August 10, 2021

TANESCO NA STAMICO WASAINI UTEKELEZAJI MRADI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Agosti 10, 2021, limesaini hati ya makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhusu utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira.

Akiongea wakati wa uwekaji saini Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira utaenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka ya urefu wa km 100 kutoka Kiwira hadi kituo cha kupokea umeme cha Mwakibete Mbeya.

Aliongeza kuwa, kwasababu mradi unagusa Taasisi mbili ni vyema kuwa na hati ya makubaliano ili kufahamu jukumu la kila Taasisi.

"STAMICO na TANESCO ni wadau wa mradi wa Kiwira, kwa maana kwamba STAMICO wao wanahusika na mgodi wa makaa ya mawe, TANESCO tutasimamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme", alisema Dkt. Mwinuka.

Amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira umeambatana na faida nyingi kwa Nchi ikiwemo uwepo umeme wa kutosha na kuweza kufanya biashara na Nchi jirani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji STAMICO, Dkt. Venance Mwase amesema jukumu kubwa la STAMICO ni uchimbaji wa madini.

Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Taasisi za Serikali kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo na hata kutoa huduma.

"Siku hii ya leo tumefikia makubaliano na TANESCO katika kuuendeleza mradi wa Kiwira kwa manufaa ya Taifa ", alisema Dkt. Mwase.








No comments:

Post a Comment