November 24, 2016

UWEKEZAJI WA TANESCO WAFIKIA SHILINGI TRILIONI 5.35, NI MKUBWA KATIKA HISTORIA YA UMEME NCHINI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini, (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Novemba 24, 2016. Alikuwa akitoa ufafanuazi kuhusu masuala muhimu ya TANESCO. Wengine pichani, kulia ni Meneja wa Vyuo vya TANESCO, Mhandisi Said Msemo na kushoto ni Kaimu Meneja Uhisano wa Shirika hilo, Leila Muhaji.

NA MAGRETH SUBI
SERIKALI kupitia TANESCO imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Miradi mbalimbali ya Umeme yenye thamani ya Shilingi Trilioni 5.35, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 24, 2016.
Akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali muhimu ya Shirika la Umeme Nchini, Mhandisi Mramba alisema, “Katika historia ya Sekta ya Umeme, haijawahi kutokea uwekezaji mkubwa kufanyika kwa wakati mmoja kama ilivyo sasa, Miradi yote ya Umeme inayoendelea na ambayo tayari imetengewa fedha ina thamani ya Shilingi Trilioni 3.85, na majadiliano kati ya Serikali na Exim Bank ya mradi wa Dar es Salaam-Arusha wa Shilingi Trilioni 1.5 yakiwa katika hatua za mwisho.” Alifafanua Mhandisi Mramba.
“ Uwekezaji huu unathibitisha kwamba nia ya Serikali ya awamau ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda sio ya maneno matupu bali inaambatana na vitendo kwa uwekezaji madhubuti kwenye umeme.” Alisema.
Mhandisi Mramba alitaja Miradi hiyo mikubwa ya umeme kuwa ni pamoja na ule wa upanuzi wa Kinyerezi I, Kinyerezi II, mradi wa Backbone, Kenya-Tanzania, TEDAP, Makambako-Songea, Uboreshaji umeme jijini Dar es Salaam, City Centre-Dar es Salaam, Electricity V, Bulyanhulu-Geita, Geita Nyakanazi na Rusumo Power Plant (T), miradi yote hii ikiwa na jumla ya thamani ya Shilingi Trilioni 3.85.
Akifafanua zaidi kuhusu uwekezji huo, Mkurugenzi Mtendaji alisema, Miradi yote ambayo thamani yake imetajwa haihusishi Miradi ya usambazaji umeme Vijijini chini ya mpango wa REA.
Akizungumzia utaratibu mpya wa manunuzi,(Procumbent), Mhandisi Mramba alisema, TANESCO imechukua hatua kadhaa ili kuboresha manunuzi ambapo kuanzia sasa makampuni yanayomilikiwa na mtu mmoja kuhodhi manunuzi ya Shirika hilo, na kwamba zabuni zote zilizotangazwa kuanzia mwaka huu wa fedha, haitaruhusiwa kampuni moja kuwa na mikataba miwili kwa wakati mmoja.
Akifafanua zaidi alisema, Katika zabuni moja haitaruhusiwa kampuni moja kupewa zaidi ya Lot 1, “Hii imeanza kusaidia kuondoa ukiritimba katika manunuzi na kuwapa Watanzania wengi zaidi nafasi pana ya kushiriki katika zabuni za kusambaza vifaa vya umeme.” Alifafanua Mhandisi Mramba.
Aidha Mhandisi Mramba alisema, ili kuwezesha Watanzania wengi kushiriki katika uchumi wa nchi, TANESCO itanunua vifaa vya umeme vinavyozalishwa hapa nchini na kuachana na mtindo wa kuagiza kutoka nje.
“Mfano kwa nguzo za umeme tumewapa Sao Hill, ambao watatuuzia nguzo 96,500, na new Forest watatuuzia nguzo za umeme 9,668, na kwa upande wa Transfoma za umeme, kandarasi hiyo imepewa kampuni ya TANELEC itakayotuuzia transfoma 1,500” Alifafanua
Akieleza zaidi kuhusu ununuzi wa vifaa, Mhandisi Mramba alisema, kampuni ya East Africa Cables, intarajiwa kupewa kazi ya kusambaza waya na kuongeza kuwa utaratibu huo pia utatumika kwenye huduma nyingine kama vile Bima, ambapo alisema Shirika linatarajia kulitumia Shirika la Bima la Taifa, (NIC), kutoa huduma hiyo.
Akizungumzia kuhusu hali ya umeme, Mhandisi Mramba aliwahakikishia Watanzania kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Shirika hilo katika kuboresha miundombinu ya umeme, hakutakuwa na mgao wa umeme nchini na ndio maana kwa muda mrefu sasa hakuna mgao wa umeme.“Mwaka 2015 nchi ilikuwa na mgao wa umeme wa jumla ya MW300, na maeneo mengine yalikuwa na hali mbaya hususan Mwanza, Arusha na Kilimanjarolakini kwa sasa hali ya umeme katika mikoa yote na mingine ni nzuri hakuna mgao na kama ikitokea umeme umekatika ni matatizo ya kiufundi katika eneo dogo na kwa muda mfupi.” Alisema.
Hata hivyo alisema Shirika lake linaongeza juhudi za kusambaza umeme kwa watanzania wengi zaidi kote nchini, kutokana na uwekezaji wa miundombinu unaoendela kila kona ya nchi.
Mhandisi Mramba aliwaondoa wasiwasi wananchi kuhusu ombi la Shirika hilo la kuongeza asilimia 18.9 ya bei ya umeme kuanzia Januari mwakani, kwa kusema ongezeko hilo halitaathiri watumiji wa kawaida majumbani. “Tunachoomba kutoka kwa Msimamizi (Regulator), ni kufanya mabadiliko ya kutenganisha watumiaji umeme wa majumbani na wale wanaotumia kibiashara kama vile mabango ya matangazo, kwani hivi sasa wote wanalipa gharama sawa na hili si sawa.” Alisema.
Aliwaasa wananchi kuridhia ongezeko hilo kwani Shirika limo katika jitihada kubwa za kuhakikisha Wananchi wengi zaidi wanapatiwa umeme kwa kufikisha miundombinu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo gharama za kufanya hivyo zimeongezeka.



 Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo
  Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo
 Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Leila Muhaji, (kushoto), akizunguzma jambo

November 23, 2016

Wadau wasifu jitihada za TANESCO kuboresha hali ya upatikanaji umeme wakati majadiliano ya Maombi Ya TANESCO Kupandisha Bei Ya Umeme Jijini Dar Es Salaam.

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini TANESCO, Mhandisi Decklan Mhaiki, akiwasilisha mambi ya TANESCO kupaandishi bei ya umeme kwa asilimia 18.9 wakati wa kikao cha majadiliano baina ya Wadau na Uongozi wa Shirika, kilichoitishwa na Mamlaka ya Udhibiti huduma za Maji na Nishati, (EWURA), na kufanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 23, 2016.
 Baadhi ya Viongozi wa TANESCO na wadau wakifuatilia mjadala


Na HENRY KILASILA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wadau wa umeme kujadili maombi ya Shirika la Umeme Nchini TANESCO ya kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.9 kwa uwazi na bila hofu lakini wakizingatia nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Nchi yenye Uchumi wa Viwanda.
Akifungua majadiliano ya wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam, Zanzibar na Uongozi wa TANESCO Jijini Novemba 23, 2016 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Maji na Nishati, (EWURA), kuhusu mapendekezo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, (pichani juu), ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Paul Makodna alisema, “Rais wetu Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, amedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ambao utafanikiwa tu endapo tutakuwa na umeme wa uhakika na ulio bora.” Alisema.
Aliwataka Wadau kusikiliza kwa makini hoja za TANESCO zinazowasukuma kupandisha bei ya umeme, lakini TANESCO nao wanapaswa kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo yao.
Akiwasilisha mapendekezo ya TANESCO kwa wadau, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Decklan Mhaiki, alisema, Shirika hilo limefikia uamuzi wa kuwasilisha mapendekezo hayo kulingana na mambo matatu ambayo ni Kufua umeme (power generation), Kusambaza umeme (Power distribution), na kusafirisha umeme (Power transmission).
“Kama mjuavyo Shirika limekuwa katika utekelezaji wa Miradi mikubwa ya kuboresha miundombinu ya umeme kote nchini, kwa lengo la kuwapatia wananchi umeme ulio bora na wa uhakika, na kwakweli mabadiliko tayari yameanza kuonekana ambapo hivi sasa kadri siku zinavyokwenda mbele hali ya umeme wetu imekuwa bora zaidi.” Alsiema Mhandisi Mhaiki.
Alisema, bei ya umeme hapa nchini ni ya chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Masharikiambapo alisema, wakati bei ya umeme kwa sasa, hapa Tanzania ni shilingi 242.21, wakati Kenya bei ni Shilingi za Kitanzania, 326 kwa unit, Uganda Shilingi 456 kwa unit, Rwanda Shilingi 438 kwa unit, na Burundi ni Shilingi 195 kwa unit.
“ Hata tukipandisha umeme bado Tanzania bei ya umeme itabaki kuwa chini ukilinganisha na majirani zetu ambapo, tunaomba unit moja ya umeme iuzwe kwa Shilingi 286.28, sawa na ongezeko la asilimia 18.9.” Alifafanua Mhandisi Mhaiki.
