March 26, 2019

"Tumieni wazawa kutekeleza Miradi ya REA", Dkt. Kalemani



Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu  (REA) kutumia Wazawa wanapokuwa wakitekeleza miradi hiyo.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Rugunga , Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma.

Aliongeza, Wananchi wanauwezo wa kufanya kazi  katika Miradi ya REA kwani kuna kazi ambazo hazihitaji ujuzi wowote, akitolea mfano kazi za kubeba Nguzo.

“Mkandarasi  usije hapa na vibarua, vibarua wanapatikana hapa hapa, kunavijana wengi na wanawezaa kufanya kazi, chukua vijana hapa, uwalipe ujira wao, na kazi ifanyike haraka bila kupoteza muda “, alisema Dkt. Kalemani.

Aidha, ameiagiza TANESCO kuanzisha Ofisi Vijijini ili kuepusha usumbufu kwa Wananchi kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kilipia huduma ya umeme.

“TANESCO anzisheni  Ofisi ndogondogo hapa kijijini, iwe ni chumba cha shule , iwe ni chini
ya mti, vyovyote vile lakini Wananchi walipie huduma ya umeme hapahapa Vijijini “, alisema Dkt.Kalemani.

Katika ziara yake, Dkt. Kalemani aliwasisitiza Wananchi kuchangamkia fursa ya umeme, na kwa kulipia kiasi cha shilingi elfu 27.

Aidha, alisisitiza kuwa umeme utafika kitongoji kwa kitongoji, nyumba kwa nyumba na Kaya kwa kaya, ili kuhakikisha Wananchi wote wa Rugunga, Vitongoji vyake 10 na vijiji vyote 37 vya Wilayani Kibondo vinapata hadi kufikia mwezi June 2019 vinapata huduma ya umeme.












Matengenezo kituo cha Ubungo II yameendelea

Machi 26, 2019



Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawataarifu Wateja wake wa Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar kuwa matengenezo kinga ya mashine namba 3 ya Kituo cha Ubungo II yanaendelea

Aidha, Kampuni ya Songas imeanza matengenezo makubwa yanayoenda sambamba na kubadilisha "engine" ya mashine namba 3 baada ya muda wake kuisha kuanzia tarehe Machi 25, 2019 na yanayotarajiwa kukamilika Aprili 09, 2019.

Kutokana na matengenezo hayo  baadhi ya maeneo ya Mikoa ya TANESCO ya Dar es Salaam ambayo ni Kinondoni Kaskazini, Kinondoni Kusini, Temeke na Ilala pamoja na Zanzibar yatakuwa na upungufu wa umeme na hivyo kuathiri maeneo hayo kwa nyakati tofauti.

TANESCO itaendelea kutoa taarifa ya Maendeleo ya kazi ya matengenezo ya kituo cha Ubungo yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Dar es Salaam na Zanzibar kwa siku zijazo.

Kituo cha miito ya simu 2194400 na 0768 985100

Tovuti: www.tanesco.co.tz,

*Mitandao ya kijamii*

Twitter, www.twitter.com/tanescoyetu,

 Facebook https://www.facebook.com/tanescoyetultd/

*IMETOLEWA NA:*

OFISI YA UHUSIANO

TANESCO MAKAO MAKUU

March 5, 2019

KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAFANYA ZIARA KATIKA KIWANDA CHA TANELEC



Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene leo wametembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha ili kukagua masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wa uzalishaji wa transfoma.

Katika ziara hiyo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kukagua shughuli za uzalishaji wa transfoma katika Kiwanda hicho, Wajumbe hao kwa nyakati tofauti waliowapongeza watendaji wa Kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma nyingi ambazo ni 14,000  kwa mwaka huku mahitaji ya transfoma kwa mwaka yakiwa ni 10,000.

Aidha Wajumbe hao wamepongeza uamuzi wa Serikali wa mwaka 2017 ambao ulielekeza kuwa miradi yote ya umeme nchini itumie vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini hali inayopelekea miradi hiyo kufanyika kwa kasi.

Wajumbe hao pia wamemtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kwa kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.

Alitoa mfano kuwa upatikanaji wa transfoma nje ya nchi unaweza kuchukua hadi miezi 12 wakati transfoma zinazozalishwa ndani ya nchi zinachukua muda mfupi kufika katika eneo zinapohitajika.

Aidha Waziri wa Nishati alisema kuwa uagizaji wa transfoma nje ya nchi ni gharama kubwa kwani transfoma moja kutoka nje ya nchi inauzwa kwa takriban shilingi milioni Tisa wakati zinazozalishwa nchini ni takriban shilingi milioni 6.5.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TANELEC, Zahir Saleh alisema kuwa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1981 kwa sasa kinazalisha transfoma kiasi cha 14,000 kwa mwaka.

Alisema kuwa,  kiwanda kinazalisha transfoma za uwezo wa kvA 50 hadi kVA 5000 na kufanya matengenezo ya transfoma kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi na Kenya.

Aliongeza kuwa, uamuzi wa Serikali kuzuia kuagiza vifaa nje ya nchi umekinufaisha kiwanda hicho kwani kabla ya uamuzi walikuwa wakizalisha transfoma 7000 kwa mwaka lakini sasa wanazalisha transfoma 14,000.

Kuhusu ajira alisema kuwa, awali waliajiri wafanyakazi 30 lakini kwa sasa wafanyakazi walioajiriwa ni 70 na kwa mwaka huu wataajiri wafanyakazi wengine 40.

Vilevile alisema kuwa kutokana na uamuzi huo wa Serikali, Kiwanda kinafanya kazi kwa faida na wameanza kupeleka gawio serikalini la takribani shilingi milioni 500 kwa mwaka 2018 na wanategemea kuongeza kiasi cha gawio hilo kwa miaka inayokuja.


March 4, 2019

Wajumbe wa Bodi ya TANESCO Waridhishwa na jitihada za Wataalamu wa TANESCO

Bodi ya Shirika la Umeme Nchini TANESCO ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Alexander Kyaruzi Machi 2, 2019 imetembelea eneo la mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Kurasini jijini Dar es Saam ili kijionea hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Kituo cha Kurasini ni moja ya vituo vitano vilivyojengwa jijini Dar es Salaam chini ya mradi wa kuboresha na kuimarisha miundombinu ya umeme yaani Tanzania Energy Development Access Project –TEDAP ambapo vituo vingine vinne tayari vimekwishaanza kazi na hiki cha Kurasini ujenzi wake unakamilika mwezi huu wa Machi, Meneja Mwandamizi wa TANESCO anayeshughulikia miradi, Mhandisi Emmanuel Manirabona amemueleza Mwenyekiti huyo wa bodi na ujumbe wake.
Mwenyekiti huyo wa bodi ambaye alifuatana na baadhi ya wajumbe wa bodi Dkt. Lugano Wilson, Balozi Dkt. James Nzagi na Bw. David Alal, alisema “Tumeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu, mradi unatia moyo kama ujuavyo mradi huu umeanza muda mrefu kama mlivyoelezwa na meneja mwandamizi wa miradi, lengo la mradi huu lilikuwa ni kuboresha na kuimarisha miundombinu ya umeme mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjarop na Arusha sehemu zingine tayari mradi umekamilika kipande kilichobaki ni hiki tu cha Kigamboni.” Alisema Dkt. Kyaruzi.
Akifafanua zaidi alisema, Dar es Salaam ilikuwa imebaki Kurasini, kuja Kigamboni na kwenda Mbagala na kama unavyoona wakandarasi wako kazini wanaendelea kuvuta waya ili Mbagala, Kigamboni na Kurasini viunganishwe na baada ya kuunganishwa kingine kitakachofanyika kutakuwa na laini (njia) ya pili ya msongo wa kilovolti 33, kwa sasa laini ya kwenda Kigamboni ni moja na tayari imeshajaa na tukiweka hii ya pili ambayo itakatisha bahari kwenye Mkondo wa Kurasini (Kurasini Creek) itakuwa imeongeza uwezo mara mbili, Alisema.
“Juhudi hizi zitawapa watu wa Kigamboni umeme Murua zaidi na katika kipindi kifupi kijacho Kgamboni mambo ya umeme yatakuwa mazuri sana.” Alitoa hakikisho Dkt. Kyaruzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Shirika la Umeme Nchini TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi, (katikati), akiwa na baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo kutoka kulia, Balozi Dkt.James Nzagi, Dkt.Lugano Wilson, na Bw. David Alal, akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotembelea eneo la utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya umeme eneo la upande Kigamboni jijini Dar es Salaam leo Machi 2, 2019.
Meneja Mwandamizi wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO, anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, akieleza juu ya utekelezaji wa mradi huo.
Dkt. Kyaruzi (wakwanza kulia) na baadhi ya wajumbe w abode akiwemo Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jafari Mpina (watatu kulia), wakiangalia kazi ya kuvuta nyaya za umeme upande wa pili wa mkondo wa Kurasini (Kurasini Creek) jijini Dar es Salaam Machi 2, 2019.
Dkt. Kyaruzi akizungumza na waandishi wa habari

Dkt. Lugano Wilson, Mjumbe Bodi ya wakurugenzi Shirika la Umeme Nchini TANESCO.
Balozi Dkt. James Nzagi, Mjumbe Bodi ya wakurugenzi Shirika la Umeme Nchini TANESCO.
Bw.David Alal, (wakwanza kushoto) Mjumbe Bodi ya wakurugenzi Shirika la Umeme Nchini TANESCO.
Mafundin wakiendelea na kazi ya kuvuta nyaya za umeme kutoka Kurasini kwenda upande wa pili wa mkondo wa Kurasini Machi 2, 2019.
Mafundin wakiendelea na kazi ya kuvuta nyaya za umeme kutoka Kurasini kwenda upande wa pili wa mkondo wa Kurasini Machi 2, 2019.
Meneja Mwandamizi wa TANESCO anayeshughulikia miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, akitoa ufafanuazi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wakati wa ziara ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Machi 2, 2019.
Meneja Mwandamizi wa TANESCO anayeshughulikia miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, akitoa ufafanuazi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wakati wa ziara ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Machi 2, 2019.