August 28, 2020

TANESCO yaunda kikosi kazi kupambana na wizi wa Umeme


 

Na Grace Kisyombe
Dar es salam.

Bodi ya Wakurugenzi  ya TANESCO imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kupambana na wizi  pamoja na hujuma katika miundombinu ya umeme.

Akizungunza katika mkutano na  Waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander L. Kyaruzi  amesema Bodi ya Wakurugenzi kupitia kamati zake imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kupambana na hujuma katika miundombinu ya umeme,

“Baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika kampeni maalum ya kukamata wahujumu miundombinu ya umeme ni, Jeshi la Polisi, Takukuru, Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa Serikali (DPP), Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na wataalam wengine kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati” Amesema Dkt. Kyaruzi

Dkt Kyaruzi aliongeza kusema kuwa, kikosi kazi hicho kitakuwa na jukumu la kukamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanao jihusisha na wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya umeme.

Kikosi kazi hicho kimeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Dar e salam, ambapo tayari watuhumiwa wanne wamekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi.

Katika hatua nyingine Dkt. Kyaruzi amewaomba wananchi na wasamaria wema kushiriki katika kampeni hii kwa kutoa taarifa za siri ambazo zitafanikisha kuwakamata wananchi wanao hujumu miundmbinu ya umeme.

Dkt Kyaruzi amesema kuwa kutakuwa na zawadi ambazo zitakuwa zikitolewa kwa wale wote watakao fanikisha kukamatwa kwa watu wanao hujumu  miundombinu ya umeme.

Zawadi hizi ni za fedha tasilimu na kiwango cha zawadi hizi kitategemea ukubwa wa mali iliyo kamatwa au kuokolewa kutoka katika hujuma hizo.

Aidha, Dkt. Kyaruzi amewakumbusha wananchi wote wenye madeni ya umeme kulipa madeni hayo haraka kwani muda wa siku 14 ulio tolewa na Mhe Waziri wa Nishati unakaribia kwisha, hivyo basi kuanzia  Septemba 1, 2020 TANESCO itakata umeme kwa kila anaye daiwa, zoezi hili litahusu taasisi, wafanyabiashara na watu binafsi wanao daiwa.




 

August 27, 2020

Wafanyabiashara wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa uhujumu uchumi

 


Wafanyabiashara wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya mahakimu wawili tofauti wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuingilia miundombinu ya TANESCO na kujiunganishia umeme kinyume na utaratibu.

Washitakiwa hao ni Ahmed Khalifa, mkazi wa Mikocheni, Abdulrazak Said na Anuary Amdani, ambao wote ni wakazi wa Temeke na Joseph Mwakabanga, mkazi wa Tandale kwa Tumbo,

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Kassian Matembele, upande wa mashitaka ulidai mnamo Julai 29, 2020 Mikocheni, Mtaa wa Ndovu Wilayani Kinondoni, washtakiwa kwa pamoja, Khalfan na Said waliingilia kwa makusudi miundombinu ya TANESCO.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujiunganisha umeme kupitia mfumo wa TANESCO na kukwepa kutumia mita, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Aidha, mnamo Agosti 7, 2020 katika Mtaa wa Magomeni Mikumi Wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, Amdani na Mwakabanga waliingilia kwa makusudi na kinyume cha sheria miundombinu ya TANESCO iliyokusudiwa kutumiwa kusambaza huduma ya umeme.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa washitakiwa hao walibadilisha mita, mali ya TANESCO kutoka kwenye nyumba inayomilikiwa na Amdani yenye deni ya shilingi 3,521,587.70 na kuweka mita mpya kwa lengo la kukwepa deni lililotajwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu mashitaka yao kwa vile mashiataka yao yanaangukia kwenye sheria ya uhujumu uchumi.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mawakili Waandamizi wa Serikali Mantenus Marandu and Wankyo Simon pamoja na Wakili wa Serikali Benson Mwaitenda umedai upelelezi wa mashauri yote mawili haujakamilika.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, Mahakimu katika kesi zote mbili walitoa dhamana kwa washitakiwa kwa kuzingatia masharti mbalimbali.

Khalfan na Said walipewa masharti ya kupata wadhamani wawili kila mmoja ambaye angeweka dhamana ya shilingi milioni 5 na Kila mdhamini alitakiwa awe na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake, kuwasilisha vitambulisho vyao, ambayo ni, kadi ya kitambulisho cha Taifa au Kadi ya kupigia kura.

Washtakiwa pia walizuiliwa kuondoka nchini bila kupata ruhusa ya Mahakama.

Kwa upande wa Amdani na Mwakabanga, hakimu aliwapa dhamana kwa masharti ya kupata wadhamini wawili kila mmoja ambaye atasaini dhamana ya 500,000 / na walitakiwa kuwasilisha vitambulisho vyao.

Kesi zote ziliahirishwa hadi Septemba 10, 2020.
 


 

Kampeni ya "PETA" yatatua kero za umeme Mkoani Tanga.

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Tanga hivi karibuni limezindua Kampeni ya "PETA" lengo likiwa ni kutoa elimu ya huduma zote zitolewazo na TANESCO ikiwemo kutatua kero mbalimbali za umeme kwa wananchi.

Akizindua kampeni ya PETA Kaimu Meneja Mkoa wa Tanga Mhandisi Bakari Kalulu akiambatana na wakuu wa Idara za TANESCO Mkoa wa Tanga ili kupokea Kero za Wananchi na kuzitolea majibu yake.


Mhandisi, Kalulu alisema baadhi ya Wateja wa TANESCO wanatumia umeme kwa ajili ya kufukuza giza yaani kwa ajili ya Taa tu, PETA imekuja na majibu ya kuwahamasisha wateja waache fikra hizo na kufikiri namna nzuri ya kutumia umeme kukuza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.

Akiielezea Kampeni hiyo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Tanga, Bw. Amon Bandiwe alisema PETA ni kifupi cha maneno P =Pata , E =Elimu ya matumizi Bora ya umeme, T =Toa kero yako, A = Acha kuhujumu miundombinu.

Aliongeza, kampeni ya PETA itasaidia TANESCO kufikia malengo ya utoaji wa huduma ya umeme kwa Wateja na ni chachu ya kubadili fikra za Wateja kwa kutumia nishati ya umeme kukuza vipato vyao.

Kampeni hii ni suluhisho la changamoto zote za kero zinazotokana na huduma ya umeme Mkoani Tanga.

Wakazi wa Mkoa wa Tanga wameipongeza TANESCO kwa kuzindua kampeni ya PETA kampeni ambayo itaisaidia TANESCO Mkoa wa Tanga kuboresha huduma zake kwa Mkoa na Wilaya.

Aidha, Jumla ya kero 21 zilipokelewa na kujibiwa na wakuu wa Idara papo kwa papo.