August 19, 2021
August 18, 2021
Hatua nyingine kubwa JNHPP
Kazi ya usimikaji wa bomba (Draft tube) sehemu ya chini kabisa kwenye
mashine nambari 9 imeanza Agosti 17, 2021, katika mradi wa kufua umeme
wa Julius Nyerere (JNHPP), bomba hizo zitatumika kutolea maji katika
mitambo ya kufua umeme na kuyarudisha mto Rufiji kwa ajili ya matumizi
mengine.
Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa baada ya kukamilika kwa uundwaji wa bomba
hizi zinazofungwa katika kitako cha msingi wa zege, kilichopo eneo la
mita 42.7 juu ya usawa wa bahari.
Usimikaji wa bomba hizi ndio utawezesha kuanza kwa ufungaji wa sehemu za
juu za mashine (turbine) na kisha jenereta za kufua umeme.
August 14, 2021
WAZIRI MKUU AKAGUA KITUO CHA TANESCO MSAMVU BAADA YA KUATHIRIKA NA MOTO
Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa,
leo Agosti 14, 2021 amekagua kituo cha kupokea na kupoza umeme cha
Msamvu mkoani Morogoro.
Mhe. Majaliwa amekagua athari zilizotokea baada ya kupata hitilafu
iliyopelekea kuwaka moto kwa jumba la kudhibiti mifumo ya umeme wa
msongo wa kilovolti 33 Agost 2, 2021.
Aidha, amewataka Wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kufanya kazi kwa
uaminifu na weledi kutokana na nishati ya umeme kuwa ndio injini ya
ukuaji uchumi wa Nchi.
" Watumishi wa TANESCO mmebeba mioyo ya watu, muongeze umakini katika utendaji wenu wa kazi", amesema Mhe. Majaliwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameiagiza TANESCO Kufanya mapitio ya
Wafanyakazi wanaosimamia vituo vya kupokea na kupoza umeme ili
kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi.
Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro ni moja
kati ya vituo 51 ambavyo vinapokea na kupoza umeme mkubwa wa gridi ya
Taifa.
August 11, 2021
NAIBU KATIBU MKUU AKAGUA MRADI YA UMEME LUGURUNI
Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali, Agosti 07, 2021 alikagua
utekelezaji wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Luguruni
Jijini Dar es Salaam.
Utekelezaji wa mradi wa Luguruni ulianza Aprili 01, 2020 na unatarajiwa
kukamilika Septemba 30, 2021 ikiwa ni miezi 18 ya utekelezaji wa mradi.
Kukamilika kwa mradi wa Luguruni kutaboresha hali ya upatikanaji wa
umeme katika Mikoa wa Pwani na Dar es salaam hasa kwa maeneo ya Kimara,
Mbezi, Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, msigani, kibamba, kibwegere,
kisarawe, Maili moja na TAMCO (Industrial area) ambayo yamekuwa na
changamoto ya kukosekana kwa umeme wa uhakika kutokana na njia za umeme
zinanipeleka maeneo hayo kusafiri umbali mrefu.
Gharama za uzalishaji mradi wa Luguruni ni Shilingi Bilioni 15.2 ambazo
zinagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MANUFAA YA KITUO CHA UMEME DEGE KWA KIGAMBONI NA MAENEO YA JIRANI
Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Dege ni mkombozi katika kukuza
shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Wilaya ya Kigamboni na maeneo jirani
kutokana na kuimarisha upatikanaji wa umeme baada ya kukamilika kwa
utekelezaji wake Aprili 30, 2021.
Maeneo ya Viwandani, Pemba Mnazi, Mwasonga, Mwongozo, Kimbiji na maeneo
jirani awali yalikuwa yanapata changamoto ya umeme kukatika au kuwa
mdogo kutokana na njia ya umeme kusafiri umbali mrefu kutokea Mkoa wa
kitanesco wa Ilala.
Akitembelea kituo hicho Agosti 07, 2021 Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw.
Kheri Mahimbali ameridhishwa na usimamizi wa kituo cha Dege ambacho
kilianza kujengwa Mei 02, 2019.
Aidha, mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Kigamboni ni megawati 18 huku uwezo
wa kituo cha Dege ni megawati 48 lakini malengo ya Serikali ni
kukiongezea uwezo hadi hadi kufikia megawati 96.
August 10, 2021
TANESCO NA STAMICO WASAINI UTEKELEZAJI MRADI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Agosti 10, 2021, limesaini hati
ya makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhusu
utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia
makaa ya mawe ya Kiwira.
Akiongea wakati wa uwekaji saini Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito
Mwinuka amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira utaenda sambamba na
ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka ya urefu wa km 100 kutoka
Kiwira hadi kituo cha kupokea umeme cha Mwakibete Mbeya.
Aliongeza kuwa, kwasababu mradi unagusa Taasisi mbili ni vyema kuwa na hati ya makubaliano ili kufahamu jukumu la kila Taasisi.
"STAMICO na TANESCO ni wadau wa mradi wa Kiwira, kwa maana kwamba
STAMICO wao wanahusika na mgodi wa makaa ya mawe, TANESCO tutasimamia
ujenzi wa mtambo wa kufua umeme", alisema Dkt. Mwinuka.
Amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira umeambatana na faida nyingi kwa
Nchi ikiwemo uwepo umeme wa kutosha na kuweza kufanya biashara na Nchi
jirani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji STAMICO, Dkt. Venance Mwase amesema jukumu kubwa la STAMICO ni uchimbaji wa madini.
Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Taasisi za Serikali kushirikiana
katika miradi mbalimbali ya maendeleo na hata kutoa huduma.
"Siku hii ya leo tumefikia makubaliano na TANESCO katika kuuendeleza mradi wa Kiwira kwa manufaa ya Taifa ", alisema Dkt. Mwase.