October 27, 2017

KUKATIKA KWA UMEME NCHI NZIMA: DKT. KALEMANI AWAOMBA RADHI WANANCHI.


WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (pichani juu), amewaomba radhi Wananchi kufuatia kukatika kwa umeme nchi nzima Oktoba 25 na 26, 2017 kulikosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa.

Dkt. Kalemani ambaye alikuwa mjini Dodoma akishiriki vikao vya kamati za Bunge, alilazimika kusafiri mapema jana Asubuhi Oktoba 26, 2017 kuja jijini Dar es Salaam ili kufuatilia juhudi za kurekebisha tatizo hilo.

"Ndugu Wananchi hali ilivyotokea sisi kama Shirika la TANESCO na Serikali tunawaomba radhi kwa matatizo yaliyotokea, lakini niseme tu kwamba kuna hatua madhubuti zinazochukuliwa hivi sasa kurekebisha hali hiyo ili Wananchi muendelee kupata umeme wa uhakika." Alisema Dkt. Kalemani katika taarifa yake kwa Wananchi aliyoitoa Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam baada ya ziara yake ya kutembelea kituo cha udhibiti cha Gridi ya Taifa, (GCC), kilichoko Ubungo na kituo cha kufua umeme wa gesi cha Kinyerezi1 jijini Dar es Salaam.

Taarifa za awali zilieleza kuwa kukatika kwa umeme kulisababishwa na "Gridi kuchomoka" Oktoba 25, 2017 majira ya saa 10;08 alfajiri na kurejea saa 12:09 Asubuhi ambapo umeme ulirejea Mikoa yote isipokuwa Zanzibar, ingawa juhudi za mafundi wa TANESCO ziliwezesha umeme kurejea Zanzibar majira ya saa 1 asubuhi.
Hata hivyo tatizo hilo lilirejea tena majira ya saa 12:30 jioni siku hiyo hiyo ya Oktoba 25, 2017, ambapo takriban Mikoa yote iliathirika. Umeme ulirejea tena majira ya saa 3 usiku lakiji ilipofika Oktoba 26, 2017 majira ya saa 12:03 tatizo hilo likajirudia tena na kuathiri takribani Mikoa yote ikiwemo Zanzibar.

"Nimekuja kutoka Dodoma ili kuona nini kimetokea, nini kimesababisha na hatua gani za haraka zinachukuliwa ili kuondoa tatizo hilo, hii ndio hasa dhamira ya safari yangu." Alisema Dkt. Kalemani baada ya kufika kwenye kituo cha udhibiti Gridi ya Taifa, Ubunmgo.

Lakini niwapongeze TANESCO kwa kutoa taarifa mapema kwa Wananchi kuwajulisha kuhusu tatizo hilo, alisema.
Akifafanua zaidi Dkt. Kalemani alisema, chanzo cha tatizo ni pamoja na mfumo wenyewe (GCC) na bado unafanyiwa marekebisho na taratibu zinaendelea, na kule Kinyerezi kuna mashine moja haifanyi kazi nayo inafanyiwa marekebisho ikiwa ni pamoja na Valvu moja iliyoharibika nayo pia inafabnyiwa kazi.

"Gridi ya Taifa imerejea tangu usiku wa Oktoba 25, na umeme unapatikana nchi nzima lakini hata hivyo yapo maeneo machache ambayo hayapati umeme wa kutosha kwa sababu mtambo mmoja wa Ubungo namba mbili wenye jumla ya megawati 129 haujaanza kufanya kazi na nimeelekeza wataalamu wafanye kazi usiku na mchana na wamenihakikishia kufikia saa 5 asubuhi kesho (Oktoka 27), mtambo huo utaanza kufanya kazi na umeme utarejea katika hali yake ya kawaida." Alibainisha.

Dkt. Kalemani akiwa kwenye kituo cha udhibiti wa Gridi ya Taifa (GCC), Ubungo jijini Dar es Salaam
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia uzalishaji (Generation), Mhandisi Abdallah Ikwasa, (kushoto), akimpatia maelezo Waziri Dkt. Kalemani alipotembelea mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi 1 jijini Oktoba 26, 2017. Wakzanza kulia ni NJaibu Katibu Mkuu Nishati, Dkt. Juliana Palagyo
Meneja Mwandamizi wa TANESCO, anayeshughulikia uzalishaji, Mhandisi Costa Rubagumya akifafanua jambo.
Meneja wa udhibiti ifumo ya Gridi ya Taifa (Protection), Mhandisi Izahaki Mosha, akimfafanulia Waziri Dkt. Kalemani (kushoto).
Dkt. Kalemani (kushoto), akiwa kwenye chumba cha udhibiti cha Kinyerezi 1 akifafanua jambo.

October 16, 2017

TATIZO LA UMEME MTWARA NA LINDI KUPATIWA UFUMBUZI KATIKA KIPINJDI CHA SIKU 10: WAZIRI DKT.KALEMANI
Waziri wa Nishati Dkt. Medardi Kalemani, akizungumza baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme mkoani Mtawara leo Oktoba 16, 2017 ili kujionea kazi inayofanywa na mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO) kurekebisha mashine 8 kati ya tisa zilizoharibika. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda, na kulia ni Kamu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka.

 NA K-VIS BLOG/Mtwara
Serikali imewaomba wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kuwa na subira, katika kipind hiki ambapo upatikanaji wa umeme kwenye mikoa hiyo umeathirika baada ya mashine 5 kati ya 9 za kufua umeme (turbines) kuharibika.

Hata hivyo Mafundui wa TANESCO wamekuwa katika juhudi kubwa za kuzifanyia matengenezo mashine hizo, zilizofungwa miaka 10 iliyopita.

"tayari tumeagiza vipuri kwa ajili ya kutengeneza mashine hizo ambazo kwa ujumla wake huzalisha Megawati 18 za umeme, ambazo zitawasili ndani ya siku 7 ili kuweza kuondoa tatizo la kuzimika umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara." Alisema Dkt. Kalemani.

Alisema, baada ya kwasili kwa vipuri hivyo, kazi ya kuzifanyia matengenezo itaendelea na amememuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, kuleta wataalamu wote wa TANESCO popote walipo nchini, wafika Mtwara na kuungana na wataalamu waliopo ili kazi ya kuzitengeneza mashine hizo iende kwa kasi.

Kati ya mshine 9 ni mashine nne tu zinazotoa Megawati 8 ndio zinafanya kazi, hali inayosababisha kuwepo kwa mgao wa umeme unaofikia hadi masaa 8 kwa siku.

 Dkt. Kalemani ambaye amewasili mkoani Mtwara leo Oktoba 16, 2017 ili kujionea juhudi za Mafundi wa TANESCO  za kurejesha upatikanaji wa umeme katika hali yake ya kawaida amesema vipuri hivyo vifungwe kwa muda wa siku tatu badala ya wiki 3na kwamba ndani ya siku 10 umeme utakuwa katika hali yake ya kawaida.

Mkoa wa Mtawara na Lindi unategemea mashine hizo zinazozalisha umeme unaotumia gesi asilia.
Ukiachilia mbali kuharibika kwa mashine hizo, miundombinu mingine ya umeme kwenye mikoa hiyo iko salama na katika ubora wa hali ya juu ambapo vituo vipya vya kupoza na kusambaza umeme wa 132kV hapo hapo mkoani Mtwara na kingine huko Mahumbika mkoani Lindi vinafanya kazi pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (transmission lines), nao uko katika hali bora.

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (wapili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Evod Mmanda, (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt,. Tito Mwinuka, wakitembelea kituo cha kufua umeme mkoani Mtwara leo Oktoba 16, 2017.
 Waziri wa Nishati Dkt. Medardi Kalemani, akizungumza baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme mkoani Mtawara leo Oktoba 16, 2017 ili kujionea kazi inayofanywa na mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO) kurekebisha mashine 8 kati ya tisa zilizoharibika
 Fundi wa TANESCO, akitengeneza moja ya mashine zilizoharibika kwenye kituo cha kufua umeme mkoani Mtwara.
  Fundi wa TANESCO, akitengeneza moja ya mashine zilizoharibika kwenye kituo cha kufua umeme mkoani Mtwara.
 Fundi wa TANESCO, akichukua spana ili kuendelea na kazi.
 Hii ni moja kati ya mashine zizlizoharibika.

October 15, 2017

Wahandisi Wa TANESCO Wapambana usiku na mchana kurejesha umeme katika hali yake ya kawaida Mikoa ya Mtwara na Lindi
 WAHANDISI na Mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wanapambana usiku na mchana kuzifanyia matengenezo mashine za kufua umeme, ili kuondoa tatizo la kukosekana kwa umeme kwa vipindi virefu kila siku kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi.
 Akizungumza mjini Mtwara Oktoba 14, 2017, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Kaitwa Bashaija, amesema kwa sasa Wahandisi na Mafundi wa TANESCO wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana ili kutengeneza mitambo ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Baadhi ya Wananchi wameshuhudia mafundi hao wakifanyakazi ya kurekebisha mitambo hiyo katika Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia Mkoani Mtwara.
“Mitambo hii ina kiasi cha mika 10 tangu ifungwe, na kadiri miaka inavyokweda ndivyo ongezeko la uhitaji wa umeme hususan Mkoani Mtwara linazidi kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi,” Alisema Mhandisi Bashaija.

Aliongeza, miaka michache iliyopita baadhi ya mitambo iliweza kuzimwa na bado hali ya umeme ilikuwa imara.
Wiki iliyopita Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliagiza TANESCO kufanya juhudi za ziada kuhakikisha tatizo la umeme mkoani Mtwara na Lindi linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kutokana na hali hiyo Mhandisi Bashaija, alisema kuwa kwa sasa TANESCO winamipango ya muda mfupi na mrefu katika kuhakikisha miundombinu ya umeme katika Mikoa ya kusini inaimarika.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia gesi asilia cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba, alisema licha ya changamoto hiyo kwa sasa bado mitambo iliyopo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme katika Mikoa hiyo.
“Pamoja na hali hii lakini kwa sasa tunakwenda vizuri kiasi ila si sana maana umeme kuna wakati unarudi na kukatika. Na tunaamini tutafanikiwa kurudi katika hali ya kawaida na kikubwa tunawaomba Wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kutuvumilia kwani nasi tunajua umuhimu wa umeme katika shughuli za uzalishaji.” Alitoa rai Mhandisi Chinumba.


October 2, 2017

Dkt. Kalemani afanya ziara Miradi ya Uboreshaji Miundombinu ya Umeme Mkoa wa Ilala


Na Henry Kilasila


Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Matogolo Kalemani, amekagua Miradi ya uboreshaji wa Miundombini ya Umeme Jijini Dar es Salaam, inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Ilala, City Center, Muhimbili, Masaki na Msasani iwapo vimekamilika na vinafanya kazi vizuri, ambapo aliridhishwa na vituo hivyo.

Aidha, Dkt. Kalemani aliipongeza Menejimenti ya TANESCO, Uongozi wa Kanda, Mkoa na Wafanyakazi kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo, Chuo cha Muhimbili na Hospitali ya Mwananyamala ambapo kila moja imejengewa njia ya umeme ya msongo wa Kilovolti 11 hivyo kuondoa matatizo ya umeme katika maeneo hayo.

“Mahitaji ya Muhimbili ni Megawati 4 wakati kituo cha Muhimbili kinamegawati 12, mahitaji ya Hospitali ya Mwananyamala ni Megawati 1.5 wakati kituo kina Megawati 12, hivyo sitegemei kusikia umeme umekatika katika maeneo haya”. Alisema Dkt. Kalemani na kuutaka Uongozi wa TANESCO kuvisimamia vizuri vituo hivyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugrnzi Mtendaji TANESCO Dkt. Tito E. Mwinuka alisema, Serikali iliona uwepo mkubwa wa mahitaji ya umeme, hivyo kupitia TANESCO iliamua kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuviongezea uwezo Vituo vya kupoza na kusambaza umeme, uboreshaji wa vyumba vya kuendeshea mitambo pamoja na uboreshaji wa njia za kusafirisha umeme. 

“TANESCO tunafanya jitihada za kuendelea kukamilisha Miradi ambayo haijakamilika ya Mbagala na Kurasini, kwani Miradi hiyo ikikamilika maeneo ya Kigamboni yatapata umeme wa uhakika hivyo mji wote wa Dar es Salaam kuwa na umeme wa uhakika.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri pia alitembelea Chuo cha Ufundi TANESCO cha Masaki eneo ambalo Wanafunzi wanafanya Mafunzo kwa vitendo na kutoa pongezi kwa TANESCO na kuutaka Uongozi kuongeza idadi ya Wanachuo.

Serikali kupitia TANESCO imeendelea na uboreshaji wa Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala kimeongezwa uwezo kutoka MVA 210 hadi MVA 240, ujenzi wa chumba kipya cha kuongezea mitambo na kujenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 132 kutoka Ubungo hadi Ilala.

Pia ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme kupitia chini ya ardhi ya msongo wa Kilovolti 33 katika Vituo vya City Center, Sokoine, Railway na Kariakoo.