Kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa handaki la kuchepusha maji katika
mradi wa Julius Nyerere, kazi inayofuatia ni uchepushaji wa maji ili
kuanza ujenzi wa tuta kuu.
Handaki hilo lina urefu wa mita 703 na upana wa mita 17 huku kimo chake kikiwa mita 12.
Akiongea kuhusu kufikiwa kwa hatua hiyo muhimu, Mhandisi Said Kimbanga
ambaye ni Meneja Ujenzi, amesema zoezi linalofanyika kwa sasa ni utoaji
wa udongo kwenye njia ya kuingilia maji, kufikia kwenye level ya 68.5
juu ya usawa wa bahari ili maji yaweze kupita.
"Hapa tulipo maji yanapita kuelekea baharini, hatuwezi kujenga tuta kuu
hadi tutakapo yachepusha maji kupita kwenye handaki na eneo hilo kubaki
kavu" alisema Mhandisi Kimbanga.
Aliongeza handaki hilo limekamilika kwa asilimia 100, zoezi
linaloendelea ni uondoaji wa vifaa ndani ya handaki na kukata udongo
uliopo mbele ya lango la kuingilia maji ili kuruhusu maji kuingia ndani
ya handaki.
Aidha, zoezi lingine litakalofanyika ni ujazaji wa udongo kwenye mto
kujenga tuta (cofferdam) ili kufunga mto na kuruhusu maji kupita kwenye
handaki mchepusho.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano TANESCO, Johary Kachwamba amesema
kukamilika kwa mradi wa Julius Nyerere Tanzania itakuwa na umeme wa
uhakika na wa gharama nafuu.
"Umeme unaozalishwa kwa maji ni umeme wa bei nafuu, kutokana na umeme wa
maji kuzalishwa kwa gharama kidogo hivyo tutarajie bei ya umeme kwa
Wateja kushuka" amesema Kachwamba.
Aliongeza, kutokana na umeme wa maji kuwa wa gharama nafuu ambapo unit
moja inazalishwa kwa shilingi 36 TANESCO itaweza kujiendesha kwa faida
zaidi.
"Tanzania inaelekea sehemu ya kihistoria, kwa kuwa na maendeleo
endelevu, tutaokoa mazingira kwani wananchi wataweza kumudu gharama za
umeme hivyo kuondoa matumizi ya kuni na mkaa" alisisitiza Kachwamba.
November 11, 2020
JNHPP - Zoezi la kuchepusha Maji kuanza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment