September 26, 2021

TANESCO MPYA IMEZALIWA LEO, TUNATAKA IENDESHWE KIBIASHARA- Waziri Makamba

 

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amesema ni wakati sasa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuanza kujiendesha kibiashara, kwa ufanisi ili kuchangia uchumi wa Taifa.

Mhe. Makamba amesema hayo leo Septemba 26, 2021 wakati akizungumza na Mameneja wa TANESCO wa ngazi ya Kanda, Mikoa, Wilaya na Makao Makuu. 

Aidha Mhe. Makamba amewatambulisha Wajumbe wa Bodi ya TANESCO wakiogozwa na Mwenyeki, Bw. Omari Issa, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Maharage Chande, walioteuliwa Septemba 25, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe wa Bodi ya TANESCO waliotambulishwa ni pamoja na Bw. Nehemia Mchechu, Bi. Zawadia Nanyaro, Bw. Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Masawe, Balozi Mwanaidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim,  Bw. Abubakar Bakhresa na Bw. Christopher Gachuma.

Mhe. Makamba amesema Bodi iliyochaguliwa ina wajumbe kutoka nyanja mbalimbali na watasaidia Shirika kufikia malengo.

 "Tunataka baada ya miaka mitatu Shirika liingie katika orodha ya mashirika bora, yenye thamani na yanayoheshimika Afrika" alisema Mhe. January Makamba

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Bw. Omari Issa, amesema atahakikisha Bodi inafanya kazi na kutimiza malengo yake kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na uwajibikaji.

 Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Maharage Chande, ameeleza vipaumbele ambavyo ni masilahi ya rasilimaliwatu, Wateja wa Shirika na utekelezaji wa mipango, hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa TANESCO.

"Nimhakikishie Mhe. Waziri tutahakikisha tunarudisha heshima ya Shirika na ufanisi kupitia ushirikiano wenu, hakuna Shirika lolote linalotoa huduma ya umeme zaidi yetu sisi, yamkini tuwape wateja wetu huduma wanayostahili", " alisema Bw. Maharage Chande

Meneja Mwandamizi Rasilimaliwatu, Bw. Francis Sangunaa, aliwahakikishia viongozi ushirikiano kwa niaba ya wafanyakazi wa TANESCO.
 



 

September 4, 2021

MIRADI YA KIMKAKATI YA NISHATI ITAKAMILIKA KWA WAKATI

 

Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali amesema miradi yote ya kimkakati ya umeme inayotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO itakamilika kwa wakati.

Bw. Mahimbali ameyasema hayo leo Septemba 03, 2021 katika ziara ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, kukagua vituo vya kuzalisha umeme kwa gesi vya Kinyerezi.

Amesema ziara ilijikita zaidi kwenye mradi wa Julius Nyerere, ambapo Sekretarieti iliweza kufahamu hatua zote za kuzalisha umeme hadi kuusafilisha.

"Leo tumewaonesha Kinyerezi complex ambayo ina Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension pamoja na Kinyerezi ll" amesema Bw. Mahimbila.

Ametoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuendeleza miradi ya umeme nchini.

Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri inahitimisha leo ziara ya siku tatu kukagua miradi ya umeme, ziara ilianzia kwenye kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Zuzu Jijini Dodoma, njia ya umeme itakayojengwa hadi Chalinze na mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere.





 

September 3, 2021

Mkandarasi JNHPP ameshalipwa trilioni 2.7

 


 Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema Mkandarasi anaetekeleza mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) Mw 2115 ameshalipwa jumla ya shilingi trilioni 2.7 kulingana na mpango kazi kati ya shilingi trilioni 6.5 anazotakiwa kulipwa hadi kukamilika kwa mradi.

Dkt. Mwinuka ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 03, 2021 katika ziara ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Ikulu na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa upande wake Karani wa Baraza la Mawaziri, Bw. Nsubili Joshua amesema ameongozana na Maafisa wa Sekritarieti ili kujionea kazi inavyoendelea JNHPP.

Amesema mradi wamekuwa wakiufahamu kwenye makaratasi hivyo wamefika kujionea hali halisi na kuona kinachoendelea.

Ameongeza kuwa wameona mambo makubwa ambayo hawayajatarajia na kutoa pongezi kwa viongozi wakuu Serikalini kwa kuutekeleza mradi huo.

Awali akieleza lengo la ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma, Bw. Lauren Ndumbaru amesema wamefanya ziara katika mradi na watumishi wa umma wa ngazi zote ili watumishi waweze kuona na kuthamini kazi ambayo Serikali inafanya katika ujenzi wa miradi ya kimkakati.

"Naamini kabisa mradi wa Julius Nyerere ukikamilika utaleta maendeleo makubwa katika Nchi yetu, niombe watumishi wa umma wafanye kazi kwa bili na waendelee kuiunga mkono Serikali ili tuone matokeo mapema" amesema Bw. Ndumbalo

Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali amesema Wizara ya Nishati imefarijika kutokana na Ofisi zote mbili kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere.

"Tunamshukuru Rais Samia Hassan kwa kuendelea kuuangalia mradi huu kwa jicho la kipekee kabisa, tunapata pesa za kuendeleza mradi kwa wakati na usimamizi mzuri, tutaendelea kuusimamia na kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati" amesema Bw. Mahimbila.