Na Henry Kilasila, Iringa
Wahandisi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wameanza
kunolewa katika kutambua nguzo bora za kusambazia umeme majumbani katika
kukabiliana na matumizi ya nguzo zisizo na ubora na ili kuongeza ufanisi na
usalama katika zoezi la kusambaza umeme nchini.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yanayofanyika mkoani
Iringa kujumuisha wahandisi wakuu wa umeme, maafisa mipango na maafisa usalama
wa TANESCO yana lengo la kuwawezesha wataalamu hawa kuwa na weledi wa hali ya
juu katika kutambua nguzo zenye sifa na umadhubuti na salama katika zoezi la
usambazaji umeme nchini.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Mkoa wa Iringa
Mhandisi Seraphine Lyimo alisema anaamini
mafunzo haya yatawawezesha washiriki kufanya vizuri zaidi katika utendaji wao
wa kazi na kuongeza kuwa Shirika halitapata tena nguzo ambazo hazina viwango na
kuwataka washiriki kuendelea kujisomea zaidi na kuzielewa nguzo ili kuokoa rasilimali
chache za Shirika.
Mhandisi Lyimo aliongeza kuwa mafunzo
hayo yana faida kubwa kwa TANESCO kwani yatasaidia Shirika kuepuka kununua
nguzo feki na hivyo kuweza kuliepushia Shirika hasara zisizo za lazima.
“Nawaomba muzingatie mafunzo haya ili muje kutumia
utaalamu huu katika kulisaidia Shirika wakati wa manunuzi ili kuweza kuwapatia
Watanzania huduma bora na salama ili kukidhi kiu yao ya hupatikanaji wa umeme,”
alisema Mhandisi Lyimo.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Prof. Reuben Mwamakimbullah kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo
(SUA), alisema kuwa baadhi ya vitu vinavyochangia kuharibu ubora
wa nguzo ni pamoja na kutoboa nguzo matundu wakati imeshawekewa dawa; na
kuongeza kuwa maji nayo huchangia kuzuia
uwezo wa dawa kupenya kwenye nguzo na ujazo wa hewa ndani ya nguzo ambayo
inatakiwa nayo itolewe ili dawa iweze kupata nafasi.
Prof. Mwamakimbullah aliwasihi washiriki wa mafunzo
hayo kuwa waangalifu katika utambuzi wa nguzo za matumizi ili kuokoa uwezekano
wa kuhatarisha maisha ya watumiaji na pia kuliokolea Shirika hasara.
“Nawaomba
muzingatie ubora wa nguzo kwa kuzingatia
unaandaaje nguzo zako, unatumia dawa gani na unatumia njia gani kuingiza dawa
katika nguzo,” aliwasihi Prof. Mwamakimbullah.
Prof. Mwamakimbullah aliwataka washiriki
kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana akiwasihi ili kufikia malengo ya
Shirika wataalamu hao hawana budi kushirikiana na wengine ili kuwezesha TANESCO
huduma bora na bidhaa bora.
Naye msimamizi wa mafunzo hayo Meneja
wa kitengo cha usalama kazini wa TANESCO, ambao ndio waandaji Mhandisi Majige Mabulla
alisema: “Tunategemea kuona ufanisi
katika utendaji kutokana na mafunzo haya mkayoyapata, kwa faida ya kwako
mshiriki na pia kwa faida ya Shirika.”
Kwa
mujibu wa taratibu za usalama, nguzo inatakiwa kwa kawaida ikae sio chini ya
miaka 40 na takwimu zinaonesha kuwa nguzo zisizo na ubora kwa wastani wa
hazifiki miaka zaidi ya saba.
Washiriki
wakifuatilia mafunzo kwa umakini |
Afisa Rasilimali watu wa TANESCO, Bw. Dickson Hunter akiwakaribisha washiriki (hawapo pichani) katika mafunzo na kuwataka waendelee kufuata sheria zote za kazi. |
Kaimu Meneja wa Mkoa wa Iringa Mhandisi Seraphine Lyimo akifungua mafunzo hayo awamu ya pili. |
Prof. Reuben Mwamakimbullah kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) akionesha kwa vitendo namna kuangalia maji kwenye nguzo kwa kutumia kifaa kinachoitwa ‘Electrical Resistance Metter’. |
No comments:
Post a Comment