COMESA- yaeleza ni mradi wa kimaendeleo Afrika
Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Nchi za
Zambia, Tanzania na Kenya zimesaini Mkataba
wa Makubaliano kuonesha dhamira ya Serikali
ya nchi hizo kujenga kwa pamoja miundombinu
ya ya kusafirisha umeme na kufanya biashara ya kuuziana umeme wa ziada baina ya
nchi hizo (ZTK) .
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es
Salaam tarehe 30 Septemba, 2014, na Mawaziri wa Nishati kutoka nchi hizo ambao
ni Waziri wa Nishati na Madini wa
Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya
Maji wa Zambia, Christopher Yaluma na Waziri wa
Nishati na Petroli wa Kenya Davis Chirchir.
Akizungumza
katika hafla hiyo Waziri wa Nishati na Madini, Tanzania Profesa Sospeter
Muhongo alieleza kuwa, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme unalenga
kuondoa tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa nchi hizo na barani Afrika.
Profesa Muhongo alisema ambalo litachangia katika kukuza uchumi wa
mataifa hayo, ikizingatiwa kuwa, nchi nyingi za Afrika bado zina uhaba wa
nishati ya umeme, ambayo ni kichocheo
kikuu cha maendeleo, hivyo, utekelezaji wake unatarajiwa kuziunganisha nchi za Kusini , Mashariki na Kaskazini mwa Afrika na
nishati hiyo.
Prof.Muhongo
aliongeza kuwa, ili nchi hizo ziweze kufanya biashara ya kuuziana umeme
itajengwa miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme katika nchi zote na
kuongeza kuwa, mkutano huo umekubaliana kwamba, kila nchi itabeba jukumu la
kujenga miundombinu ya mradi huo lengo likiwa kuhamasisha ushindani na
kuwezesha upatikanaji rahisi wa umeme katika nchi hizo.
“Ili umeme
uweze kuuzwa, lazima kila nchi ijenge miundombinu ya kusafirisha umeme huo. Tukumbuke
kwamba, umeme utakaouzwa ni wa ziada. Kwa hivyo, Tanzania itajenga miundombinu
yake vivyo hivyo kwa Zambia na Kenya”, alisisitiza Muhongo.
Akizungumzia
jitihada zilizofanywa Tanzania katika
utekelezaji wa mradi huo, alieleza kuwa, bei ya umeme nchini bado ni ghali
kutokana na matumizi ya mafuta yanayotumika kuzalisha umeme na kuongeza kwamba,
Tanzania tayari imeanza utekelezaji wa mradi huo kwa ujenzi wa njia ya umeme ya
msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa- Dodoma- Singida- na Shinyanga (backbone) ambao
ni sehemu ya mradi huo.
Vilevile,
Waziri Muhongo aliongeza kuwa, uwezeshaji wa ujenzi wa mtandao wa umeme wa
msongo wa kilovati 400 wa mradi wa Singida- Arusha hadi Namanga (Tanzania) na Namanga Isinya Kenya unaendelea
, wakati uchambuzi yakinifu wa ujenzi wa mtandao wa umeme wa njia ya Mbeya - Kasama Tanzania tayari
umekamilishwa na kinachofanyika hivi sasa ni kutafuta fedha za kukamilisha
ujezi wa mradi huo.
“Mradi kwa
nchi hizi tayari umeanza kutekelezwa. Makubaliano ya awali hayakuruhusu
ushindani. Tumeboresha namna tutavyotekeleza mradi huo. Tutatekeleza kwa pamoja
lakini kila nchi itautekeleza mradi huu kipekee,” alibainisha Waziri Muhongo.
Aidha,
Muhongo alisisitiza kuwa, hakuna haja ya nchi hizo kuendelea kuwa na upungufu
wa nishati ya umeme ikizingatiwa kuwa, nchi hizo zinayo rasilimali ya kutosha
yakiwemo makaa ya mawe, nishati jadidifu ikiwemo jotoardhi na gesi asilia.
Naye, Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya
Maji wa Zambia , Christopher Yaluma
alieleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo sio tu utaziwezesha nchi hizo kufanya
biashara bali pia utafungua fursa za uwekezaji na kusaidia katika kuondoa
umaskini miongoni mwa nchi wanachama kutokana kuzitumia fursa mbalimbali
zinazotokana na nishati ya umeme.
Waziri Yaluma
aliongeza kuwa, pamoja na kwamba mashauriano ya utekelezaji wa mradi huo yalichukua
miaka mingi kuanza kutekelezwa, hivi sasa nchi hizo zimeazimia kuhakikisha
kwamba mradi huo unatekelezwa.
Kwa upande
wake Waziri wa Nishati na Petroli Kenya, Davis Chirchir aliwataka washirika wa
maendeleo kusaidia katika kuwezesha utekelezaji wa mradi huo wa kujenga
miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme baina ya nchi hizo kutokana na
manufaa yake kwa bara la Afrika na kuongeza kuwa, kutokana na uwepo wa
rasilimali asilia za kutosha katika nchi hizo hakuna sababu ya kuwepo tatizo la
nishati katika nchi hizo na barani Afrika.
Naye, Katibu
Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika (COMESA) anayeshughulikia miradi Dkt. Kipyego Cheluget alizipongeza nchi
hizo kwa kuuendeleza utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua kipindi kirefu na
kuueleza kuwa, ni miongoni mwa miradi 16 ya kipaumbele na kimaendeleo kwa
Afrika.
Aidha, kwa
upande wao Washirika wa maendeleo waliohudhuria hafla hiyo, walionesha
kufurahishwa kwao na dhamira ya nchi hizo na kuahidi kushirikana na nchi hizo
kuhakikisha mradi huo unatekelezwa. Miongoni mwa washirika wa maendeleo
waliohudhuria ni pamoja na uwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia,
Ubalozi wa Norway, Shirika la Maendeleo
la Japani (JICA), African Development Bank(AfDB) na Ubalozi wa Ufaransa.
Mkataba
rasmi wa utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa kusafirisha na kuuziana umeme, unatarajiwa kusainiwa ifikapo tarehe 3
Novemba, 2014 nchini Zambia. Njia za ujenzi wa miundombinu hiyo ya kusafirisha umeme zinajengwa kutoka
nchini Kenya, kupitia Tanzania hadi
Zambia, ambapo Mawaziri wa nchi
husika walikubalina kukamilisha
utekelezaji wake ifikapo mwishoni mwa
mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment