Waziri Mkuu wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akipata maelezo namna ambavyo TANESCO inawatumia watalamu wa Jiolojia katika kutekeleza miradi mbalimbali. |
NA SAMIA CHANDE, DODOMA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amefungua kongamano la mwaka la Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania (Tanzania Geological Society - TGS) Jijini Dodoma.
Alisema, watalamu wa Giolojia ni muhimu katika kueleta maendeleo ya Viwanda kupitia Nishati mbalimbali za umeme kama vile kuzalisha kwa kutumia Jotoardhi.
"Jotoardhi ni chanzo kizuri cha nishati kwa hivyo niwapongeze TANESCO kupitia kampuni tanzu ya TGDC, Serikali inatarajia hivi karibuni muanze kuzalisha umeme kupitia Jotoardhi", alisema Mhe. Majaliwa.
TANESCO imeshiriki katika kongamano hilo kupitia Kampuni tanzu ya Uendelezaji wa Jotoardhi Nchini (TGDC). Aidha, Mhe. Majaliwa alitembelea banda la TANESCO na kupatiwa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa Sekta ya Jiolojia katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme.
Akimuelezea Mheshimiwa Waziri Mkuu umuhimu wa jioloji katika utekelezaji wa miradi ya umeme, Mhandisi Eliaza Wangwe kutoka Idara ya Utafiti TANESCO, alisema tasnia ya jioloji ni muhimu katika utekelezaji wa miradi ya umeme katika hatua zote kuanzia utafiti, ujenzi na usimamizi. Aliongezea, TANESCO kupitia Kampuni Tanzu TGDC inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuwezasha uzalisha umeme utokanao na rasilimali ya jotoardhi.
"Jotoardhi ni nishati jadidifu, nafuu na endelevu inayoweza kutumika katika kuzalisha umeme na matumizi mengine kama vile kilimo, ukaushaji wa mazao na ufugaji wa samaki", alisema Mhandisi Wangwe.
Kwa upande wake Meneja Mipango na Miradi kutoka TGDC Mhandisi Shakiru Kajugus, alisema Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya Megawati 5000 zitokanazo na jotoardhi.
“Nchi yetu ina zaidi ya maeneo 50 yenye viashiria vya Jotoardhi ambapo maeneo hayo mengi yanapatikana katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ambalo linapita hadi Kenya ambao tayari wanazalisha zaidi ya 700MW za Jotoardhi kwa sasa.” Mhandisi Kajugus.
TGDC inaendelea na tafiti katika maeneo mbalimbali nchini kama vile eneo la Ziwa Ngozi lililoko Mkoani Mbeya ambapo ndipo yalipo makutano ya bonde la ufa la upande wa mashariki na lile la magharibi. Utafiti huo katika hatua ya uchorongaji visima vya majaribio ili kuthibitisha uwepo na kiwango cha rasilimali ya jotoardhi iliyopo katika eneo hilo.
Katika kukuza uchumi wa viwanda joto ardhi itatumika katika miradi mbalimbali kama kilimo na viwandani.