April 26, 2018

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Africa Dkt .Akinumwi A . Adesina, ametembelea kituo cha Kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Africa Dkt .Akinumwi A . Adesina, ametembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu kilichopo Mkoani Dodoma, na kujionea jinsi kituo hicho kilivyo saidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa huo.

Kituo hiki ni miongoni mwa vituo vilivyo karabatiwa kupitia mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga ya msongo wa Kilovolti 400 ujulikanao kama  "Backbone project"  ulio jengwa kwa  ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Africa.

Vituo vingine vilivyo karabariwa katika mradi huu ni pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Tagamenda kilchopo Mkoa wa Iringa, Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Singida  pamoja na Kile cha Ibadakuli Shinyanga.

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Subira Mgalu, alimshukuru Dkt. Adesina pamoja na Uongozi wote wa Benki ya AfDB kwa kuipa kipaumbele miradi ya maendeleo ikiwepo miradi mikubwa ya umeme ambapo Tanzania ni mmoja wa wanufaika wa miradi hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango alitoa shukrani kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika   kwa ufadhili wa miradi mbali mbali ikiwemo ya umeme, Kilimo ,pamoja na miundombinu.

Dkt. Mpango alimhakikishia Rais wa Benki ya AfDB kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa MheshimiwaRais, Dkt.  John Pombe Joseph Magufuli itahakikisha fedha zote zinazotolewa na Benki hiyo zinatumika vema katika miradi iliyo lengwa  ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata  maendeleo kupitia miradi hii kama ilivyo tarajiwa.

Naye Mhandisi Peter Kigadye kwa niaba ya Mkurugenzi wa TANESCO aliwahakikishia  wageni wote kua kupitia mradi huo Mikoa ya Kanda ya kati imekuwa na umeme wa uhakika pia kupitia mradi huo zaidi ya vijiji 121 vitanufaika kwa kupatiwa umeme kwa gharama nafuu ya shilingi  27,000 tu ,pia baadhi wa wakazi walio vunjiwa nyumba zao kupisha mradi wamenufaika kwa kujengewa upya nyumba za kisasa kabisa , hii ni pamoja na majengo ya taasisi mbali mbali kama makanisa zahanati shule pamoja na misikiti iliyovunjwa kupisha mradi ilijengwa upya .  Zaidi Mradi huu umemaliza tatizo la umeme katika migodi iliyo kanda ya ziwa kwani kwa sasa eneo lote la migodi hii linapata umeme wa uhakika na wa kutosha .