February 14, 2020

Ipigie kura Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweza kushinda kipengele cha *Best Government page of the year* kwa mwaka 2020.

Ipigie kura Shirika  la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweza kushinda kipengele cha *Best Government page of the year* kwa mwaka 2020.

Chakufanya;

1. Fungua hiyo link utakutana na neno Vote chini kabisa ya ukurasa

2. Utakutana na Vipengele vitatu yani *Award Category*, *Sub Category * na *Selection*

3.Kwa upande wa Award Category chagua *DIGITAL GOVERNANCE* na chagua *BEST GOVERNMENT PAGE OF THE YEAR* kwenye kipengele cha Sub Category

4. Kwenye kipengele cha Selection chagua TANESCO

Hatua ya mwisho wameandika *VOTE NOW* ! Bonyeza hapo na utakua umefanikiwa kupiga kura yako. Asanteni sana na tunaomba ushirikiano wako!


https://www.digitalawards.co.tz


February 10, 2020

TAARIFA KWA UMMA: TAHADHARI KWA WANANCHI WANAOISHI PEMBEZONI MWA MKONDO WA MAJI YATOKAYO KWENYE VYANZO VYA KUFUA UMEME KWA MAJI VYA MTERA NA KIDATU



MKURUGENZI MTENDAJI TANESCO, DKT. TITO MWINUKA


TAARIFA KWA UMMA:


FEBRUARI 10, 2020

      
TAHADHARI KWA WANANCHI WANAOISHI PEMBEZONI MWA MKONDO WA MAJI YATOKAYO KWENYE VYANZO VYA KUFUA UMEME KWA MAJI VYA MTERA NA KIDATU


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatoa tahadhari kwa Wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mkondo wa maji yatokayo katika mabwawa ya kufua umeme kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuwa mvua bado zinaendelea na zipo juu ya wastani, TANESCO inafanya tathmini iwapo siku za usoni maji yahamie upande wa pili kwa ajili ya usalama wa Mabwawa na Mitambo.
TANESCO inatoa tahadhari hii muhimu kwa Wananchi hususani wale wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile Uvuvi, kulisha Mifugo, Kilimo na shughuli nyingine kwenye mkondo wa mto, vidimbwi au pembezoni mwa bwawa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu, kijamii na kiuchumi kwa kipindi hiki ambacho mvua za Vuli zikiwa zinaendelea kunyesha.

Hali ya Ufuaji umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu unaendelea vizuri kwa asilimia mia moja (100%) na kiwango cha maji kimeongezeka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kuanzia mita 691.22 juu ya usawa wa bahari kuanzia Desemba 01, 2019 hadi kufikia mita 698.40 juu ya usawa wa bahari Februari 10, 2020 katika bwawa la Mtera.
Shirika litaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi wote waishio maeneo ya pembezoni mwa mkondo wa maji na mabwawa ya Mtera na Kidatu kwa  ushirikiano na Viongozi wa Wananchi wa maeneo hayo.

TANESCO itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kadri hali ya mvua itakavyokuwa inaendelea.




Imetolewa na:  Ofisi ya Uhusiano
                          TANESCO-Makao Makuu


                                

February 7, 2020

WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI - TANESCO



Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa tahadhari kwa Wananchi wa Vijiji jirani na vyanzo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini(TMA) kuwa mvua bado zinaendelea kunyesha na zipo juu ya wastani.

Kufuatia taarifa hiyo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, Meneja Mwandamizi Uzalishaji Umeme Mhandisi John Skauki amesema wataalamu wa TANESCO wanafanya tathmini iwapo siku za usoni maji yahamie upande wa pili kwa ajili ya usalama wa Bwawa na mitambo.

Alisema Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza maji hayatakuwa yanasambaa bali yatapita kwenye mkondo wake wa asili ambako wananchi wanafanya shughuli zao za kijamii.

"TANESCO tumeona ni muhimu leo kutoa tahadhari kwa Wananchi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kwa kawaida Bwawa la Mtera kulijaza huchukua miezi 3 hadi 4 kwa mvua za masika, lakini kwa kipindi hiki mvua za vuli zimekuwa nyingi ndani ya mwezi mmoja kina kimeongezeka", alisema Mhandisi Skauki.

Alisema tahadhari inatolewa kwa Wananchi kusitisha shughuli zao za kijamii kama uvuvi, kulisha mifugo, kilimo na nyingine kwenye mkondo wa maji au sehemu zenye vidimbwi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Aliongeza kuwa, kawaida kina cha maji kujaa ni mita 698.50 juu ya usawa bahari na kuongeza hivi sasa kina cha maji kimefikia 698.03 juu ya usawa wa bahari.

"Ikitulazimu tutaruhusu maji kwenda upande wa pili, hili ni zoezi la kawaida na halina madhara yoyote kwa jamii, mara ya mwisho maji kuzidi kiwango ilikuwa mwaka 2008 zoezi lilifanyika na hakukuwa na madhara yoyote kwani maji hupita kwenye mkondo wake wa asili", alisisitiza Mhandisi Skauki.

Aidha, maji yatakapofika kina cha mwisho TANESCO itatolea taarifa aliongeza.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Uhusiano Bi. Leila Muhaji akizungumzia jinsi ambavyo jamii inayoishi kandokando na vyanzo vya maji inahusishwa alisema, TANESCO imekuwa ikitoa elimu kwa Wananchi hao, lakini pia kushirikiana na viongozi wa Vijiji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, Maafisa wa Uvuvi.

"Tumefika hapa kuwatoa hofu Wananchi na hii tunayotoa ni tahadhari  tuu kwa Wananchi", alisema Bi. Muhaji.

Afisa Mtendaji Kata ya Mtera Bi. Naomi Fungulia alisema siku zote wamekuwa wakishirikiana na TANESCO na wamekuwa wakitoa tahadhari kwa wananchi kupitia vikao mbalimbali wanavyovifanya.

Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1988 na limekuwa likitumika kwenye uzalishaji wa umeme kwa vituo viwili vya Mtera megawati 80 na Kidatu megawati 201.

Vyanzo vya maji vya bwawa la Mtera ni vitatu ambavyo ni Mto wa Ruaha Mkuu, Ruaha Mdogo ambvyo vipo Mkoani Iringa na Mto Kisigo unaopata maji kutokea Mikoa ya Singida na Dodoma.

Kwa hivi sasa bwawa la Mtera ndio bwawa kubwa na linachangia takribani asilimia 30 ya umeme kwenye gridi ya Taifa.

Aidha, inatarajiwa maji ya Mtera pia yatachangia kwenye ufuaji wa umeme bwawa la Nyerere kupitia mto Kilombero, bwawa la Julius Nyerere litakuwa na uwezo wa kufua megawati 2115 za umeme.