November 18, 2019

Dkt. Medard Kalemani Ahamasisha Wawekezaji wa MigodiWaziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani Ahamasisha Wawekezaji wa Migodi, Hoteli na Viwanda kuunganisha umeme wa bei nafuu Wa TANESCO Mkoani Mara ili kuongeza ufanisi pamoja na kuboresha zaidi biashara zao ambapo amesema kuwa, TANESCO tayari inapeleka umeme mwingi wa takriban Megawati 82 Mkoani humo lakini matumizi ya Mkoa mzima kwa sasa ni takriban Megawati 33 ambazo ni chache mno ukilinganisha na shughuli za kiuchumi zilizopo mkoani humo.

Waziri Kalemani aliyasema hayo alipotembelea Mkoa huo kwa ziara ya kikazi ya kukagua na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Umeme Mkoani humo hususan Miradi ya umeme Vijijini pamoja na Mijini.

‘’Mkoa wa Mara, una fursa mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo Viwanda, Mahoteli na raslimali kubwa ya madini na migodi mingi ambayo bado haijaunganishwa na umeme wa gharama nafuu wa TANESCO na wanatumia vyanzo ghali vya Umeme wa mafuta kuendesha biashara zao’’, Alisema Dkt. Kalemani

Aidha Dkt. Kalemani aliagiza, TANESCO Mkoa wa Mara na Mikoa mingine ambayo bado matumizi ya umeme yako chini, ukilinganisha na umeme unaopatikana maeneo hayo kuhakikisha kuwa wanaanzisha kampeni kabambe ya mlango kwa mlango kutembelea Wawekezaji na Wafanyabiashara wote katika maeneo yao ambao bado hawajaunganisha umeme wa TANESCO ili kuwaelimisha na kuwahamasisha kuunganisha umeme wa TANESCO kwani hivi umeme wa TANESCO ndio chanzo nafuu kabisa cha Nishati, ambayo imesambaa maeneo mengi Nchini na ndio Nishati ya uhakika na unaotabirika kwa sasa.

Aliongeza kuwa kwa kutumia Umeme Nafuu wa TANESCO, itawezesha gharama za uzalishaji mali na uendeshaji kupungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuchochea zaidi ukuwaji wa shughuli hizo kwa ujumla ikiwemo viwanda, Migodi, Mahoteli na Shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo pia zitachochea ukuwaji wa Uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.
November 15, 2019

Dkt. Kalemani aipa maagizo mazito Bodi ya Wakurugenzi TANESCOWAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani leo Novemba 15, 2019 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) aliyoiteua juzi Novemba 13, 2019.

Dkt. Kalemani akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu, ameizundia Bodi hiyo yenye wajumbe 9 juzi jijini Dodoma na kuipa maagizo yapatayo 16.

Bodi hiyo itaongozwa na Dkt. Alexander Kyaruzi ambaye aliteuliwa Novemba 9, 2019 na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kipindi kingine cha pili kuongoza Bodi hiyo.

