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekwamisha uwetekelezaji wa mradi huo ambao utekelezaji wake unahusisha wizara 11 huku ukisimamiwa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Waziri huyo wa Nishati, alisema tangu ilipoasisiwa azma ya utekelezaji wa mradi huo na Rais Dk. John Magufuli, Julai mwaka jana Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wizara nyingine walianza usimamizi wa haraka wa utekelezaji wake.
“Mradi huu utazalisha Megawati 2,100 ulibuniwa miaka mingi lakini ulichelewa kutekelezwa. Julai mwaka uliopita (2017) Rais Dk. John Magufuli aliweka wazi azma ya utekelezaji wa mradi huu.

“Waheshimiwa mawaziri na wajumbe mradi wa Mto Rufiji unaweza kuusema ni mradi rahisi sana kama miradi mingine lakini kwa historia ya uzalishaji wa umeme kwa nchi yetu huu utakuwa mradi mkubwa sana.

“Mradi mkubwa tuliona kwa sasa wenye megawati nyingi 240, ambao ni Kinyerezi namba mbili na katika miradi ya miradi ya maji ni wa megawati 204 kwa hiyo kuna kila namna ya kuongeza juhudi za kuukamilisha mradi huu. Nichukue nafasi hii kwa heshima kubwa kuipongeza Serikali hasa kupitia kwa Mheshimiwa Rais kwa kuamua kuutekeleza mradi huu nasi kama wasimamizi na watekelezaji wake tutatumia kila namna kila nguvu na akili tuliyonayo kuutekeleza kwa dhati mradi huu hadi ukamilike.

“Hatutasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote mwenye nia ama ya kuuchelewesha ama kuukwamisha hatutasita kuchukua hatua za kisheria sisi tunaomba mradi huu ndio mkombozi pekee. Kama Serikali tumedhamiria kuutekeleza mradi huu na tumejipanga vizuri,” alisema
Alisema jambo la kwanza linalohitajika ni spidi ya utekelezaji kwa wataalamu na usahihi wa utekeleza wake pamoja na uweledi kwenye mradi huo.

Waziri huyo wa Nishati alisema
Alisema kwa sasa Serikali inaendelea kumtafuta mkandarasi ambaye atatekeleza mradi huo pamoja na msimamizi wa mkandarasi ambaye sharti apatikane kabla mkandaasi hajapatikana.

“Tunaendelea kutekeleza miradi ya kujenga miradi ya kujenga usafirishaji wa umeme huo (trasmision line)  ya kuutoa umeme huo Rufiji na kuupeleka hadi Chalinze ambapo umeme huu pia unautarajia sana utumike kuendesha treni mpya ya Standard Gauge inayoanza kutumika mara baada ya mradi kukamilika.

“Kwa hiyo huu ni mradi muhimu kwetu sisi Serikali maandalizi yanakwenda sawa ikiwamo kuanza kuona kuona kuanzia sasa namna ya utekelezaji wake,” alisema Dk. Kalemani

Kama mtakumbuka Bonde la Rufiji lilikuwa chini ya usimamizi wa RUBADA, lakini kwa kuwa wao walikuwa wakisimamia walishindwa kuutekeleza kutokana na kuwa wao si kazi yao kujenga umeme kwani lilikuwa jukumu la Tanesco.

“Mwaka jana tulipoanza mradi kuliwapo na changamoto za kawaida ikiwamo kujenga uelewa wa mradi huu. Hivyo ninapenda kusema kwamba taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea na kufikia Septemba mwaka huu atakuwa amepatikana. Kazi yetu sisi ni kuweka mazingira wezeshi kwa mkandarasi ili awezwe kuutekeleza mradi huu kwa wakati,” alisema Dk. Kalemani
Alisema lengo la mkutano huo utaangalia masuala matatu ambayo ni kupata taarifa ya utekelezaji na hatua za kuchukua, kutafakari changamoto za mradi na kutembelea eneo la mradi ili kuona hali halisi.

Dk. Kalemani, alisema ni vema kila mtaalamu kwa nafasi hasa waliohudhuria kwenye mkutano huo kutafakari kwa kina na hatua za kuchukua ili kuhakikisha utekelezaji unakamilika kwa wakati.
Alisema kwa sasa nchi ina Megawati 1582 baada ya kuongezewa uwezo wa mtambo wa umeme wa Kinyerezi II na mwishoni mwakani zitaingizwa megawati 185 kupitia mtambo wa Kinyerezi I.

“Lengo ni kufikisha megawati 500 hadi kufikia mwaka 2020 na ifikapo mwaka 2025 kuwa na megawati 10,000. Mradi huu tunaweza kusema ni rahisi lakini pia ni wa kihistoria na ndiyo mradi mkubwa kwetu. Na tutaukamilisha kama ulivyopangwa na serikali.

“kupitia mkutano huu utapata taarifa na mazingira wezeshi kwa kila mdau ili kuweza kuona wapi kuna changamoto na namna ya kuchukua ili twende haraka,” alisema

Waziri huyo wa Nishati, alisema kuwa kikao hicho cha mawaziri ni cha pili kufanyika ambapo cha kwanza kilifanyika Aprili mwaka huu.


Mkutano huu umehudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba pamoja na makatibu wakuu wa Wizara Malisili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Muungano na Mazingira, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.