Akitoa Hotuba ya ukaribisho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti huduma za Maji na Nishati, (EWURA), Felix Ngamlagosi, alisema, Mamlaka hiyo imepokea maombi ya TANESCO kupandisha umeme kwa mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba 2017, kama ambavyo Sheria inavyotaka.
“Mamombi haya ya TANESCO ni halali yamekidhi Sheria, na niwaombe wadau mtoe maoni ambayo yatasaidia pande zote mbili, TANESCO na watumiaji wa umeme, ili hatimaye wananchi waendelee kupata Huduma bora ya umeme.” Alisema.
Mkurugenzi huyo alisema, tayari Mamlaka yake imekwisha kusanya maoni kutoka kanda wakilishi zote nchini nab ado wanakaribisha maoni zaidi yatumwe kwenye mamlaka yake hadi Novemba 25 mwaka huu saa 11 jioni ambapo dirisha la kupokea maoni litafungwa.
Kwa upande wa watoa maoni, Mwanasheria wa Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO), Abas Juma alsiema, kwa mujibu wa vigezo vilivyopelekea TANESCO kuomba bei ya umeme ipande, ni viwili tu ndio vinaihusu ZECO, ambavyo ni Uzalishaji na Usafirishaji umeme, na kwamba kazi ya kusambaza umeme inafanywa na ZECO yenyewe na kuliomba shirika la umeme TANESCO kuzingatia uhalisia huo na hivyo ZECO haistahili kulipa bei sawa naya wateja wa TANESCO Tanzania bara.
Mwananchi mwingine ambaye ni Mzalishaji umeme kwa kutumia bio-gas, ameipongeza TANESCO kwa kuboresha Huduma zake na kuwataka wadau kulikubali ombi la Shirika hilo ili kuwezesha kasi ya uboreshaji Huduma iweze kusonga mbele.
“Mimi ninaunga mkono maombi ya TANESCO, sisi wazalishaji umeme wadogo, tunashindwa kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ya kuendesha miradi yetu maana mabenki hayana uhakika kama tunaweza kurejesha fedha zao kwa vile bei ndogo ya umeme inayotozwa na TANESCO hailingani na gharama za uendeshaji, hivyo wanahofia wasiweze kupata fedha zao.” Alisema.
Mwananchi mwingine ambaye ni Mfugaji aliipongeza TANESCO kwa kuboresha huduma za umeme na sasa hali ya umeme imeanza kuimarika. “Mimi ni mfugaji miaka miwili iliyopita nililazimika kununua taa za mchina, ili kuhudumia kuku wangu kwa vile umeme wa TANESCO ulikuwa hautabiriki, lakini hivi sasa zile taa sio muhimu tena kwangu kwani umeme unapatikana kwa uhakika lakini sio hivyo tu hata ubora wa umeme wenyewe umekuwa wa kuridhisha sana.” Alisema.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti huduma za Maji na Nishati, (EWURA), Felix Ngamlagosi
 Baadhi ya wajumbe wa bodi ya EWURA
 Baadhi ya wadau na viongozi wa TANESCO
 Baadhi ya wadau kutoka Zanzibar na viongozi wa EWURA

 Mkuu wa Wilaya Hapi, (kushoto) na Ngamlagosi, wakifurahia jambo
 Mdau akitoa maoni yake
 Mdau kutoka ZECO, Abas Jumaa, akitoa maoni ya ZECO


Wadau kutoka Zanzibar

November 22, 2016

BANK OF AFRICA YASAINI MKATABA NA TAASISI YA AFD ILI KUWEZESHA UTOAJI WA MIKOPO YA UWEKEZAJI KATIKA NISHATI MBADALA

Kutoka kushoto ni Bw. Amishadai Owusu-Amoah Mkurugenzi Mtendaji wa BANK OF AFRICA-Tanzania akisaini mkataba na Bw. Bruno Deprince Mkurugenzi wa Kanda wa AFD Afrika Mashariki.

Kutoka kushoto ni Bw. Youssef Benrhafiane Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mikopo na Udhibiti wa BANK OF AFRICA- Tanzania, Bw. Amishadai Owusu- Amoah Mkurugenzi Mtendaji wa BANK OF AFRICA- Tanzania, HE Malika Berak, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Bw. Bruno Deprince Mkurugenzi wa Kanda wa AFD Afrika Mashariki na Bw. Thomas Richard, Mwakilishi wa Shirikisho la viwanda Tanzania.

