October 31, 2018

KATIBU MKUU NISHATI AITAKA TANESCO KUBORESHA ZAIDI UTENDAJI




Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Hamisi Mwinyimvua amepongeza utendaji kazi wa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuwataka kuongeza jitihada zaidi, hususan katika ukusanyaji wa mapato.

Ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2018 jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano wa 48 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TANESCO.

Akifafanua, Dk. Mwinyimvua amesema kuwa, ukusanyaji mapato unaweza kuongezeka kwa kuwaunganisha wateja wengi zaidi kadri iwezekanavyo.
“Sasa hivi mnazalisha umeme mwingi zaidi ya matumizi. Ongezeni jitihada za kuwaunganisha wateja wengi zaidi kwani ni kwa namna hiyo, mtafanikiwa kuongeza mapato ya Shirika.”

Amesema kuwa, ni matarajio ya Serikali kuona Shirika hilo linatengeneza faida kubwa itakayowezesha kutoa gawio serikalini.

Aidha, Dk. Mwinyimvua ameipongeza TANESCO kwa jitihada za kuboresha upatikanaji wa umeme lakini pia amelitaka Shirika kuongeza jitihada za makusudi kuhakikisha inazalisha umeme wa kutosha sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa nishati hiyo, ili kuwezesha azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda.

Amewataka wajumbe wa Baraza hilo, ambao wanawawakilisha wafanyakazi zaidi ya 6900 wa TANESCO nchi nzima, kujadili kwa kina namna ya kupambana na changamoto zinazolikabili Shirika ikiwemo wizi wa umeme, uharibifu wa miundombinu, ukatikaji wa umeme, ukuaji mdogo wa mapato ya Shirika, upotevu wa umeme na matatizo ya utoaji wa huduma ikiwemo uchelewaji katika kutatua matatizo ya dharura yanayowakabili wananchi.

Awali, akiwasilisha Hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, wakati wa Ufunguzi wa Mkutano huo; Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Wafanyakazi, Mhandisi Kahitwa Kashaija alisema kwamba hali ya makusanyo ya Shirika inaonesha kupanda ukilinganisha na mwaka 2017 ambapo mapato yamepanda kutoka wastani wa shilingi bilioni 146 hadi kufikia shilingi bilioni 158 kwa mwezi.

Aidha, alisema kwamba uwezo wa uzalishaji umeme umeongezeka, ambapo hadi kufikia Juni 2017 uwezo wa uzalishaji umeme kwenye gridi ulikuwa ni megawati 1263.6 wakati kwa sasa uwezo huo umeongezeka hadi kufikia takribani megawati 1600.
“Hii inajumuisha vituo nje ya gridi pamoja na wazalishaji wadogo wanaotuuzia umeme kwenye gridi na nje ya gridi.

Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi TANESCO ni wa siku tatu ambapo unatarajiwa kuhitimishwa Novemba 2, mwaka huu.