UFAFANUZI JUU YA TAARIFA ZILIZOTOLEWA
NA BAADHI YA VYOMBO
VYA HABARI KUHUSU OMBI LA TANESCO
KUSHUSHA BEI YA UMEME
Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) limewasilisha ombi la kushusha bei ya umeme kwa
asilimia 1.1 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) pamoja na
kuondoa kabisa gharama ya maombi ya awali kwa wateja wapya (gharama za Fomu) ya
Shilingi 5,000 na gharama za huduma (service charge) ya Shilingi 5,520 kwa
mwezi kwa wateja wote wa majumbani.
Maombi
hayo yamewasilishwa baada ya TANESCO kufanya tathmini ya kina ya kimahesabu
pamoja na kubuni namna ambayo wateja wake wanaweza kupata ahueni ya gharama kwa
kuzingatia mazingira ya sasa.
Hata
hivyo baadhi ya vyombo vya habari vimepotosha ukweli huo hivyo TANESCO inapenda
kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mosi,
Kwa mujibu wa sheria, TANESCO inapotaka kubadilisha bei za umeme, iwe kushusha
au kupandisha ni lazima iwasilishe maombi hayo EWURA kwa kuwa ndiyo mwenye mamlaka
ya kisheria ya kubadilisha bei za umeme.
Pili,
TANESCO huwasilisha maombi yake pamoja na takwimu halisi zinazoshawishi mantiki
ya kubadilishwa kwa bei hizo na kwa maombi yaliyowasilishwa EWURA Februari 24,
2016 ndivyo TANESCO ilivyofanya.
Tatu,
Baadhi ya mambo muhimu yanayoendana na mazingira ya sasa ni pamoja na
kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa gesi tofauti na ilivyokuwa hapo kabla na
pia kuongezeka kwa ujazo wa maji katika mabwawa hasa Mtera.
Nne,
japokuwa kiasi cha madeni kilichotajwa na vyombo vya habari sio sahihi, madeni
hayo yamezingatiwa kikamilifu katika mapendekezo haya ya kushusha bei, hivyo si
kweli kwamba kwa kushusha huko bei TANESCO itafilisika.
Aidha,
kusema kwamba Serikali inailazimisha TANESCO kushusha bei ya umeme na kwamba
kwa kufanya hivyo Shirika litafilisika sio sahihi hata kidogo kwani tathmini ya
kitaalamu imefanyika na pia kwa mujibu wa sheria EWURA itafanya tathmini yake
kabla ya kuidhinisha bei mpya.
Ieleweke
kwamba Serikali ya awamu ya Tano imeshatoa fedha nyingi za kusaidia miradi ya
umeme zikiwepo zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zilizotolewa hivi karibuni kwa
maelekezo ya Mh. Rais kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Mradi mkubwa wa
Kinyerezi II unaotekelezwa na Kampuni ya SUMITOMO ya Japan.
Pia
Serikali imeendelea kulipa madeni ya umeme ya taasisi zake na hadi sasa sehemu
kubwa ya madeni ya taasisi za Serikali yamelipwa.
Hivyo,
TANESCO inaishukuru Serikali kwa jitihada kubwa inazozifanya katika
kushughulikia changamoto za umeme nchini.
Imetolewa
na: Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO Makao Makuu.
No comments:
Post a Comment