May 14, 2020

Serikali yaridhika utekelezaji Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere Mw 2115

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza katika ziara  ya kukagua utekelezaji Mradi wa kufua Umeme kwa Maji wa Julius Nyerere, alipotembelea eneo la ujenzi wa Mradi.




WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Kassim Majaliwa ameridhishwa na hatua mbalimbali za ujenzi wa Mradi mkubwa wa Kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa kwenye mto Rufiji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Mei 14, 2020, baada ya kufanya ziara kwenye eneo la mradi unaotarajiwa kuzalisha jumla ya Megawati 2115“ utakapokamilika 2022.

Waziri Mkuu ambaye alifuatana na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo mhandisi Zena Said watendaji wa TANESCO wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dk.Tito Mwinuka, alisema ziara yake ililenga kupata picha halisi ya hali ya mradi na hatua iliyofikiwa.

“Nimefarijika sana kuona hatua iliyofikiwa toka mradi umeanza mwezi Juni mwaka Jana mpaka leo ni ya kuridhisha.” Alisema Waziri Mkuu.

Alisema ziara yake imempa fursa ya kujionea jinsi kazi zinavyoendelea na nimatumaini yake
utakamilika kwa wakati

“Nimepata fursa ya kuona eneo lote la mradi na kazi mbalimbali zikiendelea, wakandarasi wanafanya vizuri na sisi Kama Serikali kupitia Wizara na TANESCO tumekuwa karibu nao kuhakikisha wanafanya vizuri na hayo ndio matarajio ya watanzania.” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amewahakikishia watanzania kuwa mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa na kuwapongeza wakandarasi kampuni ya Elsewedy na Arab contractor kutoka Misri kwa kazi nzuri.

Alisema licha ya changamoto ya mvua za masika bado kazi ya ujenzi iliendelea.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema, ujenzi ulianza 15/6/2020 na utakamilika 14/6/2022.

“Mradi unashughuli kubwa saba kati ya hizo muhimu sana ni nne, ujenzi wa njia ya kuchepusha maji, kujenga bwawa lenyewe, kujenga kingo nne zitakazowezesha maji kuhifadhiwa na ya mwisho ni kujenga power house.”. alifafanua Dkt. Kalemani.

Dkt.Kalemani alisema Hadi sasa mkandarasi ameshalipwa shilingi trilioni 1.29 ya jumla ya shilingi trilioni 6.5 ya mkataba mzima.

“Malipo hayo ni sawa na asilimia 100 ambayo inahusu malipo ya awali asilimia 15 na malipo ya kazi alizofanya Hadi sasa.” Alifafanua Dkt. Kalemani.