Akizindua Bodi hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu, Dkt. Kalemani alimemkabidhi Mwenyekiti Dkt. Kyaruzi kitendea kazi ambacho ni Sheria ya Umeme ya Mwaka 2008 aliyosema ndiyo itakayowaongoza katika majukumu yao.
Aidha, aliwapa maelekezo ya kuwa umeme ndio injini ya uchumi wa viwanda hivyo ni lazima waisimamie Tanesco kuhakikisha umeme unapatikana katika shughuli zote za kiuchumi nchini. Alitaka uwepo umeme wa kutosha na unaotabirika ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali.
Aliwataka wakasimamie miradi hiyo iliyoanza kutekelezwa na itakayotelezwa na Tanesco, na katika hilo, wahakikishe Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji wa megawati 2,115, unakamilishwa kwa wakati ifikapo Juni 14, 2022, kama ilivyoelezwa katika mkataba.
Aliitaja miradi mingine kama wa Ruhuji megawati 358, Rumakari megawati 222 na Malagarasi na mengine, inasimamiwa na kukamilika kwa wakati.
Aliwataka kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 njia zote za kusafirishia umeme zinaunganishwa na Gridi ya Taifa katika kona zote za Tanzania, kwa kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wawe wameanza kutumia umeme wakiwamo wale wanaoishi vijijini.
Dkt. Kalemani pia aliitaka bodi kuhakikisha wanarekebisha, wanaboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirisha umeme, kuisimamia TANESCO na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika miradi ya umeme vijijini kwa kuwabana makandarasi kukamilisha miradi kwa wakati.
“Tusingependa kuongeza hata dakika moja kwa mkandarasi katika mradi wowote ule, tunataka wakabidhi miradi kwa wakati,” alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, aliitaka bodi kuhakikisha viwanda vinapata umeme wa uhakika kwa kutumia transfoma kubwa zenye uwezo wa kuchukua umeme mwingi, na pia kusisitiza mita, transfoma, na nyaya haziuzwi kwa mwananchi yeyote na atakayekiuka agizo hilo achukuliwe hatua.
Alisisitiza kuwa kwa vijijini, mwananchi aunganishiwe umeme kwa Sh 27,000 tu, na atakayekiuka hilo, naye achukuliwe hatua na bodi kwa yule aliye kwenye mamlaka yao.
Kuhusu mapato ya shirika, alitaka wasimamie ukusanyaji huo wa mapato, na kuagiza kuwa kwa yeyote ambaye anadaiwa Ankara na Tanesco akatiwe huduma mara moja na hasa kama madeni hayo ni sahihi na halali.
Aliagiza pia kuyaaangalia maeneo yenye tija kama viwanda, mitambo ya kusukuma maji, zahanati na mengine na kukusanya mapato, huku akiisifu Tanesco kwa kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 9 hadi kufikia Sh bilioni 46 na kutaka waongeze bidii ifike Sh bilioni 60.
Aidha, aliwataka kuongeza vyanzo vya mapato, kuondoa kero ya watu wanaosubiri kuunganishiwa umeme kwani nguzo na nyaya zipo za kutosha, kudhibiti vishoka wachache waliopo, kuhakikisha katikakatika ndogo ya umeme iliyopo inakuwa historia na kuwajengea uwezo wazalishaji wadogo wa umeme nchini.
Mbali ya kuwataka kuwa wabunifu na wenye uthubutu kwa kufanya kazi kwa kuzingatia kasi, wepesi na nidhamu, aliwaagiza kuwa sheria za manunuzi zisiwe kificho cha kuchelewesha kazi.
Kuhusu Jiji la Dodoma, aliagiza liangaliwe kwa ukaribu na kila eneo lipate huduma ya umeme, na hilo anataka kuliona limefanyika ndani ya miezi sita.
Katika utekelezaji wa hayo yote, Dkt. Kalemani ameagiza Bodi itoe taarifa kwa wizara kila baada ya miezi mitatu kuelezea utendaji wao wa kazi.
Naibu Waziri Mgalu kwa upande wake, aliwatakia kila la heri wajumbe wa bodi hiyo, na kueleza kuwa wizara inawategemea sana katika kusukuma mbele majukumu hasa ya kulisimamia shirika hilo la TANESCO.
Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Kyaruzi na wajumbe wake waliokuwapo jana, waliahidi kutekeleza maelekezo yote hayo ya Waziri kwa ushirikiano, uadilifu, weledi, na kutoa utumishi uliotukuka ili kuisaidia serikali katika sekta ya umeme kufikia Tanzania ya viwanda ifikapo 2025.November 13, 2019WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameteua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye wajumbe wanane.

Dkt. Kalemani amefanya uteuzi leo Novemba 13, 2019, unatokana na Rais John Magufuli kumteua Dkt. Alexander Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa kipindi kingine cha pili.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimteua Dkt. Kyaruzi Novemba 9, mwaka huu baada ya kuwa ameshika wadhifa huo kuanzia Mei 2016 hadi Mei 2019.

Dkt. Kalemani alisema wajumbe hao wapya watakaa madarakani kuanzia Novemba 13, 2019 hadi Novemba 12, 2022.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Balozi Dk James Nzagi (alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO iliyomaliza muda wake) na Dkt. John Kihamba (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saam - DUCE).

Wengine ni Dk Lugano Wilson (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi na Mkuu wa Teknolojia za Nishati - TIRDO), John Kulwa (Mkuu wa Idara ya Ukaguzi Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi - MUHAS) na Denis Munumbu (Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU).

Wengine ni Dk Gemma Modu (Mkurugenzi NACTE), Mathew Kirama (Mkurugenzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Gilay Shamika (Mjumbe katika bodi iliyopita).

Dkt. Kalemani alimpongeza Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua tena Dkt. Alexander Kyaruzi kuisimamia Bodi hiyo.

Alimtaka Mwenyekiti huyo kulitumikia Shirika kwa Kasi, weledi na nidhamu ili kuwahudumia watanzania kwa kuondoa kero ndogo na kuifanya heshima ya Watanzania kwa TANESCO iendelee.

"Ni matumaini yetu mtakuja na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya katika kutekeleza azma ya Hapa Kazi Tu ili kulipa nguvu Shirika letu," alisema Dkt. Kalemani.

Kwa wajumbe wote, aliwataka wachape kazi ili kuhakikisha wadau wa Tanesco wanafaidi huduma nzuri na kuhakikisha Umeme unawafikia watanzania wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Dk Kyaruzi alimshukuru Rais Magufuli kwa heshima kubwa kwake kwa kumteua tena kulisimamia shirika hilo.

Alisema TANESCO miradi mingi ya kimkakati ukiwamo Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 na wa Rusumo mkoani Kagera.

Alisema miradi hiyo na mingine wataisimamia kikamilifu kwa kuweka mikono yao humo kwa kufuata miongozo mbalimbali wanayopewa na viongozi wao.

Miongoni mwa waliohudhuria ni kikao hicho ni, Naibu Waziri Nishati Mhe. Subira Mgalu, Katibu Mkuu Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mhandisi Leonard Masanja Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Dkt. Alexander Kyaruzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt.Tito Mwinuka na Viongozi Wandamizi wa Wizara ya Nishati