Wahandisi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wanaonolewa
katika kutambua nguzo bora za kusambazia umeme wameanza mafunzo ya vitendo ya
ukaguzi na utambuzi wa nguzo bora na salama katika baadhi ya viwanda vya
kuzalishia nguzo hizo mkoani Iringa.
Ziara ya wahandisi hao wa TANESCO inalenga katika
kuwawezesha katika kukabiliana na matumizi ya nguzo zisizo na ubora na ili
kuongeza ufanisi na usalama katika zoezi la kusambaza umeme nchini.
Wahandisi hao wamepata fursa ya kutembela kiwanda cha
Sao Hill kilichopo Mafinga mjini Iringa ikiwa ni mafunzo kwa vitendo juu ya
utambuzi wa nguzo bora.
Washiriki waliweza kuona namna uzalishaji na
utayarishaji wa nguzo unavyofanyka ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa nguzo kabla
haijawekewa dawa na ukaguzi wa nguzo baada ya kuwa ya kuwekewa dawa.
Akivitaja vitu vinavyoangaliwa kabla nguzo
haijawekewa dawa Bw. Emmanuel Simkoko ambae ni mkaguzi kutoka Kampuni ya
Ukaguzi wa Ubora ya SGS ya jijini Dar es Salaam, alisema vitu vya kuzingatia
katika zoezi la utambuzi wa ubora wa nguzo ni pamoja na aina ya mti unaotumika
katika kuandaa nguzo hizo, ukubwa, pamoja na kimo cha nguzo husika.
“Kuna vitu vya kuzingatia wakati wa kuchambua aina ya
ubora wa nguzo, ni muhimu kujua aina ya mti ili kubaini hali ya unyevunyevu, na masuala mengine ya
utaalamu ikiwamo vipimo vya nguzo husika,” alisema Bw. Simkoko.
Kwa mujibu wa Bw. Simkoko, nguzo bora haitakiwi kuwa
na hali ya unyevunyevu kuvuka 25%, pamoja na ukubwa wa kitako cha nguzo kisipungue
milimita 20 na juu ya nguzo isipungue milimita 20.
Wahandisi hao walielimishwa sifa nyingine ya nguzo
bora kuwa ni pamoja na kuangalia nguzo kama imeliwa na wadudu, umbo la nguzo
iliyo panda haifai kwa kuwa haitoweza kukidhi kazi husika.
Bw. Simkoko alihitimisha kwa kuwaelimisha wahandisi
hao namna ya kuwekea dawa nguzo zilizo bora, “Baada ya nguzo kuwekewa dawa huwafanyiwa
majaribio kuangalia dawa kama imewekwa ipasavyo, na tuna utaratibu wa
kuzifanyia majaribio kila mwezi,” aliongeza Bw. Simkoko.
Wahandisi wa TANESCO wapo mkoani Iringa kwa mafunzo ya
wiki mbili yenye lengo la kuwawezesha wataalamu hao kuwa na weledi wa hali ya
juu katika kutambua nguzo zenye sifa na umadhubuti na salama katika zoezi la
usambazaji umeme nchini.
Ukaguzi 1 –3
Wahandisi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wakiwa katika mazoezi
mbalimbali ya kubaini nguzo bora
yanayofanyika katika Kiwanda cha Sao Hill, mkoani Iringa.
|
Bw. John Mwaura Njenga ambae ni Meneja wa Poles and Timber Implementation akitoa maelezo kwa
Wahandisi wa TANESCO namna kiwanda kinavyofanya kazi.
|
Wahandisi wakiwa maabara wakifanya majaribio ya namna kiasi cha dawa kilivyoingia ndani ya nguzo wakipata na maelekezo kutoka kwa Boniface Mwansatu ambae ni Mdhibiti Ubora kutoka Kampuni ya SGS. |
No comments:
Post a Comment