Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia mkataba wa kuuziana umeme
na kampuni sita binafsi ambazo zitaiuzia umeme TANESCO, Umeme ambao
utaingizwa moja kwa moja kwenye kwenye gridi ya Taifa na kutumika katika
maeneo mbalimbali Nchini.
Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mikataba kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Meneja Mwandamizi Uwekezaji, Mhandisi
Costa Rubagumya alisema wawekezaji hao wamekidhi vigezo kwa mujibu wa
kanuni zilizoidhinishwa na EWURA.
"Kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia uendelezaji wa miradi midogo ya
kuzalisha umeme, inaitaka TANESCO kuingia mikataba na wazalishaji umeme
wadogo kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa bado haijafika", alisema
Mhandisi Rubagumya.
Aliainisha vigezo vingine ni maeneo ambayo yanatatizo la umeme mdogo ili
kuimarisha ubora wa umeme na kigezo kingine ni maeneo ya usambazaji
umeme ambapo njia za umeme za TANESCO ni ndefu hivyo kusababisha
upotevu wa umeme.
Mhandisi Costa alizitaja kampuni hizo kuwa ni, Kahama Solar Power
Project MW 10.0, Kigoma Solar Power MW 5.0, Nishati Lutheran (DKK)
Investment Ltd MW 0.36.
Makampuni mengine ni, Madope Hydropower MW 1.7, Luponde Hydropower MW 0.9 na Maguta Hydropower MW 1.2.
Wakizungumza Kwa niaba ya Wazalishaji wadogo wa umeme, Padre Luciano
Mpoma na Nicholas Richardson wameishukuru Serikali kupitia TANESCO kwa
kukubali kufanya nao biashara ya umeme.
Waliongeza kuwa safari ilikuwa ni ndefu lakini hatimaye wamekuwa na
furaha kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha nishati ya umeme inamgusa
kila mwananchi.
Makampuni hayo yanatakiwa kuanza kuiuzia TANESCO umeme ndani ya miezi 18 kuanzia leo Disemba 08,2020.
No comments:
Post a Comment