SHIRIKA la Umeme Tanzania, (TANESCO), limetoa siku 14 kwa
Wateja wake wote linalowadai kulipa madeni yao, vinginevyo litasitisha utoaji
wa Huduma ya Nishati kwa wahusika.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari Machi 9, 2017 Ofisini
kwake Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito
Mwinuka, (Pichani juu) alisema, Shirika linadai jumla ya Shilingi Bilioni 275.38.
Akifafanua zaidi alisema, Wizara na Taasisi za Serikali
zinadaiwa zaidi ya Shilingi Bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO),
linadaiwa zaidi ya Shilingi Bilioni 127.87, na Makampuni binafsi na Wateja
wadogo wadogo deni ni zaidi ya Shilingi Bilioni 94.97.
“Zoezi hili litaambatana na utoaji taarifa (notice) kwa
wadaiwa wote kulipa madeni yao ndani ya kipindi cha siku 14, baada ya hapo
Shirika litachukua hatua ya kusitisha Huduma kwa Wateja watakaoshindwa kuanza
kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria.” Alisema Dkt. Mwinuka.
Aidha, alisema kwa wale Wateja wadogowadogo, Shirika
halitawaandikia barua kwani ni wengi, isipokuwa kupitia ofisi ya Uhusiano ya
Shirika, wataarifiwa kupitia vyombo vya habari
Alisema Malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha
jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya Shirika kwa
wakati, ikiwemo shighuli za Uendeshaji Shirika, Matengenezo ya Miundombinu
pamoja na utekeelzaji wa miradi mbalimbali.
“Ni matarajio ya Shirika kuwa kuli[wa kwa malimbikizo haya ya
madeni, kutasaidia TANESCO kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi mkubwa zaidi
na hivyo kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea
nishati ya umeme hapa Nchini.” Alihitimisha Dkt. Mwinuka.
Taarifa hii ya TANESCO imekuja ikiwa ni siku chache baada ya
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kuliagiza Shirika hilo, kuwakatia umeme wale
wote wanaodaiwa ikiwemo taasisi nyeti za Serikali na hata Zanzibar.
Rais alitoa agizo hilo wakati akizindua ujenzi wa mradi wa
ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wa Kilovolti 132 mkoani Mtwara
ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi.