January 10, 2018

TANESCO yawashukuru Wateja kwa mchango mkubwa mwaka 2017


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Dkt. Tito E. Mwinuka amewashukuru Wateja, wanahabari na wadau wote kutokana na mchango mkubwa kwa Shirika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ambazo zimeisaidia TANESCO katika kuboresha huduma zake.

Aidha, amesema hali ya uzalishaji umeme unaendelea vizuri kutokana na kuanza kufanya kazi kwa mashine mbili kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi II, kukamilika kwa ukarabati wa mashine ya kufua umeme Kidatu, na kuongezeka kwa kina cha maji kwenye bwawa la Mtera, kuimarika huku kumepelekea TANESCO kuwa na umeme wa ziada.

Akizungumzia njia za kusafirisha umeme, alisema ukarabati wa miundombinu unaendelea katika njia za kusafirisha umeme.

“Suala la kukatika kwa umeme Kigamboni, ufumbuzi wake utapatikana baada ya kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 132 ambapo njia hiyo imefika kituo kipya cha Mbagala”. Alisema Dkt. Mwinuka.

Aliongeza hivi sasa Kigamboni inatumia umeme kutoka njia ya umeme ya kilovolti 32 ya Kipawa – Chang’ombe ambayo pia inatumiwa na Viwanda.

Alisema, licha ya mvua kuwa na changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya umeme lakini inafaida kwa TANESCO katika mabwawa kwani inachangia asilimia 41.5.

January 7, 2018

Waziri Mkuu: “Umeme ni fedha, Kuwepo kwa Umeme ni Ajira tosha”

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma ameweka jiwe la msingi la mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na ujenzi wa jengo la Ofisi ya TANESCO Mkoani Ruvuma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la ziara hiyo ni kuwatayarisha Wananchi juu ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali huku akieleza msimamo wa Serikali ni maslahi ya nchi kwanza.

Aliongeza, mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Nishati, ni kuona mtandao wa umeme unaenea pote nchini,  na katika Vijiji ambavyo ni vigumu kufikika kwa miundombinu ya umeme Vijiji hivyo vitatumia umeme wa jua (Solar System).
Ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi TANESCO kupitia kwa Mwenyekiti wake Dkt. Alexander Kyaruzi, Menejimenti ya TANESCO pamoja na Wafanyakazi kwa kuunga mkono katika utekelezaji wa Sera za Serikali. 

“Nimpongeze Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi kwa namna Bodi inavyosimamia, hongera sana wana TANESCO kwa kuunga mkono jitihada za Serikali”. Alisema Mhe. Majaliwa.

Aidha, alisema amefarijika sana kwa kuhakikishiwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti na jingo la Ofisi mwezi Machi mwaka huu.

Aliongeza kufika kwa umeme wa gridi kutafungua fursa za kibiashara kwa Wananchi wa maeneo hayo hivyo kutokuwepo malalamiko ya ukosefu wa ajira kwa watu kujiari, “Ndugu zangu Umeme ni fedha, Kuwepo kwa Umeme ni Ajira tosha, hivyo tuwekeze katika biashara ndogo ndogo za kutuingizia kipato”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema katika kipindi cha Miaka miwili ya  Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na mafanikio katika sekta ya nishati nchini ambapo katika njia za kusafirisha umeme mkubwa zimejengwa mbili ambazo ni mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga na mmradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Makambako Mkoani Njombe  hadi Songea Mkoani Ruvuma wenye urefu wa kilometa 250.

Aliongeza kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme ya Makambako hadi Songea kutaipunguzia TANESCO gharama kwa kuacha kutumia mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta katika vituo vya Songea, Mbinga Namtumbo na Madaba .January 4, 2018

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU WATEJA WALIOHAMISHWA KUTOKA MITA ZA ZAMANI KWENDA LUKU WAKIWA NA MADENIShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tunawataarifu Wateja wetu wenye madeni, ambao walihamishwa kutoka mita za zamani (Conversional Metter) kwenda mita za LUKU kuwa,
Hapo awali walipokuwa wakifanya manunuzi ya umeme, nusu ya fedha ilikatwa kulipa deni la umeme, TANESCO sasa imebadilisha, na  kuweka mfumo mfumo ambao utawezesha madeni hayo kumalizika ndani ya miaka miwili (2).

Kwa wale ambao madeni yalitokana na wizi wa umeme yanatakiwa yakamilike ndani ya miezi sita (6).

Kwa mawasiliano toa taarifa kupitia,
Kituo cha miito ya simu Makao Makuu +255 222 194 400 na +255 768 985 100
  
Tovuti: www.tanesco.co.tz, mitandao ya kijamii: Twitter, www.twitter.com/tanescoyetu,


IMETOLEWA NA: OFISI YA UHUSIANO
                                 TANESCO MAKAO MAKUU
                                  JANUARI 04, 2018

January 2, 2018

Mhe. Mgalu akagua maendeleo ya ubomoaji jengo la TANESCO Makao Makuu


Naibu Waziri Nishati Mhe. Subira Mgalu, amekagua maendeleo ya ubomoaji wa jengo la TANESCO Makao Makuu ambapo ameridhishwa na hatua zinazoendelea.

Akielezea hatua za ubomoaji kwa Mhe. Naibu Waziri, Meneja Miradi Mhandisi Emmanuel Manirabona alisema suala la ubomoaji jengo lilianza kutekelezwa Novemba 17, 2017 baada ya kupewa notisi ya siku thelathini, ambapo Novemba 26, 2017 Wizara ilitembelea ili kukagua hatua zilizokwisha fikiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Aliongeza kati ya Novemba 27 na Desemba 06, 2017 zilifanyika kazi za kuondoa fanicha katika jengo linalobomolewa, pamoja na ubomoaji wa majengo ambayo sio ya ghorofa.

Desemba 4 hadi Desemba 10, 2017 ilifanyika kazi ya kuondoa mifumo (Miundombinu) ya TEHAMA.

Aidha, alifafanua kuchelewa kwa ubomoaji kumetokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupatikana kwa vifaa sahihi vya kubomolea.

Akielezea utekelezaji wa mradi alisema,  ubomoaji ghorofa ya tisa umekamilika na inatarajiwa jengo zima kukamilika Januari 11, 2018.

December 24, 2017

HUDUMA ZETU KIPINDI CHA SIKUKUU

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawatakia Wateja wake heri ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya wa 2018.

Katika kusherehekea msimu huu wa Sikukuu, Shirika limejipanga kuhakikisha Wateja wetu mnaendelea kupata huduma bora na za uhakika saa 24.

Huduma zetu za dharura (Emergency) na Huduma kwa Wateja (Customer Care) zitapatikana muda wote.

Tunawaomba Wateja wetu kutupatia taarifa zitakazosaidia Wataalamu wetu kukufikia wa wakati kupitia kituo cha Miito ya Simu, Naba za Mikoa na Wilaya pamoja na mitaandao ya kijamii.

Imetolewa na: Ofisi ya Uhusiano
                        TANESCO Makao Makuu.

December 21, 2017

BODI YA WAKURUGENZI TANESCO YATEMBELEA MIKOA YA KUSINI


Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dk. Alexander Kyaruzi (Pichani anayesaini) na baadhi ya Viongozi Waandamizi wa TANESCO, imefanya ziara katika Mikoa ya Kusini.

Lengo la ziara ziara hiyo ni kukagua sambamba na kujionea kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme inayoendelea katika Mikoa hiyo ikiwemo miradi ya kufua umeme na ile ya usafirishaji.

Aidha, ziara hiyo imetumika kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za Wateja wa Shirika.December 15, 2017

Dkt. Kalemani aendelea na ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya umeme

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameendelea na ziara ya kukagua hatua iliyofikiwa katika ukamilishaji wa ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua uimara wa mitambo ili Serikali kupitia TANESCO iweze kujipanga vizuri kwa kuwa na umeme wa uhakika.

"Kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika". Alisema Dkt. Kalemani.

Katika ziara hiyo pia amekagua miradi ya umeme Vijijini Awamu ya Tatu inayoendelea katika Mikoa hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Akikagua mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Dkt. Kalemani alisema mradi huo utaiunganisha Mkoa wa Ruvuma katika Gridi ya Taifa.

Pia, kukamilika kwa miradi hiyo kutaipunguzia gharama Serikali kwa kuondokana na mitambo ya mafuta.