Tanzania, 22nd Novemba 2016 –Agence Française de Développement (AFD) na BANK OF AFRICA- Tanzania leo wametia saini mkataba wa makubaliano ya kutoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 25.67 kusaidia uwekezaji kwenye nishati mbadala na ufanisi wa nishati.

Makubaliano hayo, yamewezesha upatikanaji wa zaidi ya dola milioni 11.84 kwa ajili ya kukopesha miradi mbalimbali iliyojikita katika nishati mbadala au kuongeza ufanisi wa upatikanaji au matumizi ya nishati hapa nchini kupitia BANK OF AFRICA.

Mkataba huo umesainiwa na ndugu Bruno Deprince ambaye ni Mkurugenzi wa Kanda wa AFD na ndugu Ammishaddai Owusu-Amoah, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa BANK OF AFRICA, mbele ya Mheshimiwa Bi Malika Berak, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mheshimiwa Mikael Melin Programme, Meneja katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania na Mheshimiwa Thomas Richard, Mwakilishi wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI).

Katika makubaliano hayo, taasisi zote mbili zimethibitisha kushirikiana kupitia mpango wa SUNREF (Matumizi Endelevu ya Maliasili na Nishati). Mpango huu bunifu utaiwezesha BANK OF AFRICA kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu itakayowavutia sekta ya umma na binafsi kutekeleza miradi katika nishati mbadala na ufanisi wa nishati, ambayo imekuwa ikipata changamoto katika upatikanaji wa mikopo.

Mpango huu ubunifu itawezesha BANK OF AFRICA kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu klatika viwango vya riba nafuu kulinganisha na viwango vya kawaida vya kibiashara kwa lengo la kuwawezesha wateja katika sekta binafsi na umma, kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutekeleza mpango wa nishati mbadala.

Mikopo hii inaambatana na msaada wa kiufundi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ili kuiunga mkono BANK OF AFRICA lakini pia kuiwezesha benki hiyo kuongeza uwekezaji katika miradi inayochochea ukijani.

Msaada wa kiufundi pia utatoa utaalamu kwa wawekezaji na waendelezaji wa miradi ili kuwajengea uwezo katika kuendeleza nishati mbadala na kuongeza ufanisi katika matumizi ya nishati. Msaada huu utajumuisha maeneo yote ya uwekezaji kama maandalizi ya mradi, mchakato mzima wa uwekezaji pamoja na kujengewa uwezo wa kibenki.

Kwa upande wa Afrika Mashariki, SUNREF, inakuza mpango wa matumizi ya nishati zinazotoa gesi chafu kidogo kwa kugharimia uendelezaji wa miradi ya nishati mbadala na ufanisi katika matumizi ya nishati.

AFD inazisaidia benki za ndani katika kutambua fursa za uwekezaji katika nishati mbadala na kutoa mikopo inayochochea hali ya kijani pamoja na kutengeneza utaratibu mzuri wa ulipaji wa mikopo hiyo unaziofaa pande husika.

Programu hii imeundwa ili kuzisaidia biashara ziweze kutumia fursa ya mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na kuimarisha sekta ya benki kufadhili nishati mbadala na ufanisi wa nishati. Miradi ya nishati mbadala ni ile inayozalisha aina yoyote ya nishati (joto, mvuke, nguvu) bila kutoa nishati yoyote ya mafuta au chanzo chochote cha mionzi, ikiwa ni pamoja na nishati ya upepo na nishati ya jua.

Mradi huu utachangia pia kuongeza ufanisi wa nishati na mchango wa nishati mbadala katika ukuaji wa uchumi nchini,na hivyo kuchangia kupunguza uzalishaji wa gesi ya kaboni. Mradi huu pia utaziwezesha taasisi na biashara za kitanzania kupata teknolojia ya kijani pamoja na kuboresha ufanisi wao na ushindani wa jumla pamoja kuendeleza nishati safi.

Mkakati wa AFD umejikita katika kusaidia maendeleo endelevu ya kimazingira kupitia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kutumia nishati zinazotoa gesi kidogo ya kaboni. Hii ni pamoja na, miongoni mwa mambo mengine, kuboresha ufanisi wa nishati, kupanua matumizi ya vyanzo vya nishati safi, na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

November 16, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA MRADI WA UBORESHAJI HUDUMA ZA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (katikati) na Viongozi wengine kutoka kushoto, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Juliana Palangyo,Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, (Waziri Mkuu), Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland, Kai Mykkanen, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba, wakishangilia baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa kituo cha
cha udhibiti na usimamizi wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar  es salaam kilichoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, leo Novemba 16, 2016

NA Henry Kilasila
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, amezindua kituo cha udhibiti na usimamizi wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar  es salaam kilichoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, leo Novemba 16, 2016.
Kituo hicho kipya na cha kisasa, kimejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Norway na Tanzania, chini ya mpango wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme jijini.
“Serikali ya awamu ya Tano, iliwaahidi Watanzania, wakati tukiomba kura, ya kwamba, tutaboresha huduma ya umeme kote nchini, na leo hii ni ushahidi tosha tunatekeleza kwa vitendo ahadi zetu.” Alisema Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Rais wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli.
Akimkaribisha waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Profesa Sospeter Muhongo amesema, watanzania wanahitaji umeme tena ulio bora, na sasa Kituo hicho ni jawabu la kuwapatia umeme ulio bora.
“Kati ya vitu ambavyo sitarajii kuvisikia ni mgao wa umeme, lakini pia bei ya umeme, kuusu bei tutakaa, pembeni na watu wa TANESCO kulizungumzia hili. “ Alitoa hakikisho Waziri Muhongo.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland, Mh. Kai Mykkanen, alisema, teknolojia iliyotumika kwenye mitambo ya kituo hicho ni ya kisasa ijulikanayo kama Distribution SCADA System, na inauwezo wa kutambua hitilafu ya umeme kwa haraka na hivyo kurahisisha kurekebisha hitilafu hiyo kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema, Mradi wa uboreshaji huduma za umeme jijini Dar es Salaam ulibuniwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya umeme katika jiji la Dar es Salaam kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme katika sekta za kiuchumi hususan katika maeneo ya katikati ya jiji, Kariakoo, Ilala na maeneo ya wilaya ya Kinondoni.
Alisema, utekelezaji wa mradi huu umehusisha ujenzi wa kituo cha kupoza nguvu za umeme chenye ukubwa wa 100MVA (2X50MVA), 132/33KV cha City Centre, ujenzi wa mfumo wa njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi (Underground Transmission Line) na kwa kutumia minara (Overhead Line) ya msongo wa wa kilovolti 132 kutoka kituo cha Ilala hadi kituo cha City Centre umbali wa Kilomita 3.4, vile vile ujenzi wa mfumo wa njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi, (Underground Transmission Line) kutoka kituo cha Makumbusho hadi kituo cha City Centre umbali wa kilomita 6.67.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kituo hiki ambacho kinajulikana kitaalamu kama Distribution SCADA System kitawezaesha watoa huduma wetu kufuatilia kwa haraka zaidi pale matatizo ya umeme yanapojitokeza kwa kutumia mifumo ya ksiasa ya kompyuta.” Alifafanua Mhandisi Mramba na kuongeza.
“Nia hasa ni kujenga vituo vingine kama hiki kwa kuanza na miji mingine mikubwa ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma.” Alisema.


 Waziri Mkuu na wageni wengine wakitembelea chumba cha mitambo yaudhibiti na usimamizi wa mifumo ya usambazaji umeme Distribution SCADA System
 Waziri Mkuu akitembeela moja ya mitambo inayopatikana kwenye kituo chicho (Server)
 Mtaalam wa mitambo, wa shirika la Umeme Nchini Tanzania, (TANESCO), Bi, Mwajua Turkey, kushoto, akimpatia maelezo waziri mkuu wakati akitembelea kituo hicho muda mfupi kabla ya kukizindua rasmi
 Waziri Mkuu akitoa hotuba yake
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akitoa hotuba yake
 Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland, Mh. Kai Mykkanen
 Waziri Mkuu akipokelewa na Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipowasili kwenye hafla hiyo
 Waziri Mkuu akisalimiana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
 Waziri Mkuu akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa
 Waziri Mkuu akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Juliana Palangyo
 Waziri Mkuu akisalimiana na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi
Waziri Mkuu akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba
Waziri Muhongo akizungumza na Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland, Kai Mykkanen
Waziri wa Bishara na Maendeleo wa Finland, Kai Mykkanen, (kushoto) na Balozi wa Finland Nchini, Pekka Hukka, (kulia), wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Juliana Palangyo
Waziri Mkuu, akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi huo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, (wapili kushoto), Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, (wapili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Juliana Palangyo, (kushoto) na Waziri Kai(kulia), wakishangilia baada ya uzinduzi


Meneja wa kituo cha udhibiti na usimamizi wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar  es salaam, Mhandisi Alex P. Kalanje.(mwenye kipaza sauti), akitoa maelezo kwa